Kuzuia na Kudhibiti Kupanda kwa Shinikizo la Damu
Kuzuia na Kudhibiti Kupanda kwa Shinikizo la Damu
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI
MARIAN alihofu sana! Alianza kutokwa na damu nyingi sana puani. Marian anakumbuka hivi: “Nilifikiri ningekufa.” Daktari mmoja alimwambia Marian kwamba alitokwa na damu kwa sababu shinikizo la damu yake lilikuwa limepanda sana. Marian alimjibu daktari: “Lakini mimi ni mzima.” Daktari akamwambia: “Watu wengi hawajui kwamba wana tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu kwa kuwa hawaoni dalili zozote.”
Vipi kuhusu shinikizo la damu yako? Je, maisha yako ya sasa yaweza kupandisha shinikizo la damu katika siku zijazo? Unaweza kufanya nini ili kudhibiti shinikizo la damu yako? *
Shinikizo la damu ni msukumo wa damu kwenye kuta za mishipa. Shinikizo la damu laweza kupimwa kwa ukanda wa mpira unaoweza kujazwa hewa. Ukanda huo hufungwa kwenye sehemu ya juu ya mkono na kuunganishwa na kifaa cha kurekodi shinikizo. Kifaa hicho hurekodi vipimo viwili. Kwa mfano, chaweza kurekodi kipimo cha 120/80. Nambari ya kwanza huonyesha kipimo cha shinikizo la damu wakati moyo unapopiga (systole). Nambari ya pili huonyesha kipimo cha shinikizo la damu katikati ya mapigo ya moyo (diastole). Shinikizo la damu hupimwa kulingana na milimeta za zebaki. Madaktari husema kwamba shinikizo la damu ya mgonjwa limepanda wakati kipimo kinapozidi 140/90.
Nini hupandisha shinikizo la damu? Hebu wazia unamwagilia shamba lako maji. Unapofungua mfereji au unapopunguza ukubwa wa shimo la mfereji, unaongeza shinikizo la maji. Ndivyo ilivyo pia na shinikizo la damu. Shinikizo la damu hupanda wakati damu nyingi inapopita mshipani au wakati mshipa unapokuwa mwembamba. Mtu hupataje ugonjwa huo? Mambo mengi yanahusika.
Mambo Usiyoweza Kuepuka
Watafiti wamegundua kwamba iwapo mtu ana watu wa familia wenye tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu, basi anakabili uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ugonjwa huo. Takwimu zinaonyesha kwamba mapacha wanaofanana hupata ugonjwa huo zaidi ya mapacha wasiofanana. Uchunguzi mmoja ulizungumza juu ya “kuchunguza habari zinazopatikana katika chembe za urithi ambazo husababisha tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu.” Hiyo inathibitisha kwamba kuna chembe za urithi zinazosababisha tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu. Inasemekana kwamba uwezekano wa kupata tatizo hilo huongezeka mtu anapozidi kuzeeka, na kwamba wanaume weusi wanakabili uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ugonjwa huo.
Mambo Unayoweza Kuepuka
Tilia maanani lishe bora! Shinikizo la damu ya watu fulani linaweza kupanda wanapokula chumvi (sodiamu). Hiyo inahusu hasa wagonjwa wa kisukari, watu ambao shinikizo la damu yao hupanda sana, wazee, na watu fulani weusi. Mafuta mengi katika damu yanaweza kufanyiza utando wa kolesteroli kwenye kuta za ndani za mishipa. Hivyo, mishipa huwa
myembamba na shinikizo la damu huongezeka. Watu ambao ni wazito kupita kiasi kwa asilimia 30 wanaweza kupata tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu. Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba kula vyakula vingi vyenye potasiamu na kalisi kwaweza kupunguza shinikizo la damu.Uvutaji wa sigara unaweza kusababisha utando mgumu wa mafuta kwenye kuta za mishipa, ugonjwa wa kisukari, mshtuko wa moyo, na kiharusi. Kwa hiyo, mvutaji wa sigara aliye na tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu anaweza kupata magonjwa ya moyo. Ijapokuwa uthibitisho unapingana, mfadhaiko na kafeini—inayopatikana katika kahawa, chai, na vinywaji vya kola—yaweza kusababisha tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu. Kwa kuongezea, wanasayansi wanajua kwamba kunywa kileo mara nyingi na kupita kiasi na kutofanya mazoezi kwaweza kuongeza shinikizo la damu.
Kutunza Afya
Si jambo la busara kungoja hadi upate tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu ndipo uanze kuchukua hatua zinazofaa. Mtu anapaswa kutunza afya toka anapokuwa kijana. Kutunza afya sasa kutafanya maisha yako yawe mazuri wakati ujao.
Mwafikiano wa Tatu wa Brazili Kuhusu Kupanda kwa Shinikizo la Damu ulionyesha mabadiliko fulani maishani ambayo yanaweza kupunguza tatizo hilo. Madokezo hayo yatawasaidia watu wasio na ugonjwa huo na wale wanaougua ugonjwa huo.
