Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Dhahabu Nyekundu” ya Mediterania

“Dhahabu Nyekundu” ya Mediterania

Dhahabu Nyekunduya Mediterania

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

WAKATI mmoja wasomi kadhaa walisema kwamba kitu hicho ni mboga na wengine wakasema kwamba ni madini. Kwa muda mrefu, watu wamevutiwa na rangi yake nyangavu. Kwa karne na miaka, kitu hicho kimetumiwa kama pambo, kimetumiwa katika kazi za sanaa, kimetumiwa kama talasimu, dawa, na hata pesa. Leo, kinatumiwa hasa kutengeneza vito. Ni kitu kipi hicho? Ni marijani ya Mediterania—ambayo ni yenye thamani kubwa sana hivi kwamba inaitwa dhahabu nyekundu.

Marijani ni nini, hupatikana wapi, na hufanyizwaje? Ni mbinu zipi zinazotumiwa kuikusanya? Ilitumiwaje hapo kale? Na inatumiwaje leo?

Je, Marijani Ni Mnyama, Mboga, au Madini?

Wataalamu wa kale wa elimu ya viumbe walieleza mengi kuhusu marijani ya Mediterania (Corallium rubrum), jinsi ilivyokusanywa, na jinsi ilivyotumiwa. Kabla ya karne ya 18 watu hawakujua kwamba marijani ni mizoga ya wanyama wadogo. Mtu anapoona marijani anaweza kufikiri kwamba ni maua ya mti mdogo na kumbe maua hayo ni minyiri ya viumbe, naam, makundi ya wanyama wadogo. Minyiri hiyo yenye kalisi, ambayo ina urefu wa sentimeta 25-30 hivi, hufanyizwa na makundi ya viumbe hao ili kujilinda. Minyiri yote hiyo ina rangi moja tu, lakini mingine ina aina mbalimbali za rangi nyekundu. Marijani inaweza kukua mahali popote pagumu—iwe ni mwambani, penye meli iliyovunjika, au hata penye tufe kuukuu la mzinga—kufikia kina cha meta 250. Hata hivyo, ili marijani inawiri inapaswa kuwa kwenye bahari zisizochafuliwa zenye chumvi nyingi na maji yenye joto la nyuzi 10 hadi 29 Selsiasi. Marijani hupatikana kwenye sehemu mbalimbali za Bahari ya Mediterania huko Albania, Algeria, Hispania, Italia, Morocco, Tunisia, Ufaransa, Ugiriki, na Yugoslavia na kwenye sehemu mbalimbali za Bahari ya Atlantiki huko Cape Verde na Morocco. Inakadiriwa kwamba urefu wa makundi ya marijani ndogo huongezeka kwa milimeta 4 hadi 8 kwa mwaka na kipenyo huongezeka kwa milimeta 1.5 hivi kwa mwaka.

Imekuwa Yenye Thamani Kubwa Tangu Kale

Vitu vilivyochimbuliwa vinaonyesha kwamba marijani imethaminiwa kwa muda mrefu, imetumiwa kutengenezea vitu na imeuzwa. Hapo awali, yaonekana kwamba watu walikuwa wakikusanya tu minyiri ya marijani iliyokuwa imesukumwa na maji hadi kwenye fuo za Mediterania. Masalio ya marijani, ambayo labda yalitumiwa kama hirizi, yamepatikana katika makaburi ya kale huko Uswisi. Marijani ilikuwa miongoni mwa vito vya mungu mmoja wa Wasumeria. Wamisri waliiona kuwa yenye thamani sana. Wayahudi wa kale waliiona kuwa yenye thamani kama vile fedha na dhahabu safi. (Mithali 8:10, 11; Maombolezo 4:7) Na Waselti waliihazini sana kwani waliitumia kupamba silaha zao na hatamu za farasi.

Mtaalamu wa elimu ya viumbe aliyeitwa Pliny anaripoti kwamba katika karne ya kwanza W.K., marijani ilikusanywa karibu na Sicily na vilevile kwenye Ghuba ya Lions, iliyo kwenye pwani ya magharibi ya rasi ya Italia. Makundi ya marijani yalikusanywa kwa nyavu au kukatwa kwa chuma zenye makali. Wakati huo, marijani ilionwa kuwa dawa ya homa, vijiwe vya figo, na magonjwa ya macho. Pia, watu walioimiliki walifikiri kwamba ingewalinda dhidi ya tufani na radi.

Kufikia karne ya kumi W.K., Waarabu wa Afrika Kaskazini walikuwa wamevumbua kifaa cha kukusanya marijani. Kifaa hicho kilitengenezwa kwa milingoti miwili mikubwa iliyokingamana, yenye urefu wa kati ya meta 4 na meta 5 hivi. Kifaa hicho kiliimarishwa kwa jiwe zito na kilikuwa na nyavu mbalimbali, nyingine zenye urefu wa meta 8, katikati na kandokando. Kifaa hicho kiliingizwa ndani ya sakafu za bahari zenye marijani kutoka kwenye mashua na kukokotwa. Minyiri ya marijani ilivunjwa, ikanaswa nyavuni, na kuvutwa juu. Vifaa tofauti-tofauti vya aina hiyo viliendelea kutumiwa hadi miaka michache tu iliyopita ambapo ilisemekana kwamba vilikuwa vinaharibu sakafu ya bahari na kuangamiza viumbe wa baharini. Hivyo, zoea hilo likapigwa marufuku na wapiga-mbizi wakaanza kutumiwa kukusanya marijani. Inasemekana kwamba wapiga-mbizi wanaweza kuteua marijani ipasavyo bila kuwaangamiza viumbe wengi wa baharini, lakini ukweli ni kwamba wapiga-mbizi wengine wanaweza kumaliza marijani baharini.

