Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Afya Bora Mimi ni tabibu wa maungo aliyesajiliwa, na nimefanya kazi hiyo kwa miaka 21 nikisaidia maelfu ya wagonjwa. Nina wasiwasi sana kwamba huenda watu wengi watakaosoma ule mfululizo wa makala “Afya Bora—Kuna Machaguo Gani?” (Oktoba 22, 2000) wakasita kupata matibabu ya maungo wakiogopa hatari zilizoonyeshwa.
A. K., Marekani
Mnasema kwamba ulainishaji wa shingo waweza kumletea mgonjwa kiharusi. Nimekuwa tabibu wa maungo kwa zaidi ya miaka 50, na sijawahi kuona wala kusikia juu ya jambo hilo.
B.D.B., Marekani
Hatukukusudia kuwavunja moyo wasomaji kupata matibabu ya maungo ikiwa wanataka kufanya hivyo. Gazeti la “Amkeni!” lilisema hivi: “Jambo la kutokeza ni kwamba kuna ripoti chache za athari zitokanazo na kurekebishwa maungo na tabibu mwenye uzoefu.” Kuhusu ulainishaji huo “Archives of Internal Medicine,” Buku la 158, la Novemba 9, 1998, lilisema kwamba “kiwango cha madhara yanayosababishwa bado kinatiliwa shaka” na kwamba ‘makadirio ya visa vya watu walioathiriwa huwa kisa 1 kati ya 400,000 hadi visa 3 mpaka 6 kati ya milioni 10.’ Tungalionyesha waziwazi kwamba madhara yanayosababishwa na urekebishaji wa maungo, ambayo yalisemwa kuwa hutia ndani kiharusi, hutokea mