Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Seville Lango la Kuelekea Amerika

Seville Lango la Kuelekea Amerika

Seville Lango la Kuelekea Amerika

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

KATIKA mwaka wa 1493, msafara wa meli 17 hivi ulifunga safari kutoka jiji la Cádiz la Hispania. Christopher Columbus alikuwa akianza safari yake ya pili ya uvumbuzi pamoja na mabaharia 1,500, watalii, makasisi, na wakoloni. Lengo kuu la safari hiyo lilikuwa kutawala mabara ya Amerika.

Baada ya safari hiyo ya kihistoria, jiji jingine la Hispania linaloitwa Seville, likawa lango la kuelekea mabara ya Amerika. Muda si muda, Seville likapata haki kutoka kwa mfalme ya kufanya biashara na makoloni hayo. Majahazi ya Hispania yaliondoka Seville na kurudi yakiwa yamebeba mikuo ya fedha kutoka kwenye migodi ya Bolivia, Mexico, na Peru. Baada ya miongo kadhaa, jiji hilo likawa mojawapo ya majiji makubwa na yenye ufanisi zaidi barani Ulaya. Na kumbukumbu za enzi hizo za kale bado zimo katika majengo ya kale ya Seville.

Ili kupanga biashara hiyo yenye kusitawi pamoja na Amerika, Mfalme Mhispania Philip wa Pili alijenga soko lenye kuvutia kando ya Mto Guadalquivir, ambapo wafanya biashara matajiri wangeweza kufanya biashara yao. (Askofu mkuu alikuwa amelalamika kwamba walikuwa wakifanyia biashara yao kwenye kanisa kuu.) Karne mbili baadaye jengo hilohilo likawa Hifadhi ya Indies, na leo maandishi yote kuhusu makoloni ya Hispania katika mabara ya Amerika yamehifadhiwa humo. *

Watafutaji wa hazina wanaotafuta majahazi yaliyozama bado hutembelea hifadhi hii ya Seville ili kuchunguza maandishi ya kale ya safari za meli. Hata hivyo, huenda wanahistoria wakapendezwa zaidi kuchunguza baadhi ya barua za kale za Christopher Columbus.

Mshale wa Kuonyesha Mwelekeo wa Upepo na Bustani ya Michungwa

Hata hivyo, Seville, lilikuwa na enzi nyingine ya ufanisi muda mrefu kabla ya kuvumbuliwa kwa Amerika, na mengi ya majengo yake yenye fahari yalijengwa wakati huo wa mapema. Kwa karne nyingi Wamoori, ambao wengi wao walitoka Morocco, walitawala maeneo makubwa ya Hispania. Katika karne ya 12, watawala wa ukoo wa Almohad walilifanya Seville kuwa jiji lao kuu, na wakati huo walijenga msikiti ambao mnara wake ungali unaelekeana na jiji la kisasa.

Wamoori walipofukuzwa Seville, wananchi waliubomoa msikiti huo wa jiji hilo ili kujenga kanisa la Seville, ambalo ni la tatu kwa ukubwa barani Ulaya (picha Na. 1). Hata hivyo, hawakutaka kuubomoa mnara wa msikiti huo uliokuwa maridadi sana, kwa hiyo, wakaufanya uwe mnara wa kengele wa kanisa, lililojengwa kando yake. Vipimo, matofali, na madirisha maridadi ya mnara huo huvutia sana kwenye kanisa hilo kubwa.

Miaka 500 hivi iliyopita, uharibifu uliosababishwa na tetemeko la nchi ulilazimu sehemu ya juu ya mnara huo irekebishwe, na mshale wa shaba wa kuonyesha mwelekeo wa upepo uliwekwa mahali palipokuwa na kuba ya awali. Mnara huo ukapata jina lake la Kihispania La Giralda kutokana na mshale huo (picha Na. 2), nao umekuwa jengo maarufu la Seville. Wageni wenye nguvu za kupanda Giralda hiyo mpaka juu wanaweza kuliona vizuri jiji lote.

Sehemu ya chini ya mnara wa kanisa hilo, kuna ua mdogo wa Wamoori uliokuwa sehemu ya msikiti wa awali, unaoitwa Patio de los Naranjos (Ua wa Michungwa). Nyua nyingi huko Andalusia zimetengenezwa kama ua huo uliopambwa kwa safu ya michungwa. * Na kwa kuwa barabara na bustani nyingi jijini Seville zina michungwa, wakati wa masika harufu ya michungwa inayochanua huenea katika jiji lote. Michungwa mingi ambayo ililetwa kwa mara ya kwanza na Wamoori bado imejaa jijini, na matunda yake hutumiwa kutengenezea jemu ya machungwa.

Wafanyabiashara wa Seville huutegemea sana Mto Guadalquivir, unaopitia katikati ya jiji. Mto huo uliliwezesha jiji hilo kuwa bandari kuu ya Hispania kuelekea Amerika na bado meli hutumia bandari hiyo. Kuna bustani nyingi kwenye kingo za mto huo karibu katikati ya jiji. Na katika ukingo mmoja kuna kumbukumbu nyingine ya enzi za Wamoori huko Seville, La Torre del Oro, ule Mnara wa Dhahabu.—Picha Na. 3.

