Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Je, Mazoea ya Kutazama Televisheni Yaandikwe Kwenye Rekodi za Kitiba?

Kikundi cha madaktari wa magonjwa ya watoto huko Hispania, kinapendekeza kwamba mazoea ya mtoto ya kutazama televisheni yapasa kuandikwa kwenye rekodi zake za kitiba. Kwa mujibu wa gazeti la Hispania Diario Médico, madaktari hao wanaonelea kwamba wanapaswa kujua saa ambazo mtoto mgonjwa anatumia kila siku kutazama televisheni na pia programu anazotazama na anazitazama na nani. Kwa nini? Kwa sababu uchunguzi uliofanywa na madaktari hao ulifunua kwamba kutazama televisheni huwafanya watoto wawe wavivu, wawe wachokozi zaidi, wapende kununua vitu, wasifanye vizuri shuleni, na huchangia uwezekano wa kuwa waraibu wa televisheni. Ripoti hiyo yasema hivi: ‘Madaktari wa magonjwa ya watoto wanapendekeza kwamba wazazi wasiweke televisheni katika chumba cha kulala cha watoto au mahala ambapo [watoto] wanaweza kutazama programu zozote za televisheni. Isitoshe, wapaswa kuepuka kutazama televisheni wakati wa milo, na wazazi wapaswa kupunguza saa za watoto kutazama televisheni zisizidi saa mbili kwa siku, japo itakuwa vizuri zaidi wasipozidisha saa moja kila siku.’

Ongezeko la Watu China

“Idadi ya watu nchini China imefikia watu bilioni 1.26 na watu hao wanaishi kwa muda mrefu zaidi, wanapata elimu nzuri zaidi na kustaarabika zaidi,” lasema shirika la habari la abcNEWS.com. Kulingana na Zhu Zhixin, mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Takwimu, kumekuwa na ongezeko la watu milioni 132.2 tangu mwaka wa 1990. Ongezeko hilo la chini la asilimia 1.07 kwa mwaka, limesababishwa na sera za China za kuwa na mtoto mmoja zilizoanzishwa mwishoni mwa miaka ya 1970. Hata hivyo, maafisa wana wasiwasi kwani uchunguzi uliofanywa mwaka wa 1999 ulifunua kwamba kwa kila wasichana 100 waliozaliwa, wavulana 117 walizaliwa. Huenda hiyo ni kwa sababu ya kutoa mimba za watoto wasichana kimakusudi. Ripoti hiyo yasema hivi: “Wanasosiolojia wanahofu kwamba uwiano huo usiolingana utasababisha upungufu wa wachumba wa kike, kuongezeka kwa ukahaba na kuwateka nyara wanawake na kuwauza ili waolewe.”

“Hazina ya Chini ya Ardhi”

Watafiti walioongozwa na mtaalamu wa elimu ya maji ya chini ya ardhi wa Brazili, Heraldo Campos, wamekamilisha mradi wa miaka saba wa kuchora sehemu zenye maji mengi ardhini katika Amerika ya Kusini. Tabaka la maji ya ardhini la Guarani, lililo katika sehemu fulani za Brazili, Uruguay, Paraguay, na Argentina, lina ukubwa wa kilometa za mraba zipatazo milioni 1.2 na huhifadhi kiasi cha maji kipatacho kilometa mchemraba 40,000. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Mazingira Ulimwenguni “kiasi cha maji katika tabaka hilo kwa sasa chatosha kuhudumia watu wote wa Brazili kwa miaka 3,500.” Katika siku za usoni, huenda ‘hazina hiyo ya chini ya ardhi’ itatumiwa pia kuzuia kuenea kwa majangwa, na kwa sababu ya halijoto ya maji hayo, huenda itatumiwa kutokeza nishati. Kwa kuchora ramani ya tabaka hilo, watafiti hao wanatazamia kulinda sehemu ambazo huingiza maji mengi ili zisichafuliwe na mbolea na dawa za kuua wadudu-waharibifu.

