Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Babu na Nyanya Nimetoka tu kusoma makala ya “Vijana Huuliza . . . Ninawezaje Kusitawisha Uhusiano wa Karibu Pamoja na Babu na Nyanya?” (Mei 22, 2001) Wazazi wangu wamenitia moyo kwa muda mrefu niwe na uhusiano wa karibu pamoja na babu na nyanya yangu, lakini kwa kuwa sikuzote kumekuwa na mgogoro kati ya wazazi wangu na babu na nyanya wa upande wa mamangu, nilihisi kwamba sipaswi kuongea nao. Makala hiyo ilinisaidia kutambua kwamba Yehova anataka niwe na uhusiano wa karibu nao. Sitaunga mkono upande wowote katika mgogoro huo, bali nitaunga mkono upande wa Yehova.
C.L.M., Marekani
Makala kuhusu babu na nyanya zilikuwa nzuri ajabu! Ninashukuru kwamba mlitaja juu ya kuandika barua. Mimi ni nyanya mwenye umri wa miaka 36 na ninahifadhi barua zote ambazo wajukuu wananitumia. Ninafurahia sana kupata barua.
M. Q., Marekani
Ninataka kuwashukuru kwa makala kuhusu babu na nyanya katika matoleo ya Aprili 22 na Mei 22, 2001. Ijapokuwa nyanya yangu anaishi mbali nami, nina uhusiano mzuri pamoja naye. Uhusiano wetu ni kama mahusiano yaliyofafanuliwa katika makala hizo. Yeye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, naye amenipa ujuzi mwingi wa kiroho. Nyakati nyingine tunatayarisha mikutano ya Kikristo pamoja. Upendo wangu kwa Yehova unakua kila ninapomwona nyanya yangu akimtumikia kwa bidii. Makala hizo zinanisaidia kudumisha uhusiano huo wa pekee. Asanteni sana!
G. M., Yugoslavia
Nina swali. Babu yangu ni mgonjwa sana, na nyanya yangu hana fedha nyingi. Ninawezaje kuwa na uhusiano wa karibu nao nisipoweza kwenda kwenye tafrija pamoja nao?
T. O., Marekani
“Amkeni!” linajibu: Ikiwa babu na nyanya yako wanaishi karibu, huenda ukaweza kuwatembelea au kuongea nao kwa simu mara kwa mara. Hata huenda ukaweza kuwasaidia na kazi mbalimbali. Kama vile makala hiyo ilivyopendekeza, kuandika barua ni njia nyingine ya kuwa na uhusiano wa karibu pamoja na babu na nyanya. Kwa vyovyote vile, babu na nyanya watathamini jitihada zozote unazofanya kushirikiana nao.
Simu Kwa kuwa ninafanya kazi katika idara ya fizikia kwenye chuo kikubwa cha elimu, nilivutiwa na makala ya “Simu Zinaunganishwaje?” (Mei 22, 2001) Iliandikwa kwa njia rahisi, na ninatumaini kwamba itawatia moyo wale walio na tatizo la kuelewa somo la fizikia.
S. T., Uingereza
Asanteni kwa makala ya “Simu Zinaunganishwaje?” Nimejiuliza swali hilo mara nyingi. Mimi ni mwanafunzi wa shule ya sekondari, na ninapenda kusoma Amkeni! Gazeti hilo limenisaidia sana katika kazi zangu za shule. Asanteni kwa jitihada zenu!
H. W., Marekani
Kebo ya telegrafu iliyopitishwa kwenye Bahari ya Atlantiki mwaka wa 1866 haikuwa kebo ya kwanza kupitishwa kwenye bahari hiyo. Kebo ya kwanza ilipitishwa mwaka wa 1858 kati ya Ireland na Newfoundland. Imesahaulika kwa kuwa haikudumu kwa muda mrefu.
L. D., Uingereza
“Amkeni!” linajibu: Makala yetu ilisema tu kwamba “mwaka wa 1866, kebo ya ‘telegrafu’ ilipitishwa kwenye bahari ya Atlantiki kati ya Ireland na Newfoundland.” Ile ya kwanza, kama ulivyotaja, ilikuwa ile iliyowekwa mwaka wa 1858. Hata hivyo, kebo hiyo iliharibika baada ya majuma machache tu na kusahaulika.