Upimaji-Ramani Ni Nini?
Upimaji-Ramani Ni Nini?
WAMISRI waliwaita “wakaza-kamba.” Wao walikuwa nani? Walikuwa kikundi cha watu wa kale waliokuwa na daraka la kugawanya shamba upya kwa madhumuni ya kutoza kodi kila mwaka baada ya kingo za Mto Nile kufurika. Wanaume hao walikuwa watangulizi wa wataalamu wa siku hizi wanaoitwa wapimaji-ramani.
Siku hizi wapimaji-ramani wanaweza kuonekana kandokando ya barabara kuu na katika mahali pa ujenzi. Huenda umejiuliza, ‘Upimaji-ramani ni nini?’
“Upimaji-ramani umegawanywa katika nyanja mbili,” chasema kichapo Science and Technology Illustrated. Hizo ni “(1) kupima eneo fulani, kuandika rekodi ya mahali ambapo eneo hilo lipo, na kutumia habari hiyo kuchora ramani au maelezo; ama kwa upande mwingine, (2) kutumia ramani au maelezo hayo ili kutia alama kwenye mipaka ya shamba au kuelekeza ujenzi. Upimaji-ramani hutambulisha, au kutia alama, mahali maalumu ardhini, chini ya ardhi, au hata angani.”
Historia ya Upimaji-Ramani
Inavyoonekana, shamba la kwanza kuwa na mipaka lilikuwa bustani ya Edeni. Biblia huonyesha kwamba wapimaji-ramani walikuwako Israeli, nao walihusika katika kuamua mipaka na umilikaji wa shamba. Mithali 22:28 husema hivi: “Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani, uliowekwa na baba zako.” Waroma hata walikuwa na kijimungu kilichoitwa Terminus, kilichosimamia mipaka na alama yake ilikuwa jiwe.
Mabomba na barabara za Waroma, nyingine ambazo bado ziko, zinathibitisha ustadi wa Waroma wa kale wa upimaji-ramani. Walitumia vifaa vichache na wakapata matokeo mazuri. Yapata mwaka wa 200 K.W.K., Mgiriki Eratosthenes, ambaye alikuwa mtaalamu wa anga, mwana-hisabati na mwana-jiografia, alipima urefu wa mzunguko wa dunia.
Karibu na mwaka 62 W.K., Hero, ama Heron, wa Alexandria, katika kitabu chake kilichoitwa Dioptra, alionyesha jinsi ambavyo sayansi ya jiometri, jina linalomaanisha “vipimo vya dunia,” ingetumiwa katika upimaji-ramani. Na kati ya mwaka wa 140 na 160 W.K., Klaudio Ptolemi, akitumia njia iliyoanzishwa na Hipparchus, aliorodhesha mahali 8,000 katika ulimwengu uliojulikana pamoja na vipimo vyake vya latitudo na longitudo.
Kufikia karne ya 18, jamaa ya Cassini, kwa kipindi cha vizazi vinne, ilikuwa imefanya upimaji-ramani wa kisayansi wa kwanza wa taifa zima la Ufaransa na kuchora ramani ya La Carte de Cassini. Kitabu kinachoitwa The Shape of the World kinaeleza kwamba “Ufaransa iliongoza katika sayansi ya kuchora ramani; Uingereza ikawa ya pili; na mataifa ya Austria na Ujerumani yakafuatia. Katika sehemu nyingine za Ulaya upimaji-ramani wa kitaifa ulianza mapema katika karne ya kumi na tisa.” Nje ya
Ulaya, ule Upimaji-Ramani Mkubwa wa India ulifanyika mnamo 1817 ili kukamilisha uchoraji wa ramani ya India. Upimaji-ramani huo uliongozwa na George Everest, na mlima mrefu zaidi duniani ukaitwa kwa jina lake.Wapimaji-ramani hao wa mapema walifanya kazi yao katika hali ngumu. Kitabu Historical Records of the Survey of India cha rekodi zinazofikia mwaka wa 1861, kinafunua kwamba kikundi hicho cha wapimaji-ramani waliugua homa, na inasemekana kuwa huenda mtu 1 tu kati ya 70 ndiye aliyerudi Uingereza. Wapimaji-ramani wengine walishambuliwa na wanyama wa mwitu au walipata chakula kidogo sana. Hata hivyo, wanaume walivutiwa na kazi hiyo ya nje, wajibu, na uhuru wa kiasi fulani ambao kazi hiyo iliwapa.
Kikundi kimoja cha wapimaji-ramani walioitwa Pundit walipata umaarufu wa kipekee kwa kazi yao nzuri huko Nepal na Tibeti. Kulikuwa na sheria na mikataba iliyowapiga marufuku wageni kuingia katika nchi hizo, kwa hiyo wapimaji-ramani hao walijifanya kuwa makasisi wa Kibudha ili waruhusiwe kuingia. Ili kujitayarisha kwa kazi hiyo ya siri, kila mmoja wao alikuwa amezoezwa kutembea hatua 2,000 ili kuhesabu maili moja (kilometa 1.6). Rozari yenye shanga mia moja ilitumiwa kuhesabu hatua hizo ili kupima umbali.
Watu wengi, kama vile maraisi wa Marekani wa awali Washington, Jefferson, na Lincoln walifanya kazi ya upimaji-ramani kwa kiasi fulani. Watu wengine hata huonelea kwamba mafanikio ya kisiasa ya Lincoln, kwa kiasi fulani, yalitokana na kazi yake ya upimaji-ramani, ambao ulimleta karibu na wananchi wenzake.
Upimaji-Ramani Leo
Siku hizi upimaji-ramani katika mitaa yetu unafanywa kwa njia tatu. Kwanza, kuna upimaji-ramani wa kisheria, ambao unahusika na kutambua mipaka halali ya ardhi. Ardhi inapohitaji kugawanywa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ama wakati serikali inapotaka kujenga barabara mpya au njia kuu, wapimaji-ramani wa shamba husaidia kugawanya ardhi na kuchora ramani za matumizi ya kisheria.
Aina nyingine ya upimaji-ramani inahusisha kupima na kuonyesha ukubwa na umbo la kipande cha ardhi, na kina mteremko kiasi gani, na pia kuonyesha mahali ambapo barabara, nyua, miti, na majengo ya huduma mbalimbali na kadhalika yatakapokuwa, na vilevile majengo yaliyopo tayari. Wahandisi wa huduma za umma, wachoraji na wahandisi wa ujenzi, na wataalamu wengine hutumia habari hizo sahihi wanapopanga ujenzi katika kipande hicho cha ardhi. Habari hiyo huwawezesha kuchora ramani ambazo zitahusisha mambo yote na wakati mwingine hata kutia ndani mambo hayo katika michoro yao.
Baada ya michoro, idhini, ramani, na mambo mengine kukamilishwa, na mradi wa ujenzi unapokaribia kuanza, bado kuna jambo la kufanya, yaani kuamua mahali ambapo kila kitu kinapaswa kuwa. Katika hatua hiyo, wapimaji-ramani wa aina ya tatu wanaweka alama kuonyesha mahali ambapo majengo ya huduma, barabara, na mambo mengine yanapaswa kuwa kulingana na ramani. Wanafanya hivyo kwa kupigilia vijiti ardhini na kwa kukaza kamba kati ya vituo hivyo.
* Kazi hiyo hufanywa kwa usahihi sana.
Upimaji-ramani wa mashamba madogo yasiyozidi kilometa 19 unaitwa upimaji-ramani wa nchi tambarare. Eneo kubwa linahitaji aina ya upimaji-ramani unaozingatia kwamba dunia si tambarare bali ni mviringo. Mara nyingi vipimo hivyo huhusianisha vipimo vya kitaifa vya latitudo na longitudo.Upimaji-ramani wa kisasa pia unatumia satelaiti za kipekee zinazopeleka habari kupitia redio na wapimaji-ramani wanapata habari hizo kupitia kompyuta. Kwa kutumia vifaa vinavyoweza kuchukuliwa kwa urahisi, wapimaji-ramani wanaweza sasa kutambulisha mahali mbalimbali duniani kwa usahihi sana. Upimaji-ramani mwingine ambao huenda hatujaufahamu ni kutumia satelaiti kupiga picha za eneo fulani, na upimaji-ramani wa majini ambao huonyesha ufuo wa bahari na kutambua kina na miinuko na eneo la mito, ziwa, bahari, na mahali pengine palipo na maji.