Kuongezeka kwa Kansa ya Ngozi

Kwa mujibu wa shirika la habari la El Pais Digital la Hispania, visa vya watu wenye uvimbe hatari zaidi wa ngozi unaoitwa melanoma, vimeongezeka sana. Kufikia katikati ya karne ya 20, mtu mmoja kati ya kila watu 1,500 aliugua ugonjwa huo. Lakini kufikia mwaka wa 2000, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka kuwa mtu mmoja kati ya kila watu 75, hasa kwa sababu ya mtindo wa kujianika juani. Kwenye mkutano wa Jumuiya ya Ulaya ya Matibabu ya Uvimbe, Profesa J. Kirkwood alisema kwamba asilimia 40 ya visa vya uvimbe wa melanoma husababishwa na chembe za urithi na asilimia 60 iliyosalia husababishwa na kuchomwa sana na jua. Wanawake wenye umri wa kati ya miaka 23 na 50 ndio huathiriwa sana. Profesa Kirkwood alisema kwamba katika kipindi cha utotoni na vijana wanapobalehe, mnururisho wa jua waweza kusababisha mabadiliko katika chembe za rangi ya ngozi, japo huenda kansa ikatokea baada ya miaka mingi. Profesa Kirkwood alisema hivi: ‘Ngozi huhifadhi mnururisho wa jua.’

Kugeuza Sukari Iwe Plastiki

Wanasayansi kwenye Taasisi ya Brazili ya Uchunguzi wa Tekinolojia wamegundua jamii mpya ya bakteria inayoweza kugeuza sukari iwe plastiki. Jamii za bakteria zilizogunduliwa awali ziliyeyusha na kugeuza sukari ambayo ilikuwa imevunjwa katika molekuli ndogondogo. Lakini “uwezo mkubwa wa jamii hiyo [ya bakteria iliyogunduliwa hivi karibuni] ni kwamba inaweza kujenga na kuvunja sukari moja kwa moja,” asema mhandisi Carlos Rossell. Bakteria zinapopata sukari nyingi kupita kiasi, zinatumia sukari hiyo ya ziada kutengeneza chembe ndogondogo za plastiki inayoweza kuoza. Wanasayansi hupata chembe hizo kwa kutumia kiyeyusho. Kulingana na watafiti hao, “kilogramu moja ya plastiki yaweza kutengenezwa kwa kutumia kilogramu tatu za sukari,” lasema gazeti la O Estado de S. Paulo.

Mafuta Katika Milo Hudhoofisha Akili

Gazeti la New Scientist lasema hivi: “Milo yenye mafuta mengi yaweza kuziba ubongo wako na pia kuziba ateri zako za moyo.” Ili kuelewa jinsi milo yenye mafuta mengi inavyoathiri ubongo, watafiti nchini Kanada “walilisha panya wenye umri wa mwezi mmoja chakula chenye mafuta mengi ya nyama au ya mboga hadi panya hao walipofikia umri wa miezi minne.” Panya wengine walilishwa chakula kisicho na mafuta mengi. Vikundi vyote viwili vya panya vilifundishwa mambo fulani. Matokeo yakawa nini? Panya waliolishwa vyakula vyenye mafuta mengi ‘hawakujifunza mengi kama panya wembamba.’ Mtafiti Gordon Winocur alisema hivi: “Vyakula vyenye mafuta mengi hudhoofisha uwezo wetu wa kufanya karibu mambo yote. Inashangaza sana jinsi wanyama hao walivyodhoofika.” Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watafiti hao wanahisi kwamba “mafuta huzuia ubongo [usiingize] glukosi, labda kwa kuathiri utendaji wa insulini, ambayo husaidia kudhibiti viwango vya sukari katika damu.”

