Je, Sherehe Zinazopendwa Zinaweza Kudhuru?
Je, Sherehe Zinazopendwa Zinaweza Kudhuru?
KATIKATI ya mwezi wa Oktoba, mabadiliko ya ajabu yanaanza kutukia katika majiji fulani nchini Ufaransa. Maduka yanajaa maboga, viunzi vya mifupa, na tando za buibui. Katika maduka makubwa, makeshia wamevalia kofia nyeusi zilizochongoka. Siku inayotangulia sherehe hiyo, watoto wadogo hurandaranda mitaani huku wakiwa wamevalia kama wachawi, hubisha milango na kutisha kuwashambulia wenyeji iwapo hawatapewa peremende.
Desturi hizo za ajabu ni sehemu ya sherehe inayoitwa kwa Kiingereza Halloween. Hapo awali ilionwa kuwa sikukuu ya Marekani, lakini sherehe ya Halloween imeenea ulimwenguni pote na inapendwa sana na watoto na watu wazima pia. Yaonekana kwamba sikukuu hiyo husherehekewa kwa shamrashamra nchini Ufaransa. Kadirio moja lilionyesha kwamba thuluthi moja hivi ya wakazi wa Ufaransa walisherehekea sikukuu hiyo mwaka uliopita. Gazeti La Repubblica la Italia linalochapishwa kila siku linasema kwamba sherehe hiyo inayopendwa sana inaenea kotekote katika Italia. Gazeti la Nordkurier linasema kwamba “raia wengi sana [wa Ujerumani] hawapendi kukosa burudani hiyo yenye kushtua.”
Sherehe ya Halloween hupendwa sana katika sehemu nyinginezo mbali na Ulaya. Kutoka Bahamas hadi Hong Kong, Halloween husherehekewa kwa shangwe kuu. Gazeti la International Herald Tribune laripoti kwamba mwaka uliopita kituo kimoja cha redio nchini Sri Lanka kilikuwa na mashindano ya “maelezo ya mapishi ya Halloween
ya ajabu zaidi na mashindano ya kupaaza kilio chenye kuogofya zaidi kama mtu anayeuawa kikatili.” Sherehe hiyo pia imeanza kutia mizizi nchini Japani. Maelfu ya watu wamekuwa wakishiriki maandamano ya kusherehekea Halloween jijini Tokyo wakiwa na maboga yenye taa yaliyochongwa kama uso wa mwanadamu.Hata katika nchi nyinginezo ulimwenguni ambako Halloween si maarufu, mara nyingi kunakuwa na sikukuu na sherehe kama za Halloween. Wakati wa sherehe ya Usiku wa Guy Fawkes nchini Uingereza, unaweza kuona watoto wengi wakirandaranda mitaani wakiomba pesa na kufanya vituko kama vya sherehe ya Halloween. Huko Taiwan, kuna Sherehe ya Kandili yenye madoido mengi. Watoto hutembea-tembea mitaani wakiwa wamebeba kandili zenye maumbo ya ndege na wanyama hatari. Nchini Mexico kuna Siku ya Wafu inayoitwa Día de los Muertos. Sherehe hiyo imefika nchini Marekani kutoka Mexico. Mwandishi Carlos Miller anasema kwamba bado Wamarekani fulani wa Mexico ‘wanavalia vinyago vya mbao vinavyoitwa calacas. Wao hucheza dansi za kuwaheshimu watu wao wa jamaa waliokufa.’
Huenda watu wengi wakaona kwamba sherehe hizo haziwezi kudhuru, au ni kisingizio kwa watoto na watu wazima kuvalia mavazi ya pekee na kufanya kama wapendavyo. Hata hivyo, maoni hayo ya kutojali hayazingatii ukweli wa kwamba sherehe hizo zilianzishwa na wapagani. Kwa mfano, Sherehe ya Kandili nchini Taiwan, ilianza wakati watu walipowasha kandili ili kujaribu kuona viumbe wa roho kutoka mbinguni ambao iliaminika kwamba walikuwa wanaelea angani. Siku ya Wafu nchini Mexico ilitokana na desturi moja ya Waazteki ya kuwaheshimu wafu.
Huenda wengine wakabisha kwamba chanzo cha sherehe kama hizo si muhimu. Lakini jiulize hivi, ‘Je, kweli sherehe zilizotokana na vyanzo viovu zaweza kuonwa kuwa zisizodhuru?’ Bila shaka wafanyabiashara wanaodhamini sherehe hizo hawajali. Kuhusu sherehe ya Halloween, mwakilishi wa Taasisi ya Utamaduni ya Barcelona, nchini Hispania, anasema kwamba “ni sherehe inayoenezwa kwa sababu za kibiashara.” Kwani, mwaka uliopita mapato yaliyotokana na Halloween nchini Marekani peke yake, yalikadiriwa kuwa dola bilioni 6.8. Kwa muda wa miaka mitatu tu, kampuni moja inayotengeneza mavazi ya Halloween nchini Ufaransa imepata faida inayozidi ile ya kawaida kwa mara 100.
Lakini je, unapaswa kushiriki sherehe hizo eti kwa sababu zinapendwa au zinaleta faida? Ili kupata jibu, tutachunguza kwa undani zaidi sherehe ya Halloween.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Mafuvu yaliyotengenezwa kwa sukari yanayotumiwa wakati wa Siku ya Wafu nchini Mexico
[Hisani]
SuperStock, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Mioto mikubwa huwashwa kwenye sherehe ya Usiku wa Guy Fawkes nchini Uingereza
[Hisani]
© Hulton Getty Archive/gettyimages