Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Visababishi Vikubwa vya Kifo Ulimwenguni
Gazeti la Frankfurter Allgemeine Sonntagszeitung lasema kwamba “bado magonjwa yanayosababishwa na virusi, bakteria, na vimelea ndiyo huwaua watu sana ulimwenguni pote.” Kila mwaka, “mamia ya mamilioni ya watu huambukizwa na watu milioni 10 hufa” kutokana na magonjwa matatu tu, yaani, UKIMWI, malaria, na kifua kikuu. Gazeti hilo lasema hivi: “Kufikia katikati ya karne ya 20, hata wataalamu wengi walikuwa na uhakika kwamba baada ya muda mfupi magonjwa ya kuambukiza hayangesababisha vifo vingi. Hata hivyo, kama ilivyoonekana wazi tangu kuenea kwa UKIMWI, ugonjwa wa kichaa cha ng’ombe, na pia ugonjwa wa midomo na miguu ulipoenea hivi majuzi, [bado] viini vinavyoambukiza vinahatarisha sana wanadamu na wanyama. . . . Virusi na bakteria hatari zilitokea bila kutarajiwa katika sehemu mbalimbali ulimwenguni.” Ijapokuwa maumbile ya viini vyenyewe mara nyingi husababisha hali hiyo, utendaji na mazoea ya wanadamu huchangia pia kutokea na kuenea kwa viini hivyo vinavyosababisha magonjwa.
Kupora Mali ya Dini
Gazeti La Croix la Kikatoliki la Ufaransa lasema kwamba “licha ya kutungwa kwa sheria nyingi, wizi na uuzaji wa mali ya dini unaongezeka huko Ulaya.” Vitu vilivyoibwa vyatia ndani misalaba, fanicha, vitu vya dhahabu na fedha, sanamu, picha, na hata madhabahu. Kwa mujibu wa Baraza la Kimataifa la Majumba ya Makumbusho, katika miaka ya hivi majuzi vitu 30,000 hadi 40,000 vimeibwa katika Jamhuri ya Cheki na zaidi ya vitu 88,000 vimeibwa nchini Italia. Wezi huvamia sana pia nchi ya Ufaransa kwani ina makanisa makuu 87. Kati ya miaka ya 1907 na 1996, vitu 2,000 hivi vinavyoonwa kuwa vitu muhimu vya ukumbusho viliibwa katika majengo ya kidini huko Ufaransa, na chini ya asilimia 10 ya vitu hivyo ndivyo vilivyopatikana tena. Ni vigumu kuzuia uporaji huo, hasa kwa sababu ni rahisi kuingia katika makanisa na kwa kawaida hayana ulinzi mkali.
Maji ya Chini ya Ardhi Yanahatarisha Jiji la London
“Visima vinachimbwa ili kuondoa maji chini ya ardhi ambayo yanahatarisha [jiji],” laripoti gazeti la The Economist. Sasa tabaka la maji lipo meta 40 chini ya ardhi ya ua wa Trafalgar Square. Katika karne iliyopita wakati viwanda vilitumia mamilioni ya lita za maji, ilikadiriwa kwamba tabaka hilo la maji lilikuwa meta 93 chini ya ardhi ya ua huo. Kila mwaka, tabaka hilo huinuka kwa meta tatu, na laweza kuharibu reli ya chini ya ardhi, waya nyingi zinazopita chini ya ardhi na misingi ya majengo mengi ya London. Yakadiriwa kwamba ni lazima visima 50 hivi vichimbwe. Gazeti hilo lasema kuwa ‘Shirika la Mazingira linakadiria kwamba karibu lita milioni 50 za maji huvutwa kila siku kutoka chini ya ardhi ya London,’ lakini ni lazima kiasi cha maji yanayovutwa kiongezeke maradufu katika miaka kumi ijayo ili kuondoa hatari hiyo.
“Sisi Si wa Kipekee Kama Tulivyodhani”
“Hatujawahi kamwe kudhalilishwa hivyo,” lasema gazeti la New Scientist. “Tunapojivunia mafanikio ya kufahamu muundo wa seti ya chembeuzi za mwanadamu, uchunguzi wa seti hiyo umefunua kwamba sisi si wa kipekee kama tulivyodhani. Imebainika kwamba idadi ya chembe zetu za urithi inazidi ile ya bakteria mara tano tu, inazidi ile ya mnyoo kwa theluthi moja na inazidi ile ya nzi mara mbili.” Kwa kuongezea, “asilimia 40 hivi ya chembe zetu za urithi zinafanana na zile za mnyoo anayeitwa nematode, asilimia 60 zinafanana na zile za mdudu anayeharibu matunda na asilimia 90 zinafanana na zile za panya.” Gazeti hilo lasema kwamba ujuzi juu ya seti ya chembeuzi za mwanadamu unabadili maoni yetu kuhusu jamii za wanadamu. Watu wawili wa jamii moja wanaweza kufanana, lakini huenda chembe zao za urithi ziwe tofauti kabisa hata kuliko zile za watu wawili wa makabila tofauti. Luigi Cavalli-Sforza wa Chuo Kikuu cha Stanford asema hivi: “Tofauti kati ya watu wa jamii moja ni kubwa sana hivi kwamba ni upumbavu kufikiri kuwa jamii mbalimbali hutofautiana—au hata kufikiri kwamba kuna jamii mbalimbali.”
Biashara ya Ponografia
Gazeti la The New York Times Magazine lasema hivi: “Pesa zinazotokana na biashara ya ponografia zinazidi jumla ya zile zinazopatikana katika soka, mpira wa vikapu na besiboli ya kulipwa. Huko Marekani, watu hutumia pesa nyingi kila mwaka ili kutazama ponografia kuliko zile wanazotumia katika sinema na michezo yote ya kuigiza. Inakadiriwa kwamba kila mwaka biashara ya
ponografia huko Marekani huchuma dola bilioni 10 hadi bilioni 14. Idadi hiyo inatia ndani pesa zinazochumwa na vituo vya kuonyesha ponografia au zile zinazoonyesha filamu hizo kwa njia ya kebo na setilaiti, vituo vya Internet, filamu zinazoonyeshwa kwenye televisheni hotelini, mazungumzo ya ngono kwenye simu, vifaa vinavyotumiwa kuamsha hamu ya ngono na . . . magazeti.” Makala hiyo yaongezea kusema hivi: ‘Kwa kuwa biashara hiyo huchuma dola bilioni 10 za Marekani, hiyo ni biashara kubwa kuliko hata biashara ya Broadway ambayo huchuma dola milioni 600 za Marekani.’ Kwa mfano, mwaka jana shirika la Hollywood lilitoa filamu 400 mpya, na biashara ya ponografia ilitoa video 11,000 za ngono. Lakini ni vigumu kusikia Mmarekani yeyote akikubali kwamba yeye hutazama video hizo. Gazeti la Times lasema hivi: “Hakuna biashara nyingine inayozidi biashara ya ponografia. Jambo la kushangaza ni kwamba biashara hiyo haiwezi kuanguka hata ingawa kwa kawaida watu hawakubali kwamba wanatazama ponografia.”Nguvu za Transmita za Redio ya Vatikani Zapunguzwa
Gazeti la New Scientist laripoti hivi: “Wasimamizi wa kituo cha Redio ya Vatikani wamekubali kupunguza muda wa kurusha matangazo kwa sababu ya malalamiko kwamba huenda mnururisho wa transmita zake zinazotumia nguvu nyingi za umeme unadhuru afya.” Muda wa kurusha matangazo kwa masafa ya kati utapunguzwa mara mbili. Nguvu za umeme zinazotumiwa kupeleka ishara zitapunguzwa pia. Matangazo ya kila siku husambazwa kotekote duniani katika lugha 60 kwa kutumia frikwensi mbalimbali. Kituo hicho kilipojengwa miaka 50 iliyopita, antena zake 33 ziliwekwa kwenye eneo lisilokaliwa na watu wengi, nje ya jiji la Roma. Leo, watu 100,000 hivi huishi karibu na hapo, na kuna wasiwasi kwamba transmita hizo zinazotumia nguvu nyingi za umeme zimesababisha ugonjwa wa kansa ya damu. Kituo hicho hakijaweka vyombo vya kupeleka na kurudisha ishara katika nchi za nje ili kuongeza volteji ya ishara hizo. Italia ilipotunga sheria mpya kuhusu mnururisho mnamo mwaka wa 1998, iliomba Vatikani ipunguze kiasi cha nguvu za umeme za kituo hicho. Gazeti la New Scientist lilisema kwamba Vatikani ilikubali kupunguza matumizi hayo ya umeme kama “tendo la hisani,” ijapokuwa ilikataa kukubali kwamba kuna hatari zozote za afya na kwamba Italia haina mamlaka yoyote juu yake kama serikali jirani.
