Kiwanda cha Kemikali Kilipolipuka
Kiwanda cha Kemikali Kilipolipuka
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA
SEPTEMBA 21, 2001, siku kumi tu baada ya majengo ya World Trade Center kushambuliwa huko New York, kulitokea mlipuko mkubwa sana ulioharibu viunga vya jiji la Toulouse, lililo kusini-magharibi mwa Ufaransa. Gazeti la Le Point la Ufaransa lilisema kwamba “huo ulikuwa msiba mbaya zaidi wa kiwanda uliowahi kutukia nchini Ufaransa tangu Vita ya Pili ya Ulimwengu.”
Tani 300 hivi za mbolea zililipuka na kufanyiza shimo kubwa lenye kipenyo cha meta 50 na kina cha meta 15. Mlipuko huo uliwaua watu 30 na kujeruhi zaidi ya watu 2,200. Nyumba 2,000 hivi zilibomoka na nyumba nyingine 27,000 zikaharibika kufikia umbali wa kilometa nane kutoka mahali pa mlipuko. Watu waliogopa sana kwa kuwa walidhani kimakosa kwamba mlipuko huo ulisababishwa na shambulizi la magaidi na kwamba gesi yenye sumu ilikuwa imeenea kutoka kiwandani.
Baadhi ya Mashahidi wa Yehova walijeruhiwa na mlipuko huo, na wengi waliathiriwa kwa njia nyingine. Upendo wa Kikristo uliwachochea Mashahidi wengine watoe msaada mara moja. (Yohana 13:34, 35) Habari ifuatayo yaonyesha jinsi msaada huo ulivyotolewa.
“Jengo Lote Lilibomoka”
Khoudir ni kati ya wafanyakazi wa kiwanda hicho cha kemikali walionusurika. Alipoteza fahamu alipogongwa na vifusi vilivyorushwa hewani na mlipuko, na taya lake likavunjika na mfupa wake wa begani ukateguka. Benjamin aliyefanya kazi karibu na kiwanda hicho alirushwa kutoka upande mmoja hadi mwingine ofisini na kubamizwa ukutani. Vipande vya vioo vilivyorushwa vilimkatakata na kulidunga jicho lake la kulia na kuathiri uwezo wake wa kuona. “Ninashukuru kwamba sikuketi kwenye meza yangu,” akasema. “Matofali yenye uzito wa kilogramu 600 yalianguka kwenye kiti changu.”
Alain, mwalimu mmoja wa shule iliyo umbali wa meta 200 tu kutoka kiwanda hicho alikuwa akipiga fotokopi mlipuko ulipotokea. Alisema hivi: “Jengo lote lilibomoka, ni vipande vya chuma tu vilivyobaki. Hakuna kitu kingine kilichobaki, wala kuta wala paa. Nilijeruhiwa na vipande vya vioo vilivyorushwa. Nilikuwa na majeraha makubwa usoni. Ni kana kwamba nilipigwa usoni kwa rungu.” Jicho moja la Alain lilipofushwa na uwezo wake wa kusikia ukaathiriwa.
Misaada Yatolewa Upesi
Mara moja wazee katika makutaniko 11 ya Mashahidi wa Yehova yaliyoathiriwa na msiba huo, waliwasiliana na kila mtu katika makutaniko hayo ili kujua waliojeruhiwa na hasara iliyotokea. Mashahidi wa Yehova waliojitolea walitumwa mara moja kuwasaidia waliohitaji msaada. Watu hao waliojitolea waligundua kwamba nyumba 60 za Mashahidi ziliharibika, nao wakasaidia kuhamisha familia kumi hivi. Watu waliojitolea walisaidia pia kurekebisha Majumba mawili ya Ufalme yaliyoharibika. Isitoshe, waliwasaidia kuomba malipo ya bima.
