Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Utundu wa Nyani
Watu fulani wamesema kwamba nyani wengi sana wanaweza kuandika vitabu vyote vya Shakespeare wakipewa taipureta nyingi sana. Hivyo, watafiti katika Chuo Kikuu cha Plymouth nchini Uingereza waliwaachia nyani sita kompyuta moja kwa mwezi mmoja. Gazeti The New York Times linaripoti kwamba nyani hao “hawakuunda hata neno moja.” Nyani hao sita katika Bustani ya Wanyama ya Paignton, kusini-magharibi mwa Uingereza “walijaza kurasa tano tu,” zenye herufi nyingi za s. Mwishoni mwa kurasa hizo, nyani hao waliandika j chache, a chache, l chache, na m chache. Pia, walitumia kichapishi cha kompyuta hiyo kama choo chao.
Vipepeo Waliomo Hatarini
Mnamo Januari 13, 2002, milima ya Mexico ilikumbwa na dhoruba. Vipepeo wa monarch huhamia kwenye milima hiyo wakati wa baridi kali na kuishi katika misonobari. Dhoruba hiyo ilisababisha baridi kali, na inakadiriwa kwamba vipepeo milioni 500 walikufa kwa sababu ya unyevu na baridi na kurundamana karibu urefu wa meta 1 chini ya miti. Toleo la kimataifa la gazeti The Miami Herald lilisema: “Katika siku moja, asilimia 70 mpaka 80 ya vipepeo wote wa monarch ambao hurejea Mashariki ya Marekani katika majira ya kuchipua walikufa.” Lakini sasa huenda janga jingine likatukia. Licha ya juhudi za serikali ya Mexico za kuanzisha Mbuga ya Vipepeo wa Monarch, makao yao yanaharibiwa kwa sababu miti inakatwa isivyo halali. Karibu asilimia 44 ya mbuga hiyo imeharibiwa. Ijapokuwa viumbe hao hufaulu kusafiri umbali wa kilometa 4,000, tutaona kama wataendelea kuwepo makao yao ya majira ya baridi kali yanapoendelea kuharibiwa.
Wakulima Taabani
Gazeti New Scientist linasema kwamba kulingana na ripoti moja, “harakati za kuboresha uzalishaji wa chakula ulimwenguni pote zilisababisha tatizo moja: mamilioni ya wakulima maskini zaidi ulimwenguni wanaoishi barani Afrika walizidi kuwa maskini.” Jinsi gani? Kuanzia miaka ya mwishoni mwa 1950 na kuendelea, mbegu za hali ya juu za ngano na mpunga zilizalishwa ili kupunguza njaa iliyotarajiwa kwa sababu ya ongezeko kubwa la watu duniani. Hata hivyo, kwa kuwa chakula kingi kupita kiasi kilizalishwa, bei zilishuka. Gazeti New Scientist linasema: “Wakulima ambao wangeweza kununua mbegu hizo mpya waliepuka hasara kwa kuongeza mazao yao, lakini wale ambao hawakuweza walipata hasara.” Isitoshe, mbegu hizo mpya hazikufaa hali za Afrika kwa sababu zilibuniwa kwa ajili ya mashamba ya Asia na Amerika Kusini.
Madereva Wanaosinzia Ni Hatari!
Uchunguzi ulioripotiwa katika jarida Medical Journal of Australia (MJA) unasema kwamba “tatizo la madereva wachovu au wanaosinzia limeenea na ni tatizo kubwa katika jamii.” Kulingana na watafiti, “uchunguzi umeonyesha kwamba zaidi ya asilimia 20 ya misiba ya barabarani husababishwa na madereva wanaosinzia.” Ripoti ya jarida hilo inasema: “Misiba hiyo hutukia hasa dereva aliye peke yake anapoendesha gari kwa kasi usiku au wakati wa alasiri ambapo watu hulala kidogo. Kama ilivyo na misiba mingine ya barabarani, misiba inayosababishwa na kusinzia husababishwa na wanaume walio chini ya umri wa miaka 30.” Watu wanaokabili hatari kubwa zaidi ya kusinzia wanapoendesha gari ni wale wenye ugonjwa wa kuziba koo wanapolala. Jarida hilo linasema kwamba ugonjwa huo hukumba “asilimia 25 hivi ya wanaume wa makamo.” Watu wenye ugonjwa huo huenda wasitambue wakisinzia wanapoendesha gari.
