Kutambua Matatizo ya Kukosa Usingizi
Kutambua Matatizo ya Kukosa Usingizi
NYAKATI nyingine dalili za mtu zinaweza kuonyesha kwamba ana tatizo kubwa la usingizi. Kuna tatizo la kukosa usingizi ambalo hudumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na mara nyingi huhusianishwa na magonjwa mengine makubwa, kama vile kushuka moyo. Tatizo hilo linaweza pia kuwa dalili ya ugonjwa mbaya.
Kushindwa Kupumua Unapolala
Mario alikuwa na tatizo la kusinzia kupita kiasi mchana. Alipokuwa akiendesha gari lao, ilimbidi mke wake amtazame kwa uangalifu kwa kuwa *
alikuwa na zoea la kusinzia kwa ghafula na hakukumbuka jambo hilo. Alikoroma kwa sauti kubwa mara kwa mara kila usiku na wakati mwingine alishtuka na kuamka, huku akipumua kwa shida.Mario alikuwa na dalili za tatizo la kushindwa kupumua anapolala. Mtu anaweza kushindwa kupumua kwa sekunde kumi mpaka dakika mbili au tatu. Mara nyingi mtu mwenye tatizo hilo hupinduka-pinduka akipumua kwa shida kisha hurudi kulala, na tatizo hilo hujirudia mara nyingi sana kila usiku. Kuna aina tatu za tatizo hilo.
Tatizo la kwanza hutukia wakati ubongo hautoi ishara inayomwezesha mtu kupumua kikawaida. Katika tatizo la pili, sehemu ya kupitisha hewa iliyo nyuma ya koo huziba kabisa hivyo mtu hushindwa kupumua. Tatizo la tatu linahusisha tatizo la kwanza na la pili na huathiri watu wengi zaidi. Mtu aliye na mojawapo ya matatizo hayo ni kama mtu ambaye halali usiku kucha kila siku!
Huenda watu wenye matatizo ya kushindwa kupumua wanapolala wakawa hatarini kwa kuwa wanaweza kulala ghafula kazini au wanapoendesha gari. Huenda wakapata shinikizo la damu, moyo wao ukafura, na wakakabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kiharusi au moyo wao ukaacha kufanya kazi. Dakt. William Dement wa Chuo Kikuu cha Stanford, anakadiria kwamba Wamarekani 38,000 hufa kila mwaka kwa sababu ya madhara ya moyo yanayosababishwa na tatizo la kushindwa kupumua wanapolala.
Ingawa tatizo hilo huwapata sana wanaume wanene kupita kiasi waliozidi umri wa miaka 40, linaweza pia kuwapata watu wenye umri wowote, hata watoto. Kuna matibabu mbalimbali na yote yanapaswa kutolewa na daktari wa matatizo ya usingizi. Njia bora zaidi ya kutibu tatizo la kuziba koo mtu anapolala ambayo haihusishi upasuaji ni kutumia mashine ya kuingiza hewa mapafuni. Mgonjwa huvaa kifaa kinachodhibiti hewa (kilichorekebishwa na daktari ili kifae hali zake) kwenye pua usiku ili apate hewa inayohitajiwa kuzuia tatizo hilo. Ikiwa kifaa hicho hakisuluhishi tatizo hilo, kuna upasuaji mbalimbali unaoweza kufanywa, ambao unatia ndani kutumia miale ya leza au ya redio kuzibua koo.
Kusinzia Mchana
Tatizo lingine linalohitaji kutibiwa ni kusinzia sana mchana na linasababishwa na mfumo wa neva. Kwa mfano, Buck alikuwa akisinzia daima. Alikuwa analala ghafula hata wakati wa mikutano muhimu. Alianza kushikilia funguo mkononi ili zikianguka zimwamshe. Kisha magoti yake yalianza kulegea na alianguka aliposisimuka. Halafu alipokuwa akilala au kuamka mwili wake ulikufa ganzi na alianza kuona maono kabla tu ya kulala.
