Njia ya Kipekee ya Kuokoa Uhai wa Watoto Wachanga
Njia ya Kipekee ya Kuokoa Uhai wa Watoto Wachanga
Katika hospitali moja huko Bogotá, Kolombia, watoto wengi mno waliozaliwa kabla ya wakati wao walikufa. Kwa hiyo, mwaka wa 1979, daktari mmoja Mkolombia aligundua njia ya pekee ya kutatua tatizo hilo—kuwatunza watoto kama kangaruu anavyofanya.
Kuokoa uhai wa watoto waliozaliwa kabla ya wakati wao ni jambo gumu kwa madaktari. Mara nyingi, watoto wanaozaliwa wakiwa wadogo sana huwekwa katika kifaa maalumu ili watiwe joto, ambapo wao hubaki hadi waongeze uzito. Hata hivyo, katika nchi zinazoendelea, mara nyingi watoto huambukizwa magonjwa hatari kwa sababu hospitali zina wagonjwa wengi kupita kiasi na ni chafu, na kwa sababu ya upungufu wa madaktari, wauguzi, na vifaa.
Daktari mmoja nchini Kolombia aligundua suluhisho la tatizo hilo. Suluhisho hilo ni nini? Mtoto anapozaliwa kabla ya wakati wake anatunzwa hospitalini kwa njia ya kawaida hadi awe na nguvu kwa kiasi fulani, huku mama yake akizoezwa kumtunza mtoto huyo. Mtoto anapopata nguvu za kutosha, mama yake atamtia joto. Jinsi gani? Kwa kumfunga na kumbeba katikati ya matiti yake. Mtoto anayefungwa hivyo atapata joto na itakuwa rahisi kwake kunyonya maziwa ya mama yake. Hivyo ndivyo mtoto wa kangaruu anavyobebwa na kunyonyeshwa.
Vifaa vya bei ya juu havihitajiki. Mama huvalia blauzi au nguo ya kawaida yenye mshipi. Wakati ambapo mtoto ameongeza uzito vya kutosha, mama na mtoto wanaweza kwenda nyumbani, na kurudi hospitalini kwa ukawaida ili kufanyiwa uchunguzi.
Utafiti unaonyesha kwamba kuwatunza wototo jinsi kangaruu anavyofanya kuna matokeo mazuri na hakudhuru. Isitoshe, yamkini utunzaji huo unawafanya mama na mtoto wawe na uhusiano wa karibu. Si ajabu kwamba mbinu hiyo hutumiwa katika nchi nyingi. Nchini Mexico, watu wa ukoo huzoezwa kuwa “baba kangaruu,” “nyanya kangaruu,” na hata “dada kangaruu” wakati ambapo mama anahitaji kupumzika. Dakt. Guadalupe Santos, anayesimamia mpango huo nchini Mexico, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Tumetumia mbinu hiyo tangu mwaka wa 1992 na tumeona matokeo mazuri. Hatuhitaji vifaa vingi maalumu vya kuwatia watoto joto, na watoto hawahitaji kubaki hospitalini kwa muda mrefu.”