Jina la mnara huo linatokana na wakati ambapo mnara huo ulikuwa umefunikwa kwa vigae vya rangi ya dhahabu. Hata hivyo, kusudi lake kuu lilikuwa ulinzi wala si mapambo. Wakati mmoja kulikuwa na mnyororo mzito kutoka katika Mnara wa Dhahabu hadi mnara-pacha mwingine uliokuwa ng’ambo ya pili ya mto, ambao uliwasaidia walinzi kudhibiti mashua zilizokuwa zikipita. Hapo ndipo meli kutoka Amerika zilikuwa zikipakua shehena zake za dhahabu na fedha. Siku hizi, badala ya yale majahazi yaliyokuwa yakipakua shehena yake mahali hapo, mashua za watalii ndizo hushusha abiria hapo kando ya Mnara wa Dhahabu.

Bustani, Nyua, na Vigae

Wamoori walijenga kasri na misikiti, na wakapanda bustani ili kuzipamba kasri zao. Kwa hiyo, Seville hujivunia kuwa na mojawapo ya kasri maridadi sana yenye bustani huko Hispania, inayoitwa Reales Alcázares, Kasri ya Kifalme (picha Na. 4). Kasri hiyo ilijengwa karne ya 12, lakini marekebisho makubwa yalifanywa katika karne ya 14. Hata hivyo, mtindo wa Kimoori umehifadhiwa na kwa kawaida wageni huvutiwa na jinsi vyumba na nyua zilivyopambwa kwa njia yenye kupendeza pamoja na matao, vigae vya rangi mbalimbali, na kuta zilizopigwa plasta kwa ustadi.

Kasri hiyo imezungukwa na bustani yenye kupendeza yenye mabubujiko na mitende. Mtawala Mmoori hata alichimba mfereji wa maji wenye urefu wa kilometa 16 ili kuhakikisha kwamba bustani yake imetiliwa maji vizuri. Kasri hiyo na bustani zake inavutia kwelikweli hivi kwamba familia ya kifalme ya Hispania imeitumia kuwa moja ya makao yake rasmi kwa miaka 700.

Kama tu vile michungwa hutokeza kivuli na harufu yenye kupendeza kwenye barabara za Seville, vigae vya rangi mbalimbali hufanya nyumba za jiji hilo ziwe za kipekee. Mtindo huo pia ulianzishwa nchini Hispania na Wamoori. Ilikuwa desturi yao kufunika kuta za ndani za vyumba vyao kwa vigae vilivyopambwa kwa michoro. Leo hii, vigae vya kupamba vya kila aina hurembesha upande wa nje wa nyumba, maduka, na nyumba za kifahari.

Mbali na vigae, kuna vitu vingine maridadi katika barabara nyembamba za Seville ya kale. Vizingiti vya madirisha na roshani ndogo zilizojaa maua ya jireniamu au waridi hupamba kuta zilizopakwa chokaa. Na kwa sababu ya hali nzuri ya hewa, maua huchanua karibu mwaka mzima, na kulifanya jiji liwe lenye kuvutia zaidi.

Matukio ya Kimataifa Jijini Seville

Katika karne iliyopita, matukio ya kimataifa yameimarisha uhusiano kati ya Seville na Amerika. Soko la Hispania, Plaza de España, (picha Na. 5), lilijengwa mwaka wa 1929 kwa ajili ya Maonyesho ya Kimataifa ya Hispania, na bado huwavutia watalii wengi. Upande mmoja wa soko hilo, kuna jengo kubwa lenye umbo la nusu duara ambalo kuta zake zina vigae maridadi vinavyowakilisha kila mkoa wa Hispania.

Katika mwaka wa 1992, karne tano tangu Columbus alipoabiri kuelekea Amerika kwa mara ya kwanza, Maonyesho ya Kibiashara ya Ulimwengu yanayoitwa Expo ’92 yalifanyiwa jijini Seville. Kupatana na kichwa cha maonyesho hayo, “Enzi ya Uvumbuzi,” kulikuwa na meli ya mfano inayotoshana na kufanana na ile meli ya Columbus (picha Na. 6), ambayo udogo wake uliwakumbusha wageni jinsi safari hizo za baharini zilivyokuwa hatari. Jengo jingine kwenye maonyesho hayo ya kihistoria, ambalo siku hizi ni jumba la makumbusho la sanaa, ni ile nyumba ya watawa iliyorekebishwa inayoitwa La Cartuja (picha Na. 7). Columbus alijitayarishia humo kwa ajili ya mojawapo ya safari zake za kuvuka Atlantiki na hapo ndipo alipozikwa mwanzoni.

Uwanja mpya wa Olimpiki wa Seville utatumiwa kwa ajili ya tukio jingine muhimu katika mwaka wa 2003—kusanyiko la kimataifa la Mashahidi wa Yehova. Pindi hiyo itawawezesha wajumbe kutoka Ulaya na Amerika kuijua Seville vizuri zaidi—lile lango la kuelekea Amerika.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Hifadhi hiyo ina hati milioni 86 na ramani na michoro 8,000.

^ fu. 11 Andalusia ni sehemu ya kusini kabisa ya Hispania, ambapo uvutano wa Kimoori uliodumu kwa karne nane hivi huonekana waziwazi.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Godo-Foto

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Godo-Foto

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Godo-Foto