Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Faida za Kutembea

Faida za Kutembea

Faida za Kutembea

MAMILIONI ya watu hufikiri kwamba ikiwa hawawezi kujiunga na klabu fulani cha mazoezi na kutumia wakati mwingi humo, basi hawawezi kufanya mazoezi. Lakini hiyo si kweli. Dakt. Russell Pate wa Chuo Kikuu cha South Carolina anasema hivi: “Nafikiri tunapaswa kutambua kwamba inafaa kabisa kutembea baada ya mlo wa jioni.”

Lakini je, kutembea kuna faida? Je, kuna manufaa nyingi za kiafya?

Kutembea Huboresha Afya

Daktari Mgiriki Hippocrates aliona kutembea kuwa “dawa bora ya wanadamu.” Kwa hakika kuna msemo unaosema, “Nina madaktari wawili, mguu wangu wa kushoto na wa kulia.” Je, kweli kutembea huboresha afya?

Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba watu wanaotembea kwa ukawaida hawawi wagonjwa mara nyingi kama wale wasiofanya mazoezi ya kutembea. Uchunguzi huo unaonyesha kwamba kutembea hupunguza hatari ya kuugua ugonjwa wa moyo na kiharusi. Kunaweza kuzuia ugonjwa wa kisukari kwa kuboresha uwezo wa mwili wa kutumia insulini. Kunaimarisha mifupa, hivyo kuzuia ugonjwa wa mifupa. Kutembea humfanya mtu awe na nguvu na aweze kunyumbulika. Kunasaidia kupunguza na kudumisha uzito. Isitoshe, kutembea huboresha usingizi, huchochea ubongo, na kumsaidia mtu apambane na mshuko wa moyo.

Miaka kadhaa iliyopita, inasemekana kwamba watafiti katika Chuo Kikuu cha Southern California waligundua kwamba kutembea kwa dakika 15 humsaidia mtu apambane na mahangaiko na mfadhaiko kuliko dawa za kutuliza akili zenye nguvu ya kadiri! Kama mazoezi mengine ya mwili, kutembea hutokeza kemikali fulani za ubongo zinazopunguza maumivu na kumtuliza mtu, hivyo kumfanya awe na afya.

Kulingana na gazeti The Medical Post la Kanada, hata kutembea kwa starehe kunaweza kuleta faida za kiafya. Uchunguzi uliochapishwa katika gazeti The New England Journal of Medicine ulionyesha kwamba hata kutembea meta 800 kila siku, humsaidia mtu kuishi zaidi. Uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba kufanya mazoezi mara tatu kwa siku kwa vipindi vya dakika 10 hufaidi sawa na kufanya mazoezi kwa dakika 30 mfululizo. Hivyo unaweza kuegesha gari lako mbali kidogo na mahali unapoenda kisha utembee. Au unaweza kutembea kidogo mchana.

Unaweza kufaidika hata zaidi ukitembea haraka-haraka. Dakt. Carl Caspersen wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa huko Atlanta, Georgia, alisema hivi: “Kuanza kutembea haraka kwa nusu saa kwa siku kadhaa kila juma kunaweza kupunguza sana hatari [ya kuugua].” Jambo la kupendeza ni kwamba watu wa umri mbalimbali na wenye hali tofauti-tofauti za afya wanaweza kutembea. Isitoshe, si lazima uwe na ustadi maalumu au uzoefu fulani—unahitaji tu viatu vinavyofaa.

Furahia Kutembea

Valia mavazi yanayofaa na yasiyobana. Ukisikia baridi, vaa nguo ambazo ni rahisi kutoa. Tumia viatu vyepesi vilivyo na kisigino kifupi na vyenye nafasi kwa ajili ya vidole. Vinapaswa kuwa vikubwa kidogo kuliko vile vya kawaida. Ukitaka kutembea kwa zaidi ya nusu saa na hakuna maji njiani, itafaa ubebe maji kwenye kifaa chepesi. Pasha misuli joto kwa kutembea polepole kwa dakika tano za kwanza. Usijikunje unapotembea, na usikaze viwiko, magoti na mikono.

Baada ya kupasha misuli joto tembea kama kawaida na kwa haraka, huku kisigino kikikanyaga chini kwanza kisha vidole. Hivyo unapaswa kuvaa viatu vyepesi. Je, hayo ni mambo mengi sana? Usiwe na wasiwasi, watu wengi hutembea hivyo kwa ukawaida. Mwendo wako unapaswa kukuruhusu kuzungumza bila kuhema. Iwapo ni mara yako ya kwanza kufanya mazoezi hayo, ongeza muda unaotumia, umbali unaotembea, na mwendo wako hatua kwa hatua. Punguza mwendo unapokaribia kumaliza kutembea. *

Kwa kawaida, ongezeko la mpigo wa moyo, kupumua, na kutoka jasho kidogo huonyesha kwamba mtu amechoka. Huenda misuli ikauma na kulainika mwanzoni. Fuata ishara za mwili wako. Ukihisi unatembea kasi sana, punguza mwendo au upumzike kidogo. Lakini ukihisi maumivu au mkazo kifuani, moyo unapiga sana, unashindwa kupumua, kizunguzungu au kichefuchefu, acha kutembea na umwone daktari mara hiyo. *

Kwa kuwa kutembea ni mazoezi mepesi, kunafaidi mwili kuliko kukimbia na mazoezi mengine. Hivyo, si rahisi kuumiza viungo na misuli. Ama kwa hakika, kutembea ndiyo mazoezi ya kwanza kabisa yanayopendekezwa na wataalamu wa mazoezi. Kwa hiyo, ikiwa unataka kuwa na afya, tembea!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Wale wanaotaka kupunguza uzito wanaweza kuongeza mwendo wao kutoka dakika 12 kwa kilometa moja hadi dakika 9 kwa kilometa moja, hivyo kupunguza asilimia 30 zaidi ya kalori kila dakika. Kuongeza mwendo kutoka dakika 9 kila kilometa hadi dakika 7 kila kilometa, kutapunguza asilimia 50 zaidi ya uzito kwa dakika moja. Watu wengi wanaotaka kudumisha afya yao hutembea kilometa moja kwa dakika 7 hadi 9.

^ fu. 13 Labda itafaa umwone daktari kabla ya kuanza mazoezi hasa iwapo una ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu, au magonjwa mengineyo.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

MADOKEZO YA KUTEMBEA

● Usijikunje unapotembea, inua kidevu, tazama meta sita mbele

● Dumisha mwendo wa kadiri. Usitembee haraka sana kiasi cha kuhema na kushindwa kuzungumza kwa njia ya kawaida

● Usirefushe hatua zako. Ukitaka kuongeza mwendo wako, tembea hatua fupi haraka-haraka

● Peleka mikono mbele na nyuma, viwiko vikiwa karibu na mwili. Epuka kupeleka mikono kandokando

● Usikanyage chini kwa mguu wako wote mara moja. Kanyaga chini kwa kisigino kwanza, kisha uinue mguu kwa kutumia vidole

● Si lazima ubebe kitu kizito kwani kinaweza kukufanya usitembee kwa njia ya kawaida na kukaza misuli