Mto Mkubwa wa Amazon Unawategemeza Mamilioni
Mto Mkubwa wa Amazon Unawategemeza Mamilioni
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI
NI MTO mkubwa sana ukilinganishwa na mito mingine. Unapita katikati ya msitu mkubwa zaidi wa mvua duniani. Watafiti wanasema kwamba ni muhimu kwa maisha duniani. Huwavutia sana wavumbuzi na wanamazingira. Kwa mamilioni ya Wabrazili, ni njia muhimu ya usafiri. Tunazungumzia Mto wa Amazon, ulio muhimu sana katika eneo la Amazon.
Kuuchunguza ‘Mto Ulio Kama Bahari’
Mto huo huanza ukiwa kijito katika Milima ya Andes ya Peru yapata kilometa 160 kutoka kwenye Bahari ya Pasifiki, kisha huungana na mito mingine na kushuka kwa mteremko wa meta 5,000 hivi hadi Bahari ya Atlantiki. Mto huo huitwa majina tofauti kabla haujaingia Brazili, ambako kwanza unaitwa Solimões. Karibu na Manaus, mto huo huungana na Mto Negro, ambao ndio mto mkubwa zaidi unaoingia humo, na hapo ndipo unapokuwa mto mkubwa wa Amazon.
Hapo ndipo maji hukutana kwa njia maridadi ya kustaajabisha. Maji ya kahawia ya Mto Negro na maji ya matope ya Solimões hukutana na kutiririka sambamba bila kuungana kwa umbali wa kilometa kumi hivi. Kuna mambo mbalimbali yanayofanya isiungane, kama vile vitu vilivyomo, uzito, na halijoto ya mito hiyo miwili.
Haijulikani mahali hususa ambapo Mto Amazon unaanzia na kuishia kwa sababu kumekuwa na ubishi kuhusu mito mikuu inayoingia humo na machimbuko yake na vilevile jinsi mto huo unavyoingia baharini. Inakadiriwa kwamba una urefu wa kilometa 6,750 kuanzia mlango wake wa mbali zaidi wa Pará ambao unatumiwa na meli. * Kulingana na chapa ya Brazili ya kitabu The Guinness Book of Records, kubaini urefu kamili wa Mto Amazon “hakutegemei vipimo bali kunategemea mahali ambapo unadhaniwa unaanzia na kuishia.”
Hata hivyo, ukubwa wa Mto Amazon hautiliwi shaka. Ni mkubwa kuliko Mto Mississippi, * Kiasi cha maji kinachoingia katika Bahari ya Atlantiki kutoka mto huo mkubwa ni zaidi ya meta 200,000 za mchemraba kila sekunde. Hivyo, maji ya mto huo yanayoingia katika Bahari ya Atlantiki ni asilimia 15 hadi 20 ya maji baridi yanayoingia katika bahari zote ulimwenguni. Kwa sekunde 30 tu, mto huo unaweza kuzima kiu cha wanadamu wote kwa siku moja—kila mtu kati ya wakazi bilioni sita wa dunia anaweza kupata lita moja!
Nile, na Yangtze ikiunganishwa.Maji hayo mengi baridi “husukuma” maji ya bahari na kuenea katika Bahari ya Atlantiki kwa umbali wa kilometa 200. Si ajabu kwamba Vicente Yáñez Pinzón, baharia Mhispania aliyeingia Amazon mnamo Juni 1500 alipoona mlango wa mto huo, aliuita Mar Dulce (Bahari ya Maji Baridi).
Wale wanaoabiri kwenye mto huo mkubwa huuona kuwa bahari katikati ya misitu. Katika sehemu nyingine ni mpana sana hivi kwamba mtu aliye kwenye ukingo mmoja hawezi kuona ukingo wa pili. Wakati wa mafuriko sehemu fulani za mto huo huwa na upana wa kilometa 50! Katika sehemu nyingine huwa na kina cha meta 50 hadi 80 kwa wastani, ikitegemea upana wake. Mto huo una kina cha meta 130 kwenye mji wa Óbidos katika jimbo la Pará, na ndiyo sehemu yake nyembamba zaidi.
