Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Zumari Imekuwepo Tangu Zamani

Zumari Imekuwepo Tangu Zamani

Zumari Imekuwepo Tangu Zamani

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

ZUMARI tunayoifahamu leo ya Maeneo ya Milimani ya Scotland—ambayo huchezwa huko Kanada, Marekani, Uingereza, na nchi nyingine zinazosema Kiingereza—ilivumbuliwa miaka 300 hivi iliyopita. Hata hivyo, ala hiyo ilianza kutumiwa maelfu ya miaka iliyopita katika jiji la kale la Uru, ambako Abrahamu alitoka, na Misri ya kale. Wasomi wamepata matete huko na kusema kwamba hayo yalitangulia zumari ya kisasa. Lakini haijulikani wakati mfuko wa hewa ulipoongezwa kwenye zumari na yule aliyeuweka.

Kitabu cha Biblia cha Danieli kilichoandikwa zaidi ya miaka 500 kabla ya Yesu Kristo kuzaliwa, kinataja majina ya ala sita za muziki za Wababiloni. (Danieli 3:5, 10, 15) Orodha hiyo ina neno la Kiaramu sum·pon·yah, ambalo limetafsiriwa “zumari” katika Biblia nyingi.

Ingawa hatuwezi kuwa na uhakika kuhusu jinsi ala hiyo ya kale ya Wababiloni ilivyokuwa, huenda ilifanana na zumari za nchi za Mashariki. Rekodi zinaonyesha kwamba katika Uajemi (Iran), India, na China, aina tofauti-tofauti za zumari zilitumiwa, na nyingine bado zapatikana hata leo.

Zumari Mbalimbali

Mwanahistoria Mroma Suetonius aliandika kwamba Maliki Mroma Nero alipotawala katika karne ya kwanza W.K., aliahidi kwamba iwapo angeendelea kuwa maliki angeweza kucheza “kinubi cha maji, filimbi, na zumari mfululizo.” Mnamo mwaka 37 W.K., karibu miaka 50 kabla ya Nero kuzaliwa, shairi lililodhaniwa kutungwa na Virgil lilitaja “zumari iliyotoa sauti tamu.”

Kuanzia nyakati za mapema zumari zilipatikana Hispania, Ireland, Italia, Poland, Ufaransa, na Ujerumani, na pia katika nchi za Balkan na Skandinavia. Zumari ilifikaje Uingereza? Inajulikana kwamba karibu mwaka wa 500 K.W.K., Waselti waliokuwa wakihama walileta aina fulani ya zumari nchini humo na kwamba mikoa mingi ya Uingereza ilikuwa na aina tofauti-tofauti za zumari zamani hizo kama vile Scotland. Hata kichapo The Oxford Companion to Music chadokeza kwamba “zumari ilijulikana huko Uingereza karne kadhaa kabla ya kujulikana Scotland.”

Majeshi ya Roma yalikuwa na wacheza-zumari, lakini hakuna uhakika kama Waroma walianza kucheza zumari baada ya kuvamia Visiwa vya Uingereza mwaka wa 43 W.K. au waliongezea tu kutumia zumari ambazo walikuta huko.

Ukizuru Scotland leo na upate kusikia sauti ya zumari ya Milimani ya Scotland ikipigwa katika bonde, bila shaka utakubali kwamba sauti hiyo yapendeza ajabu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Mnamo Agosti 2000, maelfu ya wacheza-zumari na wapiga-ngoma, waliotajwa kuwa “bendi kubwa zaidi ya wapiga-filimbi iliyowahi kuonekana,” walipanga gwaride katika barabara maarufu sana ya Princes huko Edinburgh ili kuchanga pesa za kusaidia hazina ya wagonjwa wa kansa (ona picha). Wachezaji hawakutoka tu Ulaya, Kanada, na Marekani, bali walitoka pia sehemu za mbali kama Hong Kong na Kisiwa cha Guam katika Bahari ya Pasifiki ili wajiunge na wenzao wa Scotland.

Zumari ya Milimani ya Scotland ndiyo zumari kuu ambayo imebaki miongoni mwa zumari zinazoonwa kuwa zilivumbuliwa Scotland. Aina nyingine ni zumari ya Maeneo ya Chini ya Scotland na zumari ndogo ya Scotland. Ala pekee ya Uingereza inayopatikana ni zumari ya Northumbrian. Hiyo hutoa sauti nyororo iliyo katikati ya ile ya clarinet na oboe. Tofauti na zumari ya Milimani, aina hizo tatu za zumari zina mifuko midogo ya hewa, ambayo mchezaji huinyambua kwa mikono, badala ya kutumia pumzi.

Katika kitabu The Bagpipe—The History of a Musical Instrument, mwandishi Francis Collinson arekodi hukumu hii iliyotolewa mwaka wa 1746 na mahakama ya Uingereza: “Kikosi [cha Scotland] cha Milimani hakijawahi kamwe kwenda vitani bila zumari,” na “hivyo kisheria, zumari ilionwa kuwa silaha.” Kwa kuwa hakuna ukoo uliowahi kwenda vitani bila filimbi, zumari ya Milimani ya Scotland ilipata umaarufu wa kuwa ala pekee ya muziki “kupigwa marufuku” ikionwa kuwa silaha.

[Hisani]

Colin Dickson

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

Zumari ya Milimani ya Scotland

Zumari ya kupuliza: Hii ni ya kupulizia na haiwezi kuruhusu hewa itoke. Imeunganishwa na mrija unaopeleka hewa mfukoni. Mchezaji hupuliza hewa mfukoni. Mfuko hufura na kisha yeye huufinya kwa mkono ili kuishinikiza hewa iingie ndani kwenye mvumo

Matete: Matete ya hali ya juu hutokana na mmea uitwao Arundo donax, ambao hukuzwa kwa kusudi hilo hususa nchini Hispania, Italia, na Ufaransa

Zumari ya kucheza muziki: Ina mashimo saba ya vidole upande wa mbele na shimo la kidole-gumba upande wa nyuma. Matete mawili hutoa sauti. Hewa ya kuicheza hutoka kwenye mfuko ulio chini ya kishikio cha mchezaji

Mvumo mzito: Ala hii hutoa mvumo mzito na inafanana na ile inayotoa mvumo mwepesi. Ina noti 16 upande wa chini

Vitegemezo: Mara nyingi hivi hutengenezwa kwa pembe za tembo, meno ya nyangumi, au mifupa, lakini leo plastiki hutumiwa pia

Zumari za mivumo myepesi: Ziko aina mbili. Tete moja huvuma ndani ya kila zumari, nazo hurekebishwa ili ziwe sawia, kila noti nane zikiwa chini ya filimbi

Mfuko: Tangu zamani mfuko huu umetengenezwa kwa ngozi ya wanyama, na mara nyingi hufunikwa kwa kitambaa cha tartan

Mbao: Mbao zenye rangi nyangavu zilitumiwa nyakati za mapema—hasa boxwood—halafu zilipakwa rangi nyeusi. Kisha, aina ya mpingo kutoka West Indies, ulio mzito na mgumu, ulitumiwa sanasana. Hata hivyo, mbao nyingine kama mpingo wa Kiafrika wa jamii ya Dalbergia melanoxylon zilitumiwa

[Picha]

Tete linalovuma

Tete la zumari

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mcheza-zumari Mskoti akiwa amevalia mavazi rasmi ya Milimani

[Picha katika ukurasa wa 24]

Zumari ya mazoezi: Mcheza-zumari hujizoeza kwa kutumia zumari hii, ikiwa ala tofauti