Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Tunapenda Nguo Zetu”

“Tunapenda Nguo Zetu”

“Tunapenda Nguo Zetu”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

WAHISPANIA walipofika Mexico kwa mara ya kwanza katika karne ya 16, walipata watu wa makabila mbalimbali kama vile Waazteki, Wamaya, na wengineo. Je, makabila hayo yalimalizwa na Wazungu? La, yangalipo. Watu milioni 12 hivi nchini Mexico wametokana na makabila yaliyokuwapo kabla ya Christopher Columbus kuwasili Amerika. Wengi wao wanazungumza lugha zao za kale. Na mavazi yao yanawatofautisha.

Watu wanaoishi katika jimbo la kusini-magharibi la Oaxaca huvalia mavazi maridadi ya aina mbalimbali. Hilo ndilo eneo lenye makabila mengi katika Mesoamerika. Huko utapata watu wa kabila la Chontal, ambao hujiruzuku kwa kulima, kufuga ng’ombe, kuwinda na kukusanya chakula kwenye milima. Wao hupanda matunda, mboga, na maua mengi katika mashamba yao. Wao hushona maumbo mekundu na meusi ya wanyama na maua kwenye blauzi za wanawake, ikionyesha kwamba wanapenda mazingira. Wanawake waseja hufunga nywele zao kwa tepe za rangi mbalimbali.

Eneo la Tehuantepec ni makao ya watu wa Chontal, na vilevile makabila ya Huave na Zapotec ambayo huvaa mavazi yanayokaribia kufanana. Hata hivyo, wenyeji wanaweza kujua kabila la mwanamke kwa kutazama mavazi yake. Watu wa kabila la Zapotec, wanaosema kuwa walitoka kwenye mawingu, wanaweza pia kutambua kijiji ambacho mwanamke ametoka kwa kutazama jinsi alivyovaa nguo yake. Watu wa kabila la Chinantec, wanaoishi kaskazini mwa jimbo hilo, huvalia mavazi yenye madoido mengi zaidi. Wanawake wa kabila hilo huvalia marinda yenye madoido ambayo hayana mikono, nayo huonyesha utamaduni wao wa tangu kale. Wakati wa pindi rasmi, wao huvalia mavazi yenye madoido mengi yanayoitwa “tumbo kubwa” katika lugha yao.

Wanawake wa kabila la Mixtec, wanaoishi katika maeneo fulani ya jimbo la Oaxaca, Guerrero, na Puebla, hupenda pia kupamba nguo zao kwa nyuzi. Katika eneo moja, wanawake hupamba blauzi zao kwa mtindo unaoitwa “nitengeneze ikiwa unaweza.” Kama watu wengine wa Mexico, watu wa kabila la Mixtec wanaoishi pwani wangali wanatumia aina ileile ya kitambaa iliyotumiwa na mababu zao miaka mingi iliyopita. Unaweza kuona mtindo wao wa kisasa wa kufuma mavazi kwenye michoro na michongo iliyohifadhiwa kwenye majumba ya makumbusho, inayowakilisha wakazi wa eneo hilo kabla ya Wahispania kuwasili.

Nguo za wanaume wa kale Wamaya na Waazteki zilikuwa na madoido mengi. Leo, wanaume wa makabila mengi ya Mexico huvaa mavazi ya kisasa. Lakini, bado unaweza kuona watu wa makabila fulani wakivaa mavazi yaliyokuwapo kabla ya Wahispania kuwasili huko, kama vile kabila la Huichol. Nguo za watu wa Huichol zilizopambwa kwa uzi, huonyesha cheo cha mtu katika jamii na zina maumbo na madoido tata sana hivi kwamba utahitaji wakati mwingi kuyachunguza.

Unaweza kuona nguo zilizohifadhiwa vizuri zaidi za kabla ya wakati wa Wahispania katika makabila ya Nahuatl huko Cuetzalan katika jimbo la Puebla, ambako wanawake huvaa vitambaa kichwani ambavyo vimefungiliwa kwenye nywele zao (picha kwenye ukurasa wa 26) na vilevile quechquemitl shali nyepesi maridadi. Vitabu vya kale vinaonyesha mavazi hayo.

Kuna makabila mengi yanayoishi katika nyanda za juu za jimbo la Chiapas, na mengine yalitokana na ukoo mmoja. Katika eneo hilo, makabila ya Tzotzil, Tzeltal, na Tojolabal huvaa mavazi ambayo wanayaona kuwa ya kawaida lakini kwa mgeni yanavutia wee.

Watu wengi wa huko hujitengenezea vitambaa vyao. Bila shaka, huwezi kusahau kamwe utamaduni wako mama yako anapokufunza kujitengenezea nguo. Wanawake wa Tzotzil wanaoishi kwenye maeneo baridi ya mlimani huko Chiapas huchapa kazi ya kunyoa kondoo, kusafisha sufu, kuichana, kuisokota, na kuitia rangi za asili kabla ya kufuma nguo kwenye kitanda cha mfumi kinachofungiliwa kiunoni. Petrona, msichana anayeishi Chamula, anasema hivi kwa shauku: “Mwanzoni haikuwa rahisi, lakini nilifurahi nilipotengeneza nagua [skati] yangu ya kwanza ya sufu na kupamba blauzi ya pamba kwa nyuzi kwa mara ya kwanza. Hata nilijitengenezea mshipi.” Baada ya kutambua kazi ngumu inayofanywa, tunaelewa ni kwa nini anatuambia hivi: “Tunapenda nguo zetu.”

Katika maeneo ya Rasi ya Yucatán ambapo utamaduni umekolea zaidi, kila siku wanawake Wamaya huvaa hipil, rinda jeupe pana lililopambwa kwa nyuzi za rangi mbalimbali. Kwa kawaida, rinda hilo huvaliwa na kamisi yenye lesi. Katika pindi za pekee, wanawake na wasichana wa mashambani na mjini huvaa terno, vazi ambalo linafanana na hipil lakini lina madoido mengi zaidi.

Watalii wanaweza kuuziwa mavazi hayo ya Mexico kwa bei ghali sana. Lakini, hata ingawa wenyeji wengi ni maskini, wanaweza kuvaa mavazi hayo ya bei ghali kwa sababu wao huyatengeneza wenyewe.

Ukihudhuria mikutano ya Kikristo katika mojawapo ya makutaniko 219 ya Mashahidi wa Yehova nchini Mexico ambayo hufanywa katika lugha za kienyeji, utafurahia yale utakayoona. Kwenye pindi hizo, wahudhuriaji huvaa mavazi yao yenye madoido, urithi waliopata kutoka kwa mababu zao, nguo maridadi kwelikweli!

[Ramani katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

YUCATÁN

PUEBLA

OAXACA

CHIAPAS

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kamisi ya Wamaya

[Picha katika ukurasa wa 26]

Vazi la Zapotec

[Picha katika ukurasa wa 26]

Zapotec, Oaxaca

[Picha katika ukurasa wa 26]

Maya, Yucatán

[Picha katika ukurasa wa 26]

Nahuatl, Puebla

[Picha katika ukurasa wa 26]

Tzotzil, Chiapas