Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kukata Mapezi ya Papa
Wafanyabiashara wavuvi ulimwenguni pote, wanatafuta papa baharini kwa bidii, wakikata mapezi yao na kutupa mizoga baharini. “Zoea hilo la kutisha la kukata mapezi huchochewa na biashara ya mchuzi ghali [wa mapezi ya papa],” laripoti gazeti Science News. Katika Agosti 2002, Walinzi wa Pwani wa Marekani walikamata meli ya Hawaii karibu na pwani ya Mexico baada ya kugundua kwamba ilikuwa imebeba tani 32 za mapezi ya papa. Hakukuwa na sehemu nyingine zozote za papa melini. “Shehena hiyo yenye kutisha inaonyesha kwamba angalau papa 30,000 waliuawa na kilo zipatazo 580,000 za papa zikatupwa,” lasema gazeti hilo. “Inakadiriwa kwamba ulimwenguni pote, meli za kuvua samaki huua papa milioni 100 kila mwaka.” Mapezi ya papa yanauzwa zaidi ya dola 200 kwa gramu 450 katika soko huria lakini kiasi kilichopo hakiwezi kukidhi mahitaji ya watu.
Kutumia Vizuri Wakati
Uchunguzi wa karibuni unaonyesha kwamba “watu ambao hulalamika kwamba hawana wakati wa kutosha hujidanganya,” laripoti The Australian. Gazeti hilo linataja uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha New South Wales na Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia na kusema: “Wengi wetu tunatumia muda mwingi isivyo lazima kazini na kufanya kazi za nyumbani.” Watafiti walihesabu muda ambao wenzi wa ndoa wasio na watoto wanahitaji kufanya kazi ili kupata riziki yao. Kisha wakalinganisha muda huo waliouhesabu na muda walioutumia kazini. Uchunguzi huo uligundua kwamba wenzi wa ndoa wasio na watoto “hutumia jumla ya saa 79 kila juma kazini, saa 37 wakifanya kazi za nyumbani na saa 138 wakijitunza, lakini wanahitaji tu kufanya kazi kwa saa 20 kila juma [saa 10 kila mmoja wao], na kutumia saa 18 wakifanya kazi za nyumbani na saa 116 wakijitunza [kutia ndani kula na kulala],” lasema gazeti hilo. Ikiwa wenzi wa ndoa wangekuwa tayari kupunguza muda wanaotumia, wangeweza kupata saa 100 za ziada kila juma. Kulingana na The Australian, uchunguzi huo waonyesha kwamba wenzi wa ndoa wanaofanya kazi na ambao hawana watoto “hudai hawana wakati hata kidogo, lakini kwa kweli, wao ndio wenye wakati mwingi zaidi kuliko watu wengine wote, nao wazazi ndio wenye shughuli nyingi sana.”
Ugonjwa wa Kisukari Waongezeka India
Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kwamba zaidi ya watu milioni 170 ulimwenguni pote wana ugonjwa wa kisukari. India ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wagonjwa—milioni 32—na idadi hiyo inatarajiwa kuzidi milioni 57 kufikia mwaka 2005, laripoti gazeti Deccan Herald. Kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu kisukari barani Asia, uliofanywa Sri Lanka, wataalamu walisema kwamba chakula na mabadiliko ya mtindo wa maisha ndivyo visababishi vikuu vya ongezeko hilo, pamoja na mkazo, kurithi kisukari, watoto kuzaliwa wakiwa na uzani mdogo sana, na kuwalisha kupita kiasi. India ni mojawapo ya nchi zenye gharama ya chini sana ya kutibu kisukari. Bado matatizo ya afya yanayohusiana na kisukari na kiwango cha vifo kingali juu, kwa kadiri fulani ni kwa sababu ya kutojua na kutopimwa ugonjwa huo mapema. Uchunguzi uliofanywa katika majiji makuu ya India ulionyesha kwamba asilimia 12 ya watu wazima wana ugonjwa wa kisukari na asilimia 14 hawawezi kumeng’enya sukari ifaavyo, ambayo ni dalili ya kwanza ya kisukari.
Maripota wa Vita Wapata Kihoro
“Idadi kubwa [ya maripota wa vita] walipata kihoro kwa sababu ya mambo waliyokabili na kuona,” lasema The New York Times. Gazeti hilo lilikuwa likitoa maelezo kuhusu “uchunguzi wa maripota wa kigeni [140] wa mashirika sita maarufu ya habari ambao huripoti kwa kawaida kuhusu vita na mapambano mengine.” Makala hiyo inaeleza kwamba “maripota hao wa vita walikuwa na kiwango cha juu sana cha kushuka moyo na mfadhaiko unaosababishwa na tukio lenye kutisha kuliko [kikundi cha maripota 107] ambao hawakuripoti kuhusu vita.” Dalili hizo “zilitia ndani kumbukumbu zenye kuogopesha, ndoto za daima za kutisha, kuchokozeka, kushindwa kukaza fikira na kukosa usingizi.” Tena, “maripota hao walikuwa na magumu mbalimbali ya kushirikiana na watu, . . . kutia ndani kushindwa kupatana na wananchi wa kawaida, kuepuka kuchangamana na marafiki, kushindwa kudumisha mahusiano na kunywa pombe ili kupumbaza akili.” Kwa wastani, wanaume na wanawake waliochunguzwa “walifanya kazi kwa miaka 15 katika nchi zenye vita kutia ndani Bosnia, Rwanda, Chechnya, Somalia na Afghanistan.”
