Tamaa ya Kusafiri Salama kwa Ndege
Tamaa ya Kusafiri Salama kwa Ndege
MAJUMA machache tu kabla ya Septemba 11, 2001, Alex aliona kuwa yuko karibu kushinda woga wake wa kusafiri kwa ndege. Ndege ya abiria ilipokuwa ikianza safari toka Athens kwenda Boston, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 42 ambaye ni meneja wa uhusiano mwema katika kampuni yao alianza kuwa na wasiwasi—moyo wake ulianza kupiga kwa nguvu na mikono yake na uso wake ukajaa jasho.
Lakini alijua kile alichopaswa kufanya. Mwalimu wake aliyekuwa akimsaidia kushinda woga wa kusafiri kwa ndege alikuwa amemwambia kwamba anapaswa kuvuta pumzi, kuwazia mandhari yenye kupendeza, na kushikilia kiti kwa nguvu, na kukiachilia mara nne kila dakika. Alipobabaishwa na mitikiso na makelele ya ndege, Alex aliwazia yuko kwenye pwani tulivu. Alex alisema: “Nilidhani kwamba nimefaulu sana kushinda woga wangu.”
Mamilioni ya abiria wameogopa kusafiri kwa ndege. Katika miaka ya hivi majuzi, wengi wameshauriwa na watu wa familia, waajiri, na mashirika ya ndege waende kwenye shule za kuwasaidia watu kushinda woga wa kusafiri kwa ndege. Abiria wengi walifanya maendeleo makubwa baada ya kuhudhuria mafunzo hayo, na katika vituo vingi asilimia 90 ya waliohudhuria mafunzo hayo walifaulu kushinda woga wa kusafiri kwa ndege.
Lakini matukio ya Septemba 11, 2001 yaliharibu mafanikio hayo. Alex aliacha kuhudhuria mafunzo hayo mara moja. Na mwajiri wake alihuzunika sana wakati Alex alipovunja mpango wa kusafiri kwa ndege ili akutane na mtu mmoja mashuhuri
ambaye angekuwa mteja wao. Alex alisema hivi: “Singeweza kustahimili woga wangu wa kusafiri kwa ndege pamoja na mashambulizi ya magaidi. Mafunzo niliyopata hayakunitayarisha kukabili mambo hayo.”Usalama Wachunguzwa
Wasafiri wa ndege wenye wasiwasi wanasema kwamba wateka-nyara wa Septemba 11, 2001 waliulizwa maswali yaleyale ambayo abiria huulizwa kawaida, kama vile: “Je, mtu yeyote usiyemjua amekuomba uingize kitu fulani katika ndege hii? Je, umekuwa ukiangalia mizigo yako yote tangu ulipoifungasha?” Pasipo shaka wateka-nyara hao walijibu: “La!” Baadhi ya wataalamu wa usalama wanaonelea kwamba kwa kuwa wateka-nyara hao walifaulu kuingia katika ndege ni wazi kwamba usalama katika usafiri wa ndege umepuuzwa. Jim McKenna, aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Usalama wa Ndege, alisema hivi: “Kabla ya tukio hilo hakuna mtu yeyote wala jambo lolote ambalo lingesababisha mabadiliko katika usalama. Lakini sasa kwa kuwa ndege nne zilitekwa nyara na kuharibiwa, na maelfu ya watu kuuawa, huenda mabadiliko yatafanywa.”
Baada ya maafa hayo mabaya ya ndege, usalama kwenye viwanja vya ndege na ndani ya ndege umechunguzwa sana. Kwenye kikao kimoja cha kamati iliyoteuliwa na Bunge la Marekani, Kenneth M. Mead, mkaguzi mkuu katika Wizara ya Uchukuzi ya Marekani, alisema hivi: “Licha ya hatua za usalama zilizokuwapo na zile ambazo zimechukuliwa sasa, bado kuna uzembe mwingi katika usalama na hali ya usalama inapasa kuimarishwa.” Ni hatua zipi zinazochukuliwa ili kuimarisha usalama?