Maji ya Chupa na ya Mfereji
Gazeti la The New York Times laripoti kwamba “maji ya chupa yanapendwa sana hivi kwamba aina 700 tofauti za maji ya chupa hutengenezwa ulimwenguni.” Lakini, “mara nyingi tofauti kati ya maji ya chupa na maji ya mfereji ni chupa tu.” Shirika la Hazina ya Ulimwenguni Pote ya Mazingira (WWF) lasema kwamba “katika nchi nyingi, maji ya chupa si mazuri kuliko maji ya mfereji ingawa maji hayo hugharimu mara 1,000 zaidi.” Kutumia maji ya mfereji huokoa pesa na kunahifadhi mazingira kwani kila mwaka tani milioni 1.5 za plastiki hutumiwa kutengeneza chupa za maji, na “kemikali zenye sumu zinazotokezwa wakati chupa zinapotengenezwa na kutupwa zaweza kutoa gesi zinazoathiri hali ya hewa.” Dakt. Biksham Gujja mkuu wa Mradi wa Kimataifa wa Maji Safi wa WWF anasema kwamba “huko Ulaya na Marekani kuna sheria nyingi kuhusu maji ya mfereji kuliko zile zinazodhibiti biashara ya maji ya chupa.”
Ramani ya Jiji la Kale la Aleksandria
Ramani ya jiji la kale la Aleksandria imechorwa baada ya kuchimba na kuchunguza jiji hilo lililo chini ya maji kwa miaka mitano. Ramani hiyo yaonyesha mahala ambapo majumba ya kifalme ya Mafarao, magati, na mahekalu yalipokuwa. Mwanaakiolojia Mfaransa Franck Goddio na kundi lake walitumia michoro ambayo ilitegemea habari zilizotoka kwa wapiga-mbizi na pia uchunguzi uliofanywa kwa kompyuta kuhusu jiji hilo lililo chini ya maji, na matokeo yaliwashangaza. Goddio alisema hivi: “Muda mfupi baada ya kuchunguza bandari kwa kompyuta kwa mara ya kwanza, tulitambua kwamba mandhari ya sehemu za jiji la kale la Aleksandria ilikuwa tofauti kabisa na jinsi tulivyodhani.”
“Je, Unawaamini Malaika?”
Zaidi ya wakazi 500 wa Quebec walipoulizwa swali hilo, asilimia 66 kati yao walijibu ndiyo. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la Kanada la Le Journal de Montréal, mtafiti mmoja anasema kwamba watu wengi wanaamini nguvu zinazozidi za wanadamu si kwa sababu tu ya dini ya Kikatoliki bali pia wameshawishiwa sana na dini ya Kibudha katika jimbo hilo. Hata hivyo, mwanasosiolojia Martin Geoffroy anashangaa kwamba theluthi moja tu ya wale waliohojiwa ndio waliosema walimwamini Ibilisi. Yeye asema hivi: “Jambo linalohangaisha ni kwamba tunaamini mema tu. Tunawaamini malaika lakini hatumwamini ibilisi. Tunapuuza mabaya.”