Tumbo Lake Humwokoa!
Tumbo Lake Humwokoa!
HANA mwendo wa kasi. Watu wengi hawamwoni kuwa mwenye kuvutia. Lakini lo, ana tumbo kubwa sana! Ni nani huyo? Ni bunju mwenye miiba, pia huitwa puju na bunju-nungu. Gazeti Natural History linasema kwamba, kiumbe huyu “hubadilika sana” anapotishwa. Mwili wake ambao kwa kawaida hukua kufikia sentimeta 50, hufura “mpaka samaki huyo anapokuwa na ukubwa mara tatu kuliko kawaida, kama mpira mgumu wenye miiba. Ingawa umbo hilo halimsaidii kuogelea, humwokoa na maadui wake.”
Samaki huyo hujifurisha kwa kujaza maji tumboni, na kulifanya lipanuke karibu mara mia moja kuliko ukubwa wa kawaida! Bunju hufanya hivyo kwa kutumia mbinu rahisi sana—mikunjo yake.
Gazeti Natural History, laeleza kwamba tumbo la bunju huwa na mikunjo mingi sana. Mikunjo iliyo mikubwa zaidi ina upana wa milimeta 3 hivi na huwa “na mikunjo midogo ndani yake, na huendelea hivyo kufikia mikunjo midogo sana ambayo inaweza kuonekana tu kwa kutumia darubini,” makala hiyo ikasema.
Bila shaka, ni lazima ngozi ya bunju ipanuke tumbo lake linapofura. Ngozi yake ina tabaka mbili ambazo hupanuka kwa njia mbili tofauti. Tabaka la ndani lina mikunjo kama tumbo lake, lakini tabaka la nje huvutika kama mpira. Hali hiyo ya kuvutika huizuia ngozi kuwa na makunyanzi, ambayo yanaweza kupunguza mwendo wake majini anapoacha kufura.
Lakini bunju hufukuza maadui wake kwa njia nyingine mbali na kufura tu. Ngozi yake inapovutika, miiba iliyo kwenye ngozi husimama wima. Kwa hiyo umwonapo bunju unapoogelea baharini usimguse! Jihadhari pia na mdomo wake; anaweza kukuuma hadi mfupani!
Mungu alipomuuliza Ayubu maswali kuhusu uumbaji, Ayubu alijibu: “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.” (Ayubu 42:2) Naam, hata bunju mdogo mwenye miiba anayefurafura, asiyeweza kushinda mbio au mashindano ya urembo, huonyesha wazi nguvu na hekima ya Mungu ya uumbaji.—Waroma 1:20.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Top: Photo by John E. Randall; bottom: © Jeff Rotman