Kuwakagua Wasafiri ili Kuondosha Hatari
Afisa mkuu wa usalama katika shirika moja kubwa la ndege huko Marekani, aliulizwa iwapo anaogopa kusafiri kwa ndege, naye akasema kuwa hababaiki hata kidogo. Alisema kwamba anaamini mfumo fulani wa kompyuta wa kuwakagua wasafiri. Mfumo huo hurekodi kila tiketi iliyouzwa na mashirika ya ndege ambayo yanautumia. Mfumo huo
huonyesha kama tiketi ilinunuliwa kwenye ofisi ya kuuza tiketi ya shirika la ndege, kwenye ofisi ya usafiri, au kwenye Internet. Mfumo huo hurekodi habari nyingine kama vile, iwapo mtu anasafiri peke yake au anasafiri na watu wa familia au na marafiki wengine, na vilevile iwapo amehusika katika uhalifu au amewahi kutenda mabaya kuelekea shirika hilo la ndege, wafanyakazi wake, au kuharibu mali zake.Kila mara abiria anaporipoti kwenye uwanja wa ndege, habari hizo huchunguzwa tena na habari mpya huongezwa, kutia ndani jinsi mtu huyo anavyojibu maswali ya ukaguzi. Habari hususa zinazokusanywa na jinsi zinavyochanganuliwa ni siri inayotunzwa sana na mashirika ya ndege. Mifumo mbalimbali kama hiyo hutumiwa ulimwenguni pote, huku mingine ikiwa imeunganishwa moja kwa moja na mashirika ya ujasusi ya kiserikali na ya kimataifa kama vile shirika la Interpol. Mifumo ya kukagua pasipoti kwenye viwanja vingi vya ndege huko Ulaya inaweza kurekodi na kuchunguza jinsi ambavyo abiria amekuwa akisafiri kutoka nchi moja hadi nyingine.
Uchunguzi huo hufanywa kwa sababu inadhaniwa kwamba watu wenye nia mbaya ni hatari kwa usalama kuliko mizigo inayoingizwa ndani ya ndege. Kwa hiyo, ili kuimarisha usalama kwenye viwanja vya ndege, vifaa mbalimbali vya kuwakagua watu vimeanza kutumiwa au vinachunguzwa.
Zaidi ya kupata habari kuhusu abiria, jambo jingine muhimu linalofikiriwa ili kuimarisha usalama kwenye viwanja vya ndege ni kuzuia vitu hatari visiingizwe ndani ya ndege. Uchunguzi unaofanywa kwa eksirei una mipaka. Wafanyakazi wa usalama kwenye viwanja vya ndege hushindwa kutazama picha za eksirei za mizigo kwa muda mrefu kwa sababu kufanya hivyo huchosha. Wakati huohuo, vifaa vinavyotambua vitu vya chuma huwapumbaza wafanyakazi hao tena na tena, kwa sababu vinatambua funguo, sarafu, na vishikizo vya mishipi.
Sheria Kali Zaidi
Ili kushinda vizuizi hivyo, serikali mbalimbali zimetunga sheria za kuimarisha usalama kwenye viwanja vya ndege. Nchini Marekani sheria hizo, ambazo zinapasa kuanza kutekelezwa kufikia mwishoni mwa mwaka 2002, zinasema kwamba mizigo haitaingizwa ndani ya ndege ikiwa mwenyewe hayupo, mizigo itakaguliwa kabisa kabla ya kuingizwa ndani ya ndege, na mizigo iliyokwisha kukaguliwa itachunguzwa tena ili kuhakikisha hakuna vilipukaji vyovyote. Milango ya chumba cha rubani inaendelea kuimarishwa na kufanywa kuwa salama zaidi. Wafanyakazi wa mashirika ya ndege wanapewa mazoezi ya ziada kuhusu hali za dharura. Maafisa wa serikali wenye silaha wa kupambana na wateka-nyara wamewekwa katika ndege za abiria.