Watafiti walipendekeza kwamba watu walionenepa kupita kiasi wanapaswa kula lishe kamili isiyo na kalori nyingi, kufanya mazoezi ya kiasi kwa ukawaida, na kuepuka mbinu za kupunguza uzito haraka. Walipendekeza kwamba watu watumie gramu sita tu za chumvi au kijiko kidogo tu cha chumvi kila siku. * Hiyo inamaanisha kutumia kiasi kidogo tu cha chumvi wakati wa kutayarisha mlo, na pia kutokula sana vyakula vinavyouzwa makoponi, nyama baridi zilizopikwa (salami, hemu, soseji, na kadhalika), na vyakula vilivyokaushwa kwa moshi. Mtu anaweza kupunguza matumizi yake ya chumvi kwa kuepuka kuongeza chumvi anapokula na kwa kuchunguza vibandiko vilivyowekwa kwenye makopo ya vyakula vilivyotengenezwa viwandani ili kuona kiasi cha chumvi ambacho kimetumiwa.
Vilevile, Mwafikiano wa Brazili ulidokeza kula vyakula vingi vyenye potasiamu kwa kuwa vinaweza “kuzuia kupanda kwa shinikizo la damu.” Kwa hiyo, lishe bora yapaswa kuhusisha “vyakula vilivyo na chumvi kidogo na potasiamu nyingi,” kama vile maharagwe, mboga za kijani iliyokoza, ndizi, matikiti, karoti, viazi-sukari, nyanya, na machungwa. Ni muhimu pia kutokunywa kileo kupita kiasi. Watafiti fulani wanasema kwamba wanaume walio na ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu hawapaswi kunywa zaidi ya mililita 30 za kileo kila siku; wanawake na vilevile watu ambao si wazito sana hawapaswi kunywa zaidi ya mililita 15 za kileo.Mwafikiano wa Brazili ulikata shauri kwamba kufanya mazoezi ya mwili kwa ukawaida hupunguza shinikizo la damu na hupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu. Kuna faida kufanya mazoezi kwa kiasi kama vile, kutembea, kuendesha baiskeli, na kuogelea, kwa siku tatu hadi tano kila juma kwa muda wa dakika 30 hadi 45. * Mambo mengine yanayochangia afya bora yanatia ndani kuacha kuvuta sigara, kudhibiti ugonjwa wa kisukari na kiasi cha mafuta katika damu (kolesteroli na triglyceride), kula vyakula vyenye kalisi na magnesi ya kutosha, na kuepuka uchovu na kufadhaika kupita kiasi. Dawa fulani zaweza kuongeza shinikizo la damu, kama vile dawa za kuzibua pua, dawa za kutuliza kiungulia zilizo na sodiamu nyingi, dawa za kudhibiti hamu ya kula, na dawa za kumaliza maumivu ya kichwa na kichefuchefu zilizo na kafeini.
Kwa wazi, iwapo shinikizo la damu yako hupanda, daktari wako anaweza kukushauri kuhusu lishe na mazoea yako kulingana na mahitaji yako binafsi. Hata hivyo, kutunza afya tangu ujanani ni jambo lenye manufaa kwa watu walio na tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu na kwa washiriki wote wa familia. Marian, aliyetajwa mwanzoni mwa makala hii, alilazimika kufanya mabadiliko maishani mwake. Ijapokuwa yeye ni mgonjwa, sasa anatumia dawa na anafurahia maisha. Vipi wewe? Endelea kudhibiti shinikizo la damu yako huku ukisubiri wakati ambapo watu wote watakuwa na afya bora na “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Gazeti la Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote mahususi, kwani huo ni uamuzi wa mtu binafsi.
^ fu. 15 Iwapo una ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo, wa ini, au wa figo na unatumia dawa, muulize daktari wako kuhusu kiasi cha chumvi na potasiamu ambacho unahitaji kila siku.
^ fu. 16 Kileo cha mililita 30 kinalingana na mililita 60 za vinywaji kama wiski, vodka, na kadhalika, mililita 240 za divai, au mililita 720 za pombe.
^ fu. 17 Zungumza na daktari wako kuhusu mpango wa kufanya mazoezi.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
KUPAMBANA NA UGONJWA WA KUPANDA KWA SHINIKIZO LA DAMU
1. Mambo Yanayoweza Kusaidia Kudhibiti Kupanda kwa Shinikizo la Damu
• Punguza uzito wa mwili
• Punguza kiasi cha chumvi unachotumia
• Kula vyakula vingi vyenye potasiamu
• Usinywe sana vileo
• Fanya mazoezi kwa ukawaida
2. Mambo Mengine Yanayoweza Kusaidia Kudhibiti Shinikizo la Damu
• Tumia vidonge vyenye kalisi na magnesi
• Kula vyakula vyenye makapi mengi tu
• Dhibiti mfadhaiko
3. Madokezo ya Ziada
• Acha kuvuta sigara
• Dhibiti kiwango cha kolesteroli mwilini
• Dhibiti ugonjwa wa kisukari
• Usitumie dawa zinazoweza kuongeza shinikizo la damu
[Picha zimenadaliwa na]
Madokezo hayo yametoka kwenye Mwafikiano wa Tatu wa Brazili Kuhusu Kupanda kwa Shinikizo la Damu—Revista Brasileira de Clínica & Terapêutica.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kufanya mazoezi kwa ukawaida na kula lishe bora huzuia na kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu