Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Faraja kwa Wagonjwa Nina umri wa miaka 22, na kwa muda mrefu sana nimeugua ugonjwa wa kansa unaodhoofisha. Nilifurahia ule mfululizo wa makala “Faraja kwa Wagonjwa.” (Januari 22, 2001) Nilifarijika sana kujua kwamba Yehova huelewa mfadhaiko na hasira ninayokuwa nayo! Nilijiweka katika hali ya William na Rose Meiners na jinsi walivyoshughulikia hali yao. Yehova ajua jinsi ya kuwategemeza wale wanaompenda!
A.C.C., Chile
Vizima-Moto Asanteni kwa makala yenye kichwa “Moto! Je, Utatumia Kizima-Moto Kipi?” (Januari 22, 2001) Tafadhali tutumieni nakala 130 za toleo hilo ili tumpe kila mmoja wa waajiriwa wetu nakala ya kupelekea familia yake.
D. F., Marekani
Asanteni kwa jitihada zenu za kutayarisha makala hiyo. Hakuna gazeti jingine la kurasa 32 lenye habari tofauti-tofauti za kusaidia kama hilo. Hata hivyo, ningependa kusema kwamba ninaamini kuwa mahala mlipotaja kizima-moto cha “poda kavu” mlimaanisha kizima-moto cha “kemikali kavu.” Vizima-moto vya poda kavu, ambavyo huwa na nyota ya manjano yenye herufi D, vyaweza kutumiwa tu kuzima metali zinazoungua, lakini vizima-moto vya kemikali kavu vyaweza kutumiwa kuzima mioto ya aina ya ABC au BC.
J. H., Marekani
Asante kwa ufafanuzi huo. Katika nchi fulani usemi “vizima-moto vya poda kavu” hutia ndani vile vinavyoitwa vizima-moto vya kemikali kavu nchini Marekani. Kwa kuwa “Amkeni!” ni gazeti la kimataifa, mara kwa mara pasina budi kuwepo tofauti fulani za maneno.—Mhariri.
Mchanga Mno Kuweka Miadi ya Kijinsia? Nilifurahia sana makala “Vijana Huuliza . . . Vipi Ikiwa Wazazi Wangu Wanafikiri Mimi Ni Mchanga Mno Kuweka Miadi ya Kijinsia?” (Januari 22, 2001) Nina umri wa miaka 17, na nimekata kauli kwamba siko tayari kuoa wala kutegemeza familia. Makala hiyo ilinisaidia kufikiri sana kabla ya kuweka miadi ya kijinsia na pia kutumia ufahamu nitakapoamua kuweka miadi ya kijinsia na kuoa.
A.M.H., Marekani
Nikiwa na umri wa miaka 15 tu, mikazo ninayopata katika shule ya sekondari ya kuweka miadi ya kijinsia hunifadhaisha sana. Yanitia moyo sana kujua kwamba ninategemezwa na Biblia na Wakristo wenzangu. Hilo hunisaidia kushikilia msimamo wangu!
L. M., Kanada
Niliweza kuelewa hali ya wale vijana wawili wa jinsia tofauti katika ile picha, waliokuwa wakizungumza kwa simu, kwa kuwa nilikuwa karibu kuwa katika hali hiyo. Nililazimika kukatisha uhusiano pamoja na mtu mmoja kwa sababu ninajua kwamba siko tayari kuweka miadi ya kijinsia. Makala kama hizo hunitia moyo sana kudumisha azimio langu la kusubiri.
M.R.C., Marekani
Nina umri wa miaka 14. Makala hiyo ilinisaidia sana kuelewa jinsi ilivyo hatari kwangu kuweka miadi ya kijinsia sasa, kwani siko tayari kufunga ndoa. Makala hiyo ilinisaidia kung’amua umuhimu wa kusitawisha uhusiano pamoja na Yehova sasa hivi badala ya kutafuta mpenzi.
A. P., Kanada
Ni kana kwamba makala hiyo iliandikwa kwa ajili yangu tu. Nilifikiri kwamba wazazi wangu walikuwa wakali sana na kwamba hawakuelewa hisia zangu. Sasa ninaelewa kwamba wanafanya yote wawezayo ili kunisaidia na kunilinda. Ninatarajia kwa hamu kubwa kusoma makala zijazo za “Vijana Huuliza”!
H. E., Rumania