Catherine na Michel wanaishi karibu na kiwanda hicho. Catherine alikuwa akiendesha gari lake wakati wa mlipuko. Anaeleza hivi: “Kwanza tulidhani ni tetemeko la ardhi. Sekunde chache baadaye tulisikia mlipuko. Kisha tukaona moshi. Nilienda hadi mtaa wetu; ulionekana kama uwanja wa vita. Nyumba zote zilikuwa zimeharibika na madirisha ya maduka yalikuwa yamevunjika.
Watu walikimbia huku na huku. Wengine waliketi au kulala barabarani wakilia na kupiga mayowe. Madirisha yote, viunzi vya madirisha, na milango ya nyumba yetu ilikuwa imeng’olewa. Ndugu na dada zetu Wakristo walikuja haraka kutusaidia. Kufikia alasiri watu wa kutaniko letu walikuwa wamewasili wakiwa na ndoo na vifagio na plastiki za kufunika madirisha.”Alain na Liliane wanaishi pia karibu na kiwanda hicho. Mlipuko uliharibu kabisa nyumba yao. “Kila kitu kilivunjika-vunjika,” Alain akasema. “Kuta na vigae vilikuwa vimepasuka, na madirisha, milango, na fanicha zilikuwa zimeharibika. Hakuna kitu hata kimoja kilichobaki. Ndugu zetu Wakristo walifika mara moja ili kusaidia. Wakaondoa vifusi na walisaidia pia kusafisha vyumba vingine katika jengo hilo. Majirani wetu walishangaa kuona kwamba watu wengi walikuja kusaidia.” Asubuhi kabla ya mlipuko huo, Alain alipigiwa simu na mwanafunzi wa Biblia aliyemwomba aende ajifunze Biblia naye. Liliane alikuwa ameenda kushughulikia mambo fulani. Kwa hiyo hawakuwa nyumbani wakati wa mlipuko.
Mashahidi hawakuwasaidia watu wa kutaniko tu. Baada ya kuwasaidia wenzao, waliwasaidia majirani wao kuondoa vifusi kutoka katika nyumba zao na kufunika madirisha yaliyovunjika. Majirani walishukuru sana na walishangaa kwamba hawakutozwa malipo.
Mashahidi waliwasaidia pia watu wenye mamlaka wa eneo hilo kwa sababu walilemewa na uharibifu huo mkubwa. Mashahidi walisafisha shule na majengo mengine ya umma. Wenye mamlaka katika mtaa mmoja waliwatuma Mashahidi waliojitolea waende nyumba kwa nyumba ili kuona ni msaada wa aina gani ambao watu walihitaji.
Kutoa Msaada wa Kiroho
Mbali na msaada wa kimwili, Mashahidi wengi katika eneo la mlipuko walihitaji msaada wa kiroho. Hivyo, waangalizi wasafirio na wazee wa makutaniko ya karibu waliwatembelea wote walioathiriwa na msiba huo. Msaada huo ulithaminiwa sana. Catherine alisema hivi: “Wazee wote walikuja kutusaidia. Walikuja kututia moyo. Huo ndio msaada tuliohitaji zaidi kuliko msaada wa kimwili.”
Watu walitoa maelezo yenye kupendeza walipoona jinsi upendo wa Kikristo ulivyowasukuma kutoa msaada baada ya msiba. Shahidi mmoja aliyejeruhiwa vibaya alisema hivi: “Hatujui ya kesho. Ni lazima tumtumikie Yehova daima kana kwamba ni siku yetu ya mwisho.” (Yakobo 4:13-15) Shahidi mwingine alisema hivi: “Msiba huo umetusaidia kutambua kwamba hatupaswi kupenda mno vitu vya kimwili. Jambo muhimu zaidi ni kuwa kati ya watu wa Yehova.”
[Picha katika ukurasa wa 14]
Benjamin na Khoudir
[Picha katika ukurasa wa 14]
Alain
[Picha katika ukurasa wa 15]
Toulouse, siku iliyofuata mlipuko
[Hisani]
© LE SEGRETAIN PASCAL/CORBIS SYGMA
[Picha katika ukurasa wa 15]
Alain na Liliane