Sanaa ya Kale Nchini Italia

Wasanii wa kale huko Roma walitengeneza hirizi, shanga za mikufu, na sanamu zilizowakilisha dhana mbalimbali na maumbile. Kufikia karne ya 12, kulikuwa na ufanisi mkubwa katika biashara ya kuuza shanga, vifungo, na vitu vingine kati ya Genoa na Constantinople na bandari mbalimbali za Mediterania. Katika karne ya 13, watu huko India na katika sehemu nyingine za Kusini-Mashariki mwa Asia walipenda marijani ya Mediterania sana, na wafanyabiashara Waarabu waliipeleka hadi China.

Majiji fulani kutia ndani Trapani, Naples, na Genoa, yalitengeneza mapambo mengi laini. Katika karne ya 16 hadi ya 18, mapambo kutoka Trapani yalikuwa yenye kuvutia sana kwani vitu vingi vya mbao na chuma vilifunikwa kwa dhahabu na kutiwa vipande vidogo vya marijani vyenye maumbo mbalimbali. Vitu hivyo vilitia ndani makasha ya vito, sinia, fremu za picha, vioo, na mapambo ya makanisa. Sanamu zilizoonyesha kuzaliwa kwa Yesu zilitengenezwa kwa marijani, na maelfu ya shanga ndogondogo za marijani zilishonelewa kwenye mavazi ya bei na mapazia ya madhabahu. Mapambo mengi ya kuvaliwa yenye miundo na maumbo mbalimbali yalitengenezwa hasa katika karne ya 19. Mapambo hayo yalitia ndani seti za vito, mataji, vipuli, majebu, mikufu, sanamu, bruchi, na bangili zenye michongo ya maua, majani, wanyama, na miundo mingine ya usanii wa kale wa Wagiriki na Waroma.

Sasa mapambo ya marijani yanatengenezewa hasa katika mji wa Torre del Greco, kwenye Ghuba ya Naples, Italia. Ama kwa kweli, inakadiriwa kwamba asilimia 90 ya marijani yote inayokusanywa ulimwenguni hutumiwa katika viwanda vya mji huo. Katika mji huo, wasanii stadi hutumia misumeno yenye gurudumu kukata minyiri ya marijani vipande-vipande. Vipande vingine hutumiwa kutengeneza shanga za mviringo kwa mashine. Vipande vingine hukatwa katika maumbo na saizi mbalimbali, hupakwa rangi, na kuingizwa katika pete, vipuli, na vitu vingine. Asilimia 50 hadi 75 ya marijani hupotea bure au kutupwa wakati wa utengenezaji wa mapambo na ndiyo sababu gramu moja ya vito vya marijani ni ghali kuliko gramu moja ya vito vya dhahabu.

Biashara ya marijani imepata ufanisi mkubwa. Kwa kusikitisha, kulingana na kitabu Il Corallo Rosso (Marijani), watu “wenye tamaa ya kutajirika haraka” wanaoweza kumaliza na “kuharibu” marijani yote baharini wamevutiwa pia na biashara hiyo. Kwa kuhangaikia hatima ya marijani na biashara inayoitegemea, watu fulani wamependekeza mali hiyo ya asili itumiwe kwa busara. Ijapokuwa marijani haimo katika hatari ya kutoweka, ni vigumu kupata minyiri mikubwa vya kutosha ili kutengeneza vito. Leo, marijani inayotumiwa kutengeneza vito huko Italia hutolewa pia kwenye Bahari ya Pasifiki. Aina mbalimbali za marijani hukusanywa huko Japan na Taiwan, kwenye vina vya meta 320 hivi, hata kwa kutumia nyambizi ndogo na roboti zinazoendeshwa kutoka mbali. Kilometa 2,000 hivi karibu na Hawaii, marijani yenye thamani kubwa hukua kwenye vina vya meta 1,500.

Vito na sanamu maridadi za marijani zinaonyesha ustadi wa wasanii ambao wameendeleza sanaa hiyo ya kipekee ya kale. Na kwa habari ya watu wanaovutiwa na ufundi wa Muumba wetu, “dhahabu nyekundu” ya Mediterania ni mojawapo ya zawadi zake kemkemu za kumfurahisha mwanadamu.—Zaburi 135:3, 6.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mkufu wa karne ya 19 wenye shanga 75,000 za marijani

[Hisani]

Per gentile concessione del Museo Liverino, Torre del Greco

[Picha katika ukurasa wa 17]

Marijani inayoendelea kukua

[Picha katika ukurasa wa 18]

Taji

Kikombe cha kidini cha karne ya 17

Seti ya vito

[Hisani]

Picha zote: Per gentile concessione del Museo Liverino, Torre del Greco

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

◀Per gentile concessione del Museo Liverino, Torre del Greco▼