Barafu Inayoyeyuka
Maji yalipopungua katika visima vya Punjab huko India kwa sababu ya mvua za msimu kuchelewa, maji ya Bwawa la Bhakra katika Mto Sutlej yaliongezeka karibu mara mbili zaidi ya kiwango cha mwaka uliotangulia. Kwa nini? Gazeti Down to Earth linasema kwamba kijito kikuu cha mto huo kinapitia eneo lenye mabamba 89 ya barafu. Syed Iqbal Hasnain wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru anaeleza: “Mabamba ya barafu yanayeyuka kwa sababu mvua ya msimu hainyeshi. Pia mabamba hayo yanayeyuka kwa sababu ya ukosefu wa mawingu, jua kali, na joto jingi sana.” Wataalamu wanasema kwamba maziwa hayo yanafurika mabamba yanapoyeyuka. Isitoshe, kuyeyuka kwa barafu huenda kukasababisha upungufu wa maji, na kuathiri uzalishaji wa nishati na kilimo.
Jitihada za Kujirembesha
Gazeti The Sydney Morning Herald linasema kwamba katika jimbo la New South Wales la Australia, “watu 2850 hupata kansa ya ngozi kila mwaka na 340 hufa.” Uchunguzi uliofanywa na Chama cha Kansa cha Victoria ulionyesha kwamba katika jitihada za kujirembesha, robo ya Waaustralia hujianika juani—hilo ni ongezeko la asilimia 10 katika miaka mitatu iliyopita. Gazeti hilo linaongeza hivi: “Kwa kusikitisha, watafiti wamegundua kwamba zaidi ya asilimia 60 ya vijana walijitahidi juu chini kugeuza ngozi yao na thuluthi moja wanasema kwamba kujianika juani huboresha afya yao.” Katika maduka makubwa mauzo ya mafuta ya kugeuza ngozi yaliongezeka kwa asilimia 18 mwaka uliopita, lakini mauzo ya mafuta ya kujikinga na jua hayakuongezeka. Dakt. Robin Marks wa Chuo cha Utaalamu wa Ngozi cha Australasian anasema kwamba watu fulani wanaamini kwamba kugeuza rangi ya ngozi polepole si hatari. Lakini kulingana na gazeti hilo, “madaktari wa kansa ya ngozi wanasema kwamba watu wanaoamini kwamba kujianika juani na hata kubadili rangi ya ngozi polepole si hatari, wamekosea sana.” Dakt. Marks anaonya hivi: “Kubadili rangi ya ngozi ni kama kuwa na sugu, huonyesha kuna kasoro fulani.”
Lugha ya Wajapani Imo Hatarini
Gazeti The Japan Times linaripoti kwamba maneno mengi ya kigeni yanaingia nchini Japan, na kuwafanya hasa Wajapani wazee wasiielewe lugha yao. Maneno ya kigeni, hasa ya Kiingereza, sasa yanafanyiza asilimia 10 ya maneno ya kamusi fulani. Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 60 analalamika hivi: “[Kijapani] hakieleweki siku hizi. Nyakati nyingine, mimi huona ninahitaji mtu anitafsirie lugha yangu.” Vijana, wanasiasa, vyombo vya habari, wanamichezo, wanamitindo, na wataalamu katika viwanda huyakubali maneno ya kigeni haraka, na “kuwafanya wajihisi wameendelea na ni wa kisasa.” Hata hivyo, maneno hayo bado huandikwa katika herufizakatakana, ambazo hutumiwa kuandika maneno ya kigeni. Hivyo, kulingana na gazeti hilo, maneno hayo “yatabaki yakiwa ‘mageni,’ labda kwa miaka mingi.” Kulingana na gazeti The New York Times, Wajapani wengine “wamekasirika kwa sababu sentensi nzimanzima zinaundwa kwa kutumia maneno ya Magharibi na labda kitenzi au neno moja tu la Kijapani.” Jambo hilo linafanya familia nyingi zaidi zishindwe kuwasiliana.