Kwa majuma na miezi kadhaa baada ya Septemba 11, 2001, abiria walichunguzwa na mizigo ikakaguliwa kwa mkono katika viwanja vingi vya ndege ulimwenguni. Nyakati nyingine, abiria walichunguzwa mara mbili na mizigo pia ikakaguliwa mara mbili. Wasafiri huko Ulaya hawakuona jambo hilo kuwa jipya, kwani hatua kama hizo za tahadhari zilichukuliwa katika maeneo mengi huko katika miaka ya 1970 wakati utekaji nyara ulipokuwa umechacha. Sasa abiria hawaruhusiwi kuingiza vifaa vyovyote vyenye ncha kali ndani ya ndege. Wasafiri walio na tiketi pekee ndio wanaoruhusiwa kupita
kwenye vituo vya ukaguzi. Sasa watu wengi wamezoea zile foleni ndefu kwenye vituo vya ukaguzi na kuwaona wanajeshi wenye silaha kwenye viwanja vya ndege.Umuhimu wa Kufanya Marekebisho ya Ndege Wakaziwa
Hebu wazia tukio hili linalotukia mara kwa mara: Baada ya kupita kwenye vituo vingi vya ukaguzi kwenye uwanja wa ndege, abiria anafika mahali pa kungoja kabla ya kuingia ndani ya ndege na kumsubiri mwakilishi wa shirika la ndege atangaze kwamba ni wakati wa kupanda ndege. Kisha abiria mwingine karibu naye aliyevalia suti yenye rangi ya kijivu anamwambia: “Umesikia? Ndege itachelewa kwa sababu ya hitilafu za kimitambo.” Akiwa amevunjika moyo, abiria wa kwanza anaongeza hivi: “Natumai ndege hiyo itakuwa shwari tunapoondoka.”
Abiria wengi hawafahamu kwamba mashirika ya ndege hutumia muda mwingi na jitihada nyingi kukagua ndege kabisa. Marekebisho yanayohitajiwa hujulikana kwa kuchunguza kitabu kinachoonyesha safari na mambo yanayoipata ndege hususa. Ama kweli, mashirika hayo husisitiza na kuhakikisha kwamba ndege na injini zinakaguliwa kabisa na kurekebishwa kulingana na ratiba ya kufanya matengenezo hata kama ndege haijawahi kuharibika. Ndege hukaguliwa na kurekebishwa mara nyingi kuliko gari.
Afisa mmoja wa kurekebisha ndege katika shirika moja kubwa la ndege anathibitisha hilo. Anasema hivi: “Nimefanya kazi hii kwa karibu miaka 15 na sijawahi kuona wala kuzungumza na mtu yeyote anayefanya kazi ya kurekebisha ndege ambaye hachukui usalama kwa uzito sana. Isitoshe, marafiki na familia za wafanyakazi hao hutumia ndege hiyohiyo wanayorekebisha, kwa hiyo hawafanyi mambo kiholela.”
Mafundi wa ndege wana wajibu mkubwa sana. Mmoja wao anasema: “Sitasahau usiku ule ambao ndege yetu aina ya DC-10 ilianguka huko Sioux City, Iowa. Wakati huo nilikuwa fundi wa kurekebisha mitambo ya ndege, na nilikuwa nimepewa kazi ya kukagua na kufanya marekebisho fulani kwenye sehemu ya nyuma ya ndege nyingine ya aina hiyo. Wakati huo, hatukuwa tumepokea habari za kutosha kuhusu ndege iliyoanguka. Nakumbuka kwamba usiku huo nilifanya kazi kwa makini sana, nikijiuliza, ‘Ndege hiyo ilipatwa na nini? Je, fundi mwingine alikosa kutambua kasoro fulani ambayo huenda nikiigundua sasa nitaweza kuzuia msiba mwingine kama huo? Je, ninafanya kila kitu ipasavyo?’ Jioni hiyo, nilitumia muda mrefu kwenye sehemu ya nyuma ya ndege nikifanya ukaguzi huku nikiwaza na kuwazua.”
Mafundi wa ndege huzoezwa mara nyingi jinsi ya kushughulikia mambo yote kuhusu kazi yao, iwe ni kufanya ukaguzi wa kawaida, ukaguzi kamili, ama kugundua na kurekebisha hitilafu. Kila mwaka, mitaala ya kuwazoeza mafundi wa ndege huwa na mafunzo mapya ili kushughulikia hali zote zinazoweza kutokea, ziwe ni hali za kawaida au zisizo za kawaida.
Ndege inapoanguka, habari zinazokusanywa huchanganuliwa na kuingizwa katika kifaa ambacho huiga hali zinazotukia wakati wa kuendesha ndege. Marubani wanaofanya majaribio ya ndege na wahandisi wa ndege hutumia kifaa hicho kutafuta masuluhisho mengine ili
mafundi waweze kushughulikia vizuri matatizo kama hayo wakati ujao. Halafu, mafunzo yanayohusu matatizo hayo hupangwa ili mafundi wa ndege wapewe mwongozo hususa. Kwa kutegemea uchunguzi huo kuhusu hitilafu zinazotokea, miundo ya ndege na pia miundo ya sehemu mbalimbali za ndege hubadilishwa. Hivyo, mafundi hujifunza mambo muhimu kutokana na kasoro hizo wakitumaini kwamba habari hizo zitapunguza misiba.Fundi mmoja wa ndege anamalizia hivi: “Sisi huambiwa kwamba ‘usalama haujitokezi wenyewe—lazima utokezwe kupitia mpango maalumu.’”
Kusafiri Tena kwa Ndege
Baada ya kukataa kusafiri kwa ndege kwa miezi minne, Alex aliamua kupambana na woga wake. Ijapokuwa polisi na wanajeshi walikuwapo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Logan huko Boston, yeye hakubabaika. Hakuona ubaya wowote kupanga foleni ndefu wala mizigo yake kukaguliwa.
Alex aliona hatua hizo kuwa dalili zenye kutia moyo kwani anatamani sana usafiri wa ndege uwe salama. Bado yeye ana wasiwasi kidogo. Hata hivyo, anapopakia mfuko wake uliokaguliwa ndani ya ndege, anasema hivi: “Sasa ninahisi afadhali zaidi.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]
Mambo Fulani Kuhusu Usafiri wa Ndege
Kulingana na makadirio fulani, asilimia 20 ya abiria huogopa kusafiri kwa ndege. Hata hivyo, si wote wanaona kwamba kusafiri kwa ndege ni hatari. Mara nyingi, wasiwasi wao husababishwa na mambo mengine wanayoogopa kama vile kuwa mahali palipo juu sana au katika sehemu zenye watu wengi.
[Chati katika ukurasa wa 8]
UWEZEKANO WA KUPATA MSIBA
Katika mwaka Katika maisha yako
ni 1 kati ya: ni 1 kati ya:
Gari 6,212 81
Mauaji 15,104 197
Mashine 265,000 3,500
Kuanguka kwa ndege 390,000 5,100
Beseni ya bafu 802,000 10,500
Wanyama na mimea yenye sumu 4.2 million 55,900
Radi 4.3 million 56,000
[Hisani]
Chanzo: National Safety Council
[Picha katika ukurasa wa 6]
Usalama umeimarishwa kwenye viwanja vya ndege
[Hisani]
AP Photo/Joel Page
[Picha katika ukurasa wa 7]
Abiria wanachunguzwa na kukaguliwa
[Picha katika ukurasa wa 7]
Marekebisho mengi zaidi ya ndege yanafanywa
[Picha katika ukurasa wa 8]
Marubani wamepata mazoezi ya hali ya juu