Kufuga Vipepeo
Kufuga Vipepeo
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KOSTA RIKA
BILA shaka, mfugaji yeyote bora anafahamu kwamba ili afanikiwe, ni lazima mifugo yake iwe na afya bora. Na ndivyo na mfugaji wa vipepeo—yeye huzuia wavamizi wanaonyemelea kama vile wadudu, buibui, na ndege. Iwapo afaulu, vipepeo wake wenye mabawa mawili yenye rangi za kupendeza zaidi duniani wataanguliwa kilometa nyingi kutoka shambani.
Ufugaji wa vipepeo ni biashara ambayo huleta faida nyingi. Ufugaji huo ni njia bora sana na yenye hekima ya kuhifadhi aina tofauti-tofauti za vipepeo. Je, maswali mengi yamezuka akilini mwako? Kwa mfano, shamba la vipepeo ni nini? Hilo huendeshwaje? Kwa nini wao hufugwa? Kabla ya kujibu maswali hayo, hebu tuchunguze jinsi ufugaji wa viumbe hao hafifu ulivyoanza.
Ulianzia Huko China
Kwa karne nyingi Wachina walikuwa na desturi ya kuzalisha nondo kwa ajili ya viwanda vyao vya kutengeneza hariri. Hata hivyo, mashamba ya vipepeo yalianzishwa hivi majuzi tu. Katika miaka ya 1970, maonyesho ya vipepeo walio hai yalifanywa kisiwani Guernsey, karibu na pwani ya Uingereza.
Maonyesho ya Guernsey yalikusudia kutokeza msitu wa kitropiki uliojaa vipepeo wa aina nyingi na wenye rangi mbalimbali. Hivyo, ingebidi vipepeo wanaopatikana katika maeneo yenye joto wasafirishwe hadi huko. Lakini ingewezekanaje kusafirisha vipepeo wa maeneo yenye joto (wengine wao wanaweza kuishi kwa majuma mawili au matatu tu) wakiwa hai kwa maelfu ya kilometa bila baadhi yao kufa njiani? Hilo lilitokeza uhitaji wa kuzalisha vipepeo kwa madhumuni ya kibiashara.
Jinsi Shamba la Vipepeo Linavyoendeshwa
Sasa una nafasi nzuri ya kutembelea shamba la vipepeo na ufurahie kujionea mwenyewe jinsi linavyoendeshwa. Ni jambo la kustaajabisha kuwaona vipepeo wengi wenye rangi mbalimbali za kupendeza wakiwa karibu. Mwandishi wa Amkeni! alitembelea shamba kubwa zaidi la vipepeo katika Amerika ya Kati ambalo linauza vipepeo katika nchi za nje. Hilo ni Shamba la Vipepeo la Kosta Rika. Mbali na kuuza mabuu katika nchi za nje, shamba hilo pia linatoa mafunzo kwa wale ambao wangependa kujifunza kwa undani kuhusu vipepeo.
Unapoingia katika bustani ambamo vipepeo wamefungiwa, utavutiwa kuona mamia ya vipepeo maridadi wenye rangi za kupendeza wakipepea huku na huku na wengine wakielea tu hewani. Viumbe hao wenye rangi nyangavu zenye kuvutia huendelea na shughuli zao za kawaida za kula, kujamiiana, na kutaga mayai, bila hata kutambua kwamba kuna mgeni. Ni jambo la kuvutia sana! Unapotazama na kunusa mimea ambayo vipepeo wamekalia—maua ya msituni na migomba ya ndizi—utatambua kuwa hapo ndipo vipepeo hupata chakula na kuishi.
Bustani iliyozingirwa kabisa huzuia mayai madogo yasiharibiwe na wanyama-wawindaji. Kati ya mayai yote yanayotagwa msituni, ni asilimia 2 tu ndiyo yanayoanguliwa na kuwa vipepeo, lakini asilimia 90 ya mayai yanayotagwa katika bustani iliyofungiwa huanguliwa kuwa vipepeo.
Mimea maalum inahitajika ili vipepeo waweze kuzaana na kusitawi. Kwa hiyo, shamba hilo lina mimea ya aina tofauti-tofauti ambapo vipepeo wa kike hutagia mayai na kulisha viwavi. Vipepeo waliokomaa hunywa maji matamu kutoka kwenye mimea. Aina hususa ya vipepeo hutaga mayai kwenye mmea wa aina moja tu, na viwavi hula mmea huo mmoja tu. Kwa hiyo, ni muhimu kuwa na mimea mingi ya aina tofauti-tofauti shambani.
Kipepeo wa kike hutaga mayai 100 au zaidi kwa wakati mmoja. Mayai hayo yanafanana na matone madogo sana ya maji kama vile kituo kilichoko mwishoni mwa sentensi hii. Mbali na kutaga mayai kwenye mmea mmoja tu, kila aina ya kipepeo hutaga mayai mahali hususa kwenye mmea. Hivyo mfugaji anaweza kuyaona mayai upesi, kuyatoa, na kuyahifadhi. Kila siku mfugaji huangalia kama kuna mayai katika mmea huo, na pia kama viwavi wanakaribia kuanguliwa. Baada ya kuanguliwa, kiwavi mwenye njaa hula magamba ya mayai hayo. Katika Shamba la Vipepeo, viwavi huwekwa kwenye mimea iliyopandwa katika vyungu ambavyo viko ndani ya vyumba vidogo. Ni muhimu sana kudumisha usafi katika vyumba hivyo, kwani kukosa kufanya hivyo kunaweza kueneza magonjwa na kusababisha vifo.
Baada ya hatua ya tatu, viwavi hula sana. Inasemekana kwamba kama mtoto wa mwanadamu mwenye uzani wa kilogramu tatu angekua kwa kiwango kama cha kiwavi, angekuwa na uzani wa tani nane baada ya majuma mawili!
Katika hatua ya tano na ya mwisho, kiwavi huning’inia kwenye tawi la mti ama chini ya dari la chumba, huku aking’ang’ana kwa ustadi kuvua ngozi yake. Buu lililo na gamba gumu hutokea. Huu ni wakati wa mfugaji kutenda kwa uharaka na kwa ustadi.
Mabuu yanahitaji kukusanywa kila siku, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kutambulisha umri wake. Kisha yanapangwa kwa uangalifu sana ndani ya masanduku katikati ya safu zilizotiwa pamba, kila sanduku likiwa na kati ya mabuu 40 hadi 100. Wafugaji wa
vipepeo wana siku kumi za kusafirisha mabuu kwa wanunuzi, kisha wanunuzi wanawapelekea wateja wao. Kwa kawaida nyumba za kutazama vipepeo na vituo vingine kama hivyo hununua mabuu hayo. Iwapo mabuu hayatasafirishwa kwa wakati, vipepeo wataanguliwa njiani na kufa. Mabuu hayo yakisafirishwa kwa wakati barabara, vipepeo watatoka kwenye vifukofuko vyao maelfu ya kilometa mbali na nyumbani, bila kujua kwamba walihamishwa. Shamba la Vipepeo hupeleka kati ya mabuu 4,000 na 6,000 kila mwezi kwenye vituo mbalimbali ulimwenguni.Mashamba ya vipepeo yanazidi kuongezeka ulimwenguni pote. Tayari yako huko El Salvador, Kenya, Madagaska, Malaysia, Marekani, Taiwan, Thailand, Ufilipino na, bila shaka, Kosta Rika. Pia, nyumba za kutazama vipepeo zinaendelea kuongezeka kila mwaka, na kufanya iwe rahisi kutazama viumbe hao wa ajabu katika sehemu nyingi za ulimwengu.
Bila shaka, kufuga vipepeo kutaendelea kuwa sehemu muhimu ya kulinda aina za vipepeo zinazozidi kupungua. Na huenda biashara hiyo ikawasaidia watu kufahamu umuhimu wa viumbe mbalimbali duniani.
[Picha katika ukurasa wa 18]
Wakulima hutumia neti ili kulinda mayai na viwavi (1). Mabuu, kama yale yanayoonyeshwa hapa (2), hupangwa ndani ya masanduku kisha husafirishwa ulimwenguni kote (3)
[Hisani]
Juu kushoto kipepeo aina ya monarch na mabuu: Butterfly House, Mittagong, Australia; katikati kushoto kipepeo na wengine wakiwa katika majani: Courtesy of Buckfast Butterfly Farm
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
K. Schafer/Audiovise