Vifaa vya Kutesa Watu Vyauzwa

Makala moja katika gazeti la Südwest Presse la Ujerumani yasema hivi: “Biashara ya kuuza vifaa vya kutesa watu inaongezeka.” Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International, yasemekana kuwa makampuni 150 ulimwenguni kote yameanza biashara hiyo ya kutisha, kutia ndani makampuni 30 huko Ujerumani na 97 huko Marekani. Mbali na kuuza minyororo inayofungwa miguuni na pingu zenye menomeno zinazofungwa kwenye vidole gumba, wanauza pia vifaa vya kushtua mwili vinavyotumia nguvu nyingi sana za umeme. Yasemekana kuwa kampuni moja huko Marekani ilikuwa ikiuza kanda zilizodhibitiwa kutoka mbali ambazo hushtua mwili wa mtu kwa volteji 50,000. Vifaa hivyo vya hali ya juu vyapendwa sana na wanyanyasaji kwa kuwa haviachi alama zozote kwenye miili ya watu walioteswa.

Buibui Katika Theluji

Katika uchunguzi wake wa buibui aina ya crab, mtafiti Mjerumani Peter Jaeger wa Chuo Kikuu cha Mainz ‘amegundua aina mpya 50 ya buibui hizo zinazositawi katika theluji na barafu ya milima ya Himalaya hata kwenye kimo cha meta 3,800,’ lasema gazeti la The Asian Age. ‘Japo wanaweza kuwa na ukubwa wa sentimeta nne, buibui hao wakubwa hawahatarishi uhai wa wanadamu.’ Wao hupatikana katika nyufa miambani au ndani ya ganda la mti na hula wadudu. Wao huwapata wadudu kwa urahisi kwa sababu ya uwezo wao wa kusikia haraka. Lakini kwa nini buibui hao hawagandi wakati wa baridi kali? Tofauti na buibui wanaopatikana katika maeneo yenye joto, buibui wa Himalaya wanaweza ‘kushusha kipimo cha mgando miilini mwao,’ asema Jaeger. “Wao huhifadhi alkoholi kali sana katika umajimaji wa miili yao na hilo huwawezesha kustahimili halijoto zilizo chini ya kipimo cha mgando.”

Kugundua Magonjwa

Gazeti la sayansi la natur & kosmos la Ujerumani laripoti kwamba huenda jaribio la kunusa likasaidia kubainisha magonjwa mapema kama vile ugonjwa wa kutetemeka au ugonjwa wa Alzheimer. Mtu anapoanza kuugua ugonjwa wa kutetemeka, dalili moja ya kawaida huwa kutohisi harufu. Kutokana na jitihada za Profesa Gerd Kobal, mbinu ya kupima kiwango cha kudhoofika kwa uwezo wa kunusa imebuniwa. Ingawa dalili za wazi za ugonjwa wa kutetemeka, kama vile kutetemeka na kukakamaa kwa misuli huanza baada ya muda, yawezekana kugundua kudhoofika kwa uwezo wa kunusa harufu miezi mingi au hata miaka mingi mapema. Hilo limewezeshwa na majaribio hayo mapya ya kunusa. Uvumbuzi huo umewawezesha watu wanaougua ugonjwa huo wapate matibabu ambayo huenda yakapunguza kuenea kwa ugonjwa huo usiotibika kwa sasa.

Kutupa Chakula

Gazeti la Mainichi Daily News la Japani lasema hivi: “Kiasi kikubwa sana cha chakula hutupwa wakati wa sherehe za arusi na sherehe nyingine kubwakubwa.” Uchunguzi uliofanywa na serikali kuhusu utupaji wa chakula ulifunua kwamba, kwa wastani, familia zilitupa asilimia 7.7 ya vyakula vyao, wauzaji wa rejareja wa vyakula walitupa asilimia 1.1, na mikahawa ilitupa asilimia 5.1 ya vyakula ambavyo havijapikwa. Hata hivyo, “kwenye sherehe kubwakubwa ambapo walaji hujihudumia, asilimia 15.7 ya vyakula vilitupwa,” na asilimia 24 hivi ya vyakula vilivyotayarishwa kwenye karamu za arusi “ama vilibaki au vilitupwa,” lasema gazeti hilo. Ni watengenezaji wa vyakula tu wanaoripoti kwamba ‘wanajitahidi sana kutotupa chakula.’