Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Amani ya Ulimwengu Makala “Je, Amani ya Ulimwenguni Pote Ni Ndoto Tu?” (Mei 8, 2002) iliandikwa vizuri sana. Inafaa wanasiasa wote waisome. Vichapo vyenu huelezea wazi mambo ambayo tunahitaji kujua na jinsi tunavyopaswa kuishi.
J. S., Jamhuri ya Cheki
Jitihada ya Kijana Sikuzote nilitaka kuwaambia kwamba mimi hufurahia kusoma magazeti yenu. Hatimaye nimeamua kuwaeleza jambo hilo baada ya kusoma makala “Jitihada Yake Ilileta Thawabu.” (Mei 8, 2002) Hivi majuzi niliona jambo linalofanana na lile alilosimulia Stella. Ninafurahi sana kujua kwamba kuna vijana ulimwenguni pote ambao wanamtanguliza Yehova maishani mwao kama mimi. Masimulizi kama hayo huwatia watu wote moyo, wazee kwa vijana.
L. P., Marekani
Wanyama Nimemaliza tu kusoma makala “Chui wa Ajabu wa Theluji.” (Mei 8, 2002) Ninapenda viumbe wote ambao Yehova ameumba, hasa wale walio na manyoya! Ninasikitika kujua kwamba chui wa theluji wamebaki wachache sana. Hebu wazia jinsi Yehova anavyohisi kuhusu jambo hilo.
D. R., Marekani
Hankul Nina umri wa miaka 13, na nilifurahia kusoma makala “Hebu Tujaribu Kuandika Hankul!” (Mei 8, 2002) Kwa muda wote ambao nimejua kusoma, nimependezwa sana na lugha za kigeni. Ninatumaini mtachapisha makala nyingi zaidi kuhusu lugha za kigeni wakati ujao!
B. J., Marekani
Nina umri wa miaka 11, na nilishangaa kujua kwamba maandishi ya Hankul yaweza kutumiwa hata katika lugha isiyo ya Kikorea. Jambo hilo ni rahisi kuelewa. Asante kwa kuchapisha makala hiyo!
J. I., Marekani
Buibui Nilisisimuliwa na makala “Buibui Anayejifanya Kuwa Chungu.” (Aprili 22, 2002) Jinsi Yehova alivyo Muumba wa ajabu! Ninatazamia kuishi katika ulimwengu mpya, ambapo nitaweza kujifunza mengi zaidi kuhusu vitu ambavyo ameumba.
P. P., Sri Lanka
Meli za Wafungwa Nimefurahia kusoma magazeti yenu kwa zaidi ya miaka 50. Hivi majuzi nilisoma makala “Kipindi Kibaya Sana Kwa Wafungwa Huko Australia.” (Aprili 22, 2002) Kwenye ukurasa wa 13, mlitaja kwamba meli ya wafungwa ya Uingereza iitwayo Amphitrite ilizama katika mwaka wa 1883. Nadhani mlikosea. Kulingana na utafiti wangu, meli hiyo kwa kweli ilizama mnamo Agosti 1833. Hilo lapatana na kipindi cha wafungwa kilichotajwa katika makala hiyo, ambacho kilimalizika katika mwaka wa 1868.
D. B., Scotland
“Amkeni!” lajibu: Kwa hakika chanzo chetu cha habari chasema kwamba meli ya “Amphitrite” ilizama katika mwaka wa 1833. Twaomba radhi kwa kosa hilo.
Vijana Huuliza Asanteni kwa kuchapisha makala “Vijana Huuliza. . . Nifanye Nini Nikikutana na Mwanafunzi Mwenzangu?” (Februari 22, 2002) Miaka mingi iliyopita nilikuwa mvulana mwoga sana kwa sababu nilikuwa na kigugumizi. Hilo lilifanya utumishi uwe mgumu kwangu, hasa nilipokutana na wanashule wenzangu. Ninajua makala hiyo itawasaidia sana vijana wengine.
W. T., Marekani
Ushauri Mzuri Asanteni sana kwa kututolea vichapo vyenye habari nyingi za kuelimisha. Makala zenu hugusia mambo mengi, na tofauti na vichapo vingine, nyinyi huandika mambo yasiyowashushia heshima watu wa dini nyingine. Gazeti la Amkeni! limekuwa mwandamani wangu wa karibu sana, chanzo cha ushauri mzuri ambao hunisaidia kuwa na tumaini ninapokabiliana na matatizo maishani.
N. P., Brazili