Mambo Yanayowahatarisha Wafanyakazi
Mambo Yanayowahatarisha Wafanyakazi
“Idadi ya watu wanaokufa kazini ni kubwa kuliko ile ya watu wanaokufa kwa sababu ya misiba ya barabarani.” Maneno hayo yaliandikwa kwa herufi nzito kwenye mabango yaliyosambazwa na shirika la WorkCover linaloshughulikia usalama kazini huko New South Wales, Australia.
PASINA SHAKA, mbali na misiba inayosababisha kifo, kuna mambo mengine yanayowahatarisha wafanyakazi. Kila mwaka, mamilioni ya watu hupata majeraha mabaya sana kazini ambayo hata hubadili maisha yao kabisa. Wengine wengi hufa mapema kwa sababu ya kufanya kazi na kemikali hatari au kwa sababu ya mfadhaiko kazini.
Kwa kuwa majeraha mabaya na vifo vinavyosababishwa na hali za kikazi hutokea katika karibu aina zote za biashara na viwanda, swali hili lafaa: Uko salama kadiri gani kazini? Ni mambo gani yanayoweza kuhatarisha afya na uhai wako kazini?
Misongo Kazini
Mara nyingi, wafanyakazi hulazimishwa kufanya kazi nyingi. Neno karoshi linalomaanisha “kifo kinachosababishwa kwa kufanya kazi kupindukia,” lilitumiwa kwa mara ya kwanza huko Japani wakati familia zilizofiwa zilipodai fidia ya bima. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa huko miaka mingi iliyopita, asilimia 40 ya watu wanaofanya kazi ofisini huko Japani walihofu kwamba watakufa kwa sababu ya kufanya kazi kupindukia. Wakili mmoja anayehusika na madai ya bima alikadiria kwamba ‘kila mwaka, angalau watu 30,000 huko Japani hufa kwa sababu ya kufanya kazi kupindukia.’
Polisi huko Japani wamedai kwamba matatizo yanayosababishwa na kazi ni kisababishi kikuu cha ongezeko la visa vya kujiua miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 50 hadi 59. Kitabu The Violence-Prone Workplace kilisema kuwa mahakama moja ilimhukumu mwajiri fulani kwa kusababisha mwajiriwa wake ajiue kwa sababu ya matatizo mengi kazini.
Gazeti la The Canberra Times la Australia lilisema kwamba ‘Sasa Wamarekani ndio watu wanaofanya kazi kwa saa nyingi zaidi ulimwenguni, na hivyo wamewapita Wajapani.’ Hivyo, habari zenye vichwa kama “Watu Wafa kwa Kufanya Kazi kwa Saa Nyingi” zinaonyesha jinsi wafanyakazi waliochoka, kama vile madereva wa ambulansi, marubani, wajenzi, wafanyakazi wanaotoa huduma za usafiri, na watu wanaofanya kazi usiku wanavyofia kazini.
Makampuni yanapobadili utaratibu na kupunguza idadi ya wafanyakazi ili yaendelee kupata faida, waajiriwa hulazimika kufanya kazi nyingi zaidi. Gazeti la British Medical Journal liliripoti kwamba afya ya waajiriwa huathiriwa wakati idadi ya wafanyakazi inapopunguzwa.
Ujeuri Kazini
Wafanyakazi wanaofanya kazi kupindukia na waliofadhaika huhatarisha wafanyakazi wenzao. Uchunguzi uliofanywa huko Uingereza ulionyesha
kwamba kila siku watu wengi wanaofanyakazi ofisini hukasirishwa na wafanyakazi wenzao na mara nyingi migogoro hiyo husababisha ujeuri.Gazeti la Business Week lilisema kwamba “kila juma, wafanyakazi Wamarekani wapatao 15 huuawa kazini.” Gazeti la Harvard Business Review lasema hivi: “Hakuna mkurugenzi yeyote anayependa kuzungumza kuhusu ujeuri kazini. Lakini ukweli ni kwamba kila mwaka mamia ya wafanyakazi huwashambulia au hata kuwaua wafanyakazi wenzao.”
Kwa upande mwingine, wafanyakazi wengi huvamiwa kazini na wateja wao. Ripoti moja ya elimu ya jinai kutoka Australia inasema kuwa madaktari fulani huhofu sana kushambuliwa hivi kwamba wanaomba wasindikizwe wanapowatembelea wagonjwa nyumbani. Polisi na walimu wamo hatarini pia.
Ujeuri mwingine unaotokea kazini ni uchokozi. Shirika la Umoja wa Mataifa la Wafanyakazi huufafanua kuwa ujeuri wa kiakili. Namna moja ya ujeuri huo ni kutendewa kikatili.
Profesa Robert L. Veninga wa Chuo Kikuu cha Minnesota, Marekani, anaripoti kwamba “mfadhaiko na madhara yake huwaathiri wafanyakazi katika karibu sehemu zote za ulimwengu.” Alisema kwamba “Ripoti ya Wafanyakazi Ulimwenguni ya 1993, iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wafanyakazi, ilisema kuwa tatizo kuu ni kwamba mfadhaiko husababishwa na mazingira magumu ya kikazi, yanayobadilika-badilika, na mara nyingi yasiyopendeza.”
Hivyo basi, swali lazuka, Waajiri na waajiriwa wanaweza kufanya nini ili kuwe na usalama kazini? Swali hilo litazungumziwa katika makala ifuatayo.