Ni Muhimu Kwetu
Kwa mfano, Daraja la Golden Gate huko California, Marekani, lilifunguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1937. Daraja hilo lilifanyiwa upimaji-ramani katika mwaka wa 1991 ili kurekodi kwa usahihi mahali lilipo. Iwapo tetemeko la dunia litatokea na daraja hilo lisonge, tetemeko hilo laweza kupimwa na hatua kuchukuliwa ili kuhakikisha kwamba daraja litaendelea kuwa imara kutumiwa na umma. Huko Vermont, kituo cha kuteleza juu ya theluji kiliwaajiri wapimaji-ramani warekebishe vijia vyake na kukifanya kituo hicho kiwe na hali bora kabisa kwa mchezo huo.
Zaidi ya hilo, kwa kutumia habari za upimaji-ramani kutoka kwa satelaiti huko angani, mabadiliko katika tabaka la dunia yataweza kupimwa huko China, kukiwa na matumaini ya kwamba athari mbaya za matetemeko ya dunia kwa watu zinaweza kupunguzwa. * Kwa kuongezea, iwe ni nyumba yako, ama barabara unayoendeshea gari, ofisi unayofanyia kazi, au shule unayosomea, vyote huenda vilihusisha mpimaji-ramani vilipojengwa.
Katika njia halisi wapimaji-ramani hugusa maisha yako. Iwe walitumia kamba ama habari kutoka kwa satelaiti huko angani, wamejitahidi kuongeza umaana na utaratibu katika ulimwengu wetu ulio tata. Na kadiri tunavyoendelea kuujenga na kujua zaidi kuhusu dunia yetu, wapimaji-ramani wataendelea kuhitajiwa. Kwa hiyo, wakati ujao unapoona wapimaji-ramani wakifanya kazi kando ya barabara, utaelewa mengi zaidi kuhusu kazi yao ngumu.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 17 Kwa habari zaidi kuhusu longitudo na latitudo, ona makala “Hiyo Mistari Yenye Manufaa ya Kuwaziwa,” katika toleo la Machi 8, 1995, la Amkeni!
^ fu. 21 Kwa habari zaidi, ona makala “Volkeno—Je, Umo Hatarini?” katika toleo la Mei 8, 1996, la Amkeni!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]
Vifaa vya Vipimo Makini
Kifaa cha Elektroni cha Kupimia Umbali—Kifaa hicho hupima umbali kwa kutoa mwali wa kielektroni ambao hugonga vioo vilivyo katika eneo linalopimwa, kisha kukirudia kifaa hicho.
Vifaa Vingine—Kipima-pembe wima na mlazo (kilicho kushoto) hupima pembe. Kifaa hicho kina hadubini ambayo hukiruhusu kupima pembe kwa kutumia lenzi nyingi zilizomo. Vipima-pembe wima na mlazo zingine zinaweza kutumiwa kupima pembe ndogo sana kama vile mpindo uliopo katika kipande kimoja cha mviringo ambao umegawanywa katika sehemu 1,296,000 zilizo sawa. Vifaa vingine (vilivyo kulia) pia vinaweza kupima kwa njia ya elektroni habari zozote zilizokusanywa kuhusu ardhi na kuzirekodi, kama vile pembe, umbali na vipimo vingine. Baadaye, habari inaweza kupelekwa ofisini na kuhifadhiwa kwenye kompyuta ili ikaguliwe na kutumiwa katika michoro.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Pima-maji ya kikale
[Picha katika ukurasa wa 21]
“Wakaza-kamba” wa Misri walikuwa watangulizi wa wapimaji-ramani wa siku hizi
[Hisani]
Borromeo/Art Resource, NY