Tatizo la kusinzia mchana huanza mtu anapokuwa na umri wa miaka 10 mpaka 30. Nyakati nyingine watu wenye tatizo hilo huonekana kuwa timamu lakini hawatambui wakati ukipita. Ubaya wa tatizo hilo ni kwamba mara nyingi halitambuliwi kwa miaka mingi, *
huku mtu anayeugua akidhaniwa kuwa mvivu, kwamba anafikiri polepole, au anaonekana kuwa mtu asiyeeleweka. Kwa sasa tatizo hilo halina tiba, lakini dalili zake zinaweza kutibiwa kwa kiasi fulani kwa dawa na kufanya mabadiliko maishani.Magonjwa Mengine ya Usingizi
Magonjwa mengine mawili ambayo nyakati nyingine humpata mtu wakati mmoja, huathiri miguu na mikono na kumfanya mtu akose usingizi kabisa. Ugonjwa mmoja huifanya miguu ya mtu ishtuke-shtuke anapolala na nyakati nyingine mikono hufanya hivyo pia. Fikiria mfano wa Michael. Uchunguzi ulionyesha kwamba miguu yake iliposhtuka aliamka karibu mara 350 kila usiku!
Ugonjwa mwingine hufanya miguu isitulie, * na mgonjwa huhisi akitaka sana kusogeza miguu na magoti na hivyo hawezi kulala. Ingawa nyakati nyingine hali hiyo husababishwa na kukosa kufanya mazoezi au damu inaposhindwa kuzunguka kikamili, inaonekana wakati mwingine inasababishwa na kula na kunywa vitu vyenye kafeini. Pia kunywa kileo huongeza hali hiyo nyakati nyingine.
Ugonjwa mwingine ni ule wa kusaga au kukaza meno sana wakati mtu anapolala. Ukitokea kwa ukawaida, ugonjwa huo unaweza kuharibu meno na kusababisha maumivu makali ya taya, hivyo mtu hushindwa kulala kabisa. Kuna tiba mbalimbali kama vile upasuaji wa mdomo na kutumia kifaa cha kukinga meno usiku, ikitegemea kiwango cha ugonjwa.
Mazungumzo haya mafupi kuhusu magonjwa kadhaa ya usingizi yanaonyesha kwamba ni hatari kuyapuuza. Huenda matibabu yakawa sahili au tata, lakini mara nyingi ni ya lazima. Ikiwa wewe au mpendwa wako ana ugonjwa mbaya wa kukosa usingizi au dalili zake, inafaa kupata msaada wa kitiba haraka. Hata kama tiba haitaondoa matatizo kabisa, huenda ikapunguza sana hatari zinazohusika na kufanya hali hiyo iwe rahisi kuvumilia. Kisha, wakati ujao, wakati ahadi za Biblia zitakapotimia, “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’” Magonjwa yote yataondolewa kabisa Mungu atakapofanya “vitu vyote kuwa vipya.”—Isaya 33:24; Ufunuo 21:3-5.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Kukoroma kwa sauti kubwa wakati wowote ule ambapo koo limeziba ni tofauti na jinsi watu wengi hukoroma kidogo mara kwa mara na kuwasumbua au kuwaamsha wengine wanaolala.
^ fu. 11 Kwa habari zaidi kuhusu kusinzia mchana, ona gazeti la Amkeni! la Aprili 8, 1991, ukurasa wa 19-21, la Kiingereza.
^ fu. 14 Ona gazeti la Amkeni! la Novemba 22, 2000 kwa habari zaidi kuhusu ugonjwa huo.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Matibabu ya magonjwa ya usingizi yanapaswa kutolewa na daktari
[Picha katika ukurasa wa 10]
Huenda kukoroma kukawa dalili ya tatizo la kushindwa kupumua mtu anapolala
[Picha katika ukurasa wa 11]
Mara nyingi watu walio na ugonjwa wa kusinzia mchana hueleweka kimakosa kuwa wavivu
[Picha katika ukurasa wa 12]
Vifaa vinavyoingiza hewa mapafuni vinaweza kumsaidia mtu anayeshindwa kupumua anapolala