Watu wa Ulaya Wanaozeeka
“Ulaya ya Kale inazidi kutimiza maana ya jina lake,” laripoti gazeti la Hispania El País. Katika karibu nchi zote za Muungano wa Ulaya, angalau asilimia 20 ya wakazi imepita umri wa miaka 60. Wachunguzi wa idadi za watu wanatabiri kwamba kufikia mwaka wa 2050, raia 4 kati ya 10 katika nchi kama vile Austria, Italia, na Hispania watakuwa na umri wa zaidi ya miaka 60. Mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yatahitaji kufanywa kwa sababu ya idadi hiyo inayoongezeka ya wazee, ukasema Mkutano wa Pili wa Ulimwengu Kuhusu Uzee, uliofanywa Madrid, Hispania. Haitakuwa rahisi kulipa marupurupu ya kustaafu na bima ya afya. Kwa mfano, huenda waajiri wakalazimika kuajiri wafanyakazi wenye umri mkubwa zaidi, wapangie ratiba za kazi zenye kubadilika-badilika au za zamu, au kupanga vipindi vya kustaafu. Zaidi ya hilo, “kwa kuwa kutakuwa na vijana wachache, kampuni zinazotaka kupanuka zitahitaji kuelekeza huduma zao na bidhaa zao kwa wazee,” asema Josep Maria Riera, mfanyabiashara Mhispania.
Elimu ya Ngono Yahitajiwa Sana Sasa
Kulingana na takwimu rasmi huko Ujerumani, kati ya mwaka wa 1996 na 2001, idadi ya mimba zilizotolewa iliongezeka kwa asilimia 60 kati ya wasichana wenye umri wa miaka 15-17 na kwa asilimia 90 kati ya wasichana wenye umri mchanga zaidi, laripoti Der Spiegel. Norbert Kluge wa Chuo Kikuu cha Koblenz-Landau, ataarifu kwamba huku watoto wakizidi kukomaa wakiwa na umri mchanga zaidi, ‘hawafundishwi ifaavyo kuhusu mambo ya ngono—hawafundishwi mapema vya kutosha.’ Watoto wanahitaji kujulishwa vizuri juu ya mambo ya maisha kabla hawajafika umri wa miaka kumi, lakini wazazi wengi wanaepuka daraka lao, asema Kluge. Kulingana na gazeti Berliner Morgenpost, mkurugenzi wa Baraza la Kiserikali la Wazazi huko Bonn, awashauri wazazi wazingatie hasa mambo ya kihisia, kama vile “upendo na mahusiano,” wanapofundisha watoto wao kuhusu ngono badala ya kukazia mambo ya kibiolojia.
Barua-Pepe na Stadi za Kuwasiliana
Watafiti wawili wanasema kwamba yaelekea waajiriwa watawasiliana na mfanyakazi mwenzao aliye kwenye orofa ileile kupitia barua-pepe kama tu wanavyowasiliana na wenzao wanaofanya kazi katika maeneo ya mbali sana, lasema gazeti Globe and Mail la Kanada. Akizungumzia jinsi barua-pepe inavyoweza kuathiri mawasiliano, David Crystal, profesa wa lugha wa Chuo Kikuu cha Wales, asema, “kujibiwa moja kwa moja ni sehemu muhimu ya mazungumzo,” na barua-pepe huzuia jambo hilo kwa sababu wakati unahitajiwa ili kupokea na kujibu ujumbe. Isitoshe, mwandishi wa barua-pepe anaweza kutawala mazungumzo bila kukatizwa. “Kupokezana zamu katika mazungumzo ni sehemu muhimu ya kuwasiliana,” lasema Globe.
Je, Kuna Seti Mbili za Neva?
Binadamu wana mfumo wa pekee wa neva unaoweza kutambua upendo na wororo, laripoti jarida la Ujerumani la kisayansi Bild der Wissenschaft. Wanasayansi Waswidi waligundua kwamba mwanamke mmoja aliyepoteza uwezo wake wa kugusa bado angeweza kuhisi msisimko wa kupendeza alipoguswa na brashi laini ya kupaka rangi. Waligundua kwamba msisimko huo ulitokezwa na seti nyingine ya neva iliyo katika ngozi, yenye nyuzi zinazopitisha mipwito polepole zinazoitwa tactile C. Nyuzi hizo hufanya kazi tu zinapoguswa kwa uanana na huchochea sehemu za ubongo zinazohusiana na hisia. Likieleza ni kwa nini huenda binadamu wana seti mbili za neva, gazeti International Herald Tribune lilisema hivi: “Nyuzi zinazopitisha mipwito polepole huanza kufanya kazi mapema sana maishani, huenda hata katika tumbo la uzazi, nazo nyuzi zinazopitisha mipwito haraka hukua polepole baada ya mtu kuzaliwa. Watoto waliozaliwa karibuni wanaweza kuhisi upendo katika mguso wa mzazi kabla ya kuweza kuhisi mguso wenyewe.”