Sehemu kubwa ya Mto Amazon huteremka kina cha sentimeta mbili baada ya kila kilometa. Mlango wake tambarare huruhusu mawimbi ya bahari yaingie ndani sana mtoni. Mawimbi hayo hufika hata Óbidos, kilometa 800 kutoka kwenye mlango wa mto huo.
Mto wa Amazon hupata majira ya kiangazi ya vizio vyote viwili vya dunia kwani unatiririka sambamba na ikweta. Maji hufurika kwenye mito yake ya ukingo wa kushoto kisha kwenye mito ya ukingo wa kulia. Maji yanapoongezeka na kupungua mtoni, kwanza kaskazini kisha kusini, mto wote wa Amazon hudundadunda kama moyo mkubwa. Kila mwaka, kina cha maji huongezeka au kupungua kwa meta 9 hadi 12. Mafuriko ni muhimu kwa kilimo cha eneo hilo. Kiasi kikubwa cha madini na mbolea yanayosombwa na mto na kuachwa kwenye kingo zake hurutubisha mashamba makubwa yaliyo bondeni.
Ni Nani Aliyeuvumbua, na Wakazi Walitoka Wapi?
Mvumbuzi Mhispania Francisco de Orellana ndiye aliyekuwa Mzungu wa kwanza kuabiri katika Mto Amazon na akaupa jina mnamo mwaka wa 1542. * Lakini kwa nini akauita Amazon? Orellana alidai kwamba aliona vita vya kikabila vya wapiganaji wanawake ambao walimkumbusha Waamazoni wanaotajwa katika hekaya za Wagiriki! Safari nyingine za uvumbuzi zilifanywa na Wahispania, Waingereza, Waholanzi, na Wareno. Kulingana na kitabu Enciclopédia Mirador Internacional, Wareno walifanya “mashambulizi mengi wakijaribu kunyakua [ardhi] kwenye kingo za [Mto] Negro, Solimões, na Branco na wakamiliki eneo hilo kwa mamlaka ya mfalme.”
Ili kuendelea kumiliki eneo hilo, Ureno ilituma mishonari huko. Kitabu hichohicho kinasema kwamba katika majaribio ya kueneza Ukatoliki na kusitawisha biashara ya “dawa za miti”—mbao, utomvu, mitishamba, na viungo—“washiriki wa dini walihamisha misheni zao mara nyingi kutoka eneo moja hadi jingine karibu na kingo za mto. Vijiji vingi vilisitawi katika maeneo hayo.”
Shughuli hizo zilizofanywa katika karne ya 17 na 18 na usitawi wa mashamba makubwa ya mpira mwishoni mwa karne ya 19 ulitokeza maeneo maalumu ya makazi. Kwa kuwa mito ilikuwa njia ya kawaida ya usafiri, watu waliishi kwenye kingo za mito, na kuanzisha miji midogo na vijiji. Watu wengi leo wanaishi katika miji ya kale sana iliyo katikati ya Amazon.
Watu Husafirije?
Bonde la Amazon, lenye ukubwa wa kilometa milioni sita za mraba, ndilo bonde kubwa zaidi la mto ulimwenguni. Ni kubwa kuliko bara lote la Ulaya bila Urusi. Mto Amazon wenye mito na vijito 1,100 hufanyiza mfumo tata wa usafiri unaoweza kulinganishwa na mfumo wa
mzunguko wa damu katika mwili wa mwanadamu, na Mto Amazon unaweza kulinganishwa na mshipa mkubwa zaidi wa damu unaoitwa aota. Mfumo huo wote wa maji unafanyiza sehemu mbili kwa tatu ya maji yote baridi duniani. Mfumo huo mkubwa wa mito na vijito wenye urefu wa zaidi ya kilometa 25,000 ni muhimu kwa usafiri na maisha ya wakazi wa eneo hilo.Mamilioni ya watu wanaokaa katika eneo la Amazon husafiri kupitia mto huo mkubwa. Meli za kila aina husafiri kwenye mto huo, kutia ndani meli kubwa zinazovuka Bahari ya Atlantiki ambazo husafiri umbali wa kilometa 1,500 hadi Manaus. Meli ndogo za mizigo na zile za abiria hufika Iquitos, huko Peru, kilometa 3,700 kutoka mlango wa mto. Sehemu kubwa ya rasilimali za Amazon husafirishwa kupitia Mto Amazon, na bidhaa kutoka sehemu nyingine za ulimwengu huja kwa njia hiyohiyo. Mto Madeira, wenye urefu wa zaidi ya kilometa 3,000, ambao ndio mto mrefu zaidi unaoingia katika Mto Amazon, hutumiwa sana katika shughuli za biashara. Biashara hizo nyingi hutokeza bidhaa za tani milioni mbili katika bonde la Amazon kila mwaka. Eneo lililo katikati ya Manaus na Belém, karibu na mlango wa mto, ndilo eneo lenye shughuli nyingi zaidi.
Maisha Yakoje Kwenye Kingo za Mto Huo?
Idadi kubwa ya watu wanaoishi karibu na mto inaonyesha kwamba wanautegemea kwa usafiri na wanapendelea udongo wenye rutuba bondeni. Kulingana na Altomir, mkazi wa eneo hilo, “watu wanaoishi karibu na mto wana mashamba madogo ambayo hasa ni ya mihogo na kwa kawaida wanapenda kula mihogo kwa samaki. Wao pia hupanda matikiti, ndizi, na mahindi na vilevile hufuga ng’ombe.” Lakini wakati wa mafuriko, ng’ombe hupelekwa haraka kwenye maeneo mengine, nyakati nyingine kwa vyelezo.
Ili kustahimili mabadiliko ya ghafula ya mto, nyumba zilizo karibu na mto hujengwa juu ya milingoti, na nyumba zinazoelea hujengwa juu ya vyelezo vinavyotiwa nanga karibu na miji.
Belarmino, msafiri wa kawaida kwenye mto huo, anasema kwamba wakazi “ni wakarimu sana na huwasalimu watu wasiowajua kwa tabasamu.”Ni kawaida kuona mitumbwi midogo ikikaribia meli kubwa ili kuuza na kubadilishana bidhaa au ili ivutwe mtoni. Mwendeshaji wa mtumbwi hutupiwa kamba, naye huifungilia kwenye mtumbwi. Mazao ya eneo hilo, kama vile mboga za mchikichi, mchikichi wa divai wa Brazili, mihogo, njugu, na samaki (kutia ndani kamba wa maji baridi), huuzwa au kubadilishwa kwa nafaka na bidhaa zilizotengenezwa viwandani.
Maelfu ya Wabrazili hutegemea mto huo kupata riziki kwa kusafirisha bidhaa na abiria. Pia hutumiwa kusafirisha mbao zinazopasuliwa ndani ya msitu.
Vyakula vingi vya protini vinavyoliwa katika eneo hilo hutoka kwenye mto huo. Chapa ya Kireno ya kitabu Vida Selvagem nos Rios (Makao ya Wanyama wa Porini) inasema: “Imekadiriwa kwamba Mto Amazon una aina 2,000 hivi za samaki, ambao ni wengi kuliko samaki walio katika mto mwingine wowote duniani.” Baada ya kutembelea eneo la Amazon, mtaalamu maarufu wa bahari Jacques-Yves Cousteau alisema kwamba ‘samaki walio katika Amazon ni wengi kuliko wale walio katika Bahari ya Atlantiki.’
Nguva mla-mimea, anayekabili hatari ya kuangamia, ni mmojawapo wa viumbe wanaoishi katika maji ya eneo hilo. Wengi hutamani sana kumnasa kwa kuwa nguva wa wastani anaweza kuwa na zaidi ya lita 100 za mafuta. Kwa wastani, mnyama huyo ana urefu wa meta 2.5 na uzito wa kilogramu 350 hivi. Isitoshe, kuna pirarucu, samaki mkubwa wa maji baridi anayeitwa pia chewa wa Brazili. Kwa wastani, ana urefu wa zaidi ya meta 2 na uzito wa kilogramu 70 hivi. Pomboo wa boutu, au pomboo wa Mto Amazon, na pomboo wa kijivu huwatumbuiza watu kwa kuibuka mtoni mara kwa mara.
Safari Isiyo ya Kawaida kwa Mashua
Mashua zimetumiwa kwa muda mrefu katika eneo la Amazon. Maelfu ya wakazi wanaouza mazao yao huko huzitegemea ili kupata riziki na huboresha maisha ya wakazi wa mbali wanaoishi karibu na mto huo. Pia, ni njia ya usafiri isiyogharimu pesa nyingi katika miji na vijiji vilivyo mbali sana na barabara. Abiria wengi hubeba bembea za kulalia wanaposafiri lakini hakuna nafasi kubwa ya kuzining’iniza. Ndiyo sababu watu hung’ang’ana kuingia mashuani ili wapate nafasi ya kuning’iniza bembea zao. Wengine husafiri katika sitaha ya chini ambamo mizigo mbalimbali huwekwa. Kwa kuwa wasafiri hupenda kuzungumza na kwa kawaida safari huchukua siku kadhaa, ni rahisi kupata marafiki.
Kuna meli na mashua nyingi karibu na Manaus kwa sababu ni bandari muhimu zaidi katika eneo la Amazon. Mazao ya maeneo mengi sana huletwa hapo, hata kutoka Peru, Bolivia, na Kolombia. Biashara ya utalii inasitawi pia, kwani watalii huja kutoka Amerika Kusini na sehemu nyingine za ulimwengu.
Safari Isiyosahaulika
Huenda utapata nafasi ya kutembelea eneo hili lenye kustaajabisha ambalo limewavutia wavumbuzi na bado lina vitu vingi ambavyo havijavumbuliwa. Zaidi ya kufurahia misitu maridadi ya mvua, mtu anayetembelea eneo la Amazon huchochewa kumheshimu Muumba wa vitu vyote kutia ndani mto huu mkubwa.—Zaburi 24:1, 2.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 7 Hivyo, urefu wa Mto Amazon unazidi ule wa Mto Nile kwa kilometa 80 kabla ya kujengwa kwa Bwawa la Aswan na hivyo Amazon ndio mto mrefu zaidi ulimwenguni. Uchunguzi mwingine unaonyesha kwamba urefu wake ni kilometa 7,100.
^ fu. 8 Mto Kongo, ulio magharibi ya Afrika ya kati, ndio mto wa pili kwa ukubwa. Hata hivyo, kila moja ya mito miwili mikuu inayoingia katika Amazon, yaani Negro na Madeira, humwaga maji mengi kama Mto Kongo.
^ fu. 14 Ona Amkeni! la Machi 22, 1997, ukurasa wa 3.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
MAWIMBI YA POROROCA
Katika mlango wa Mto Amazon, maji yake hukutana na maji ya bahari na kusababisha kishindo na uharibifu mkubwa sana. Mawimbi ya bahari huzuiwa na maji ya mto yanayotiririka kwa kasi. Maji ya bahari hujaa na kufurika katika mlango wa mto. Kisha, wimbi kubwa sana lenye nguvu huingia kwa kasi mtoni na kugeuza mkondo wa mto, kuvunja kingo za mto, kung’oa miti, na kusababisha uharibifu mkubwa. Mawimbi hayo makubwa yanayosababishwa na mikondo hiyo miwili yenye nguvu yanaweza kufikia urefu wa meta nne, na kishindo hicho kikubwa kinaweza kusikiwa mbali sana. Ni kishindo cha mawimbi ya pororoca.
[Ramani katika ukurasa wa 13]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ANDES
Chanzo cha Amazon
Machu Picchu, Peru
BONDE LA AMAZON
Iquitos, Peru
Amazon (Solimões)
MANAUS
Negro
Madeira
Óbidos
Amazon
Pará
BELÉM
[Hisani]
Globe: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 15]
1. Msichana wa eneo hilo
2. Nyumba zilizo juu ya milingoti kwenye kingo za mto
3. Maji meusi ya Mto Negro yakutana na maji yenye matope ya Solimões
4. Mto Negro huingia katika Amazon
[Hisani]
Photos 1 and 2: Ricardo Beliel / SocialPhotos; photos 3 and 4: Lidio Parente / SocialPhotos
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
1. Bandari ya Manaus
2. Abiria walalia bembea mashuani
3. Kuvua samaki kwa mtumbwi
[Hisani]
Photo 1: Lidio Parente/SocialPhotos; photos 2 and 3: Ricardo Beliel/SocialPhotos
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Sunset: Ricardo Beliel / SocialPhotos; surfer: AP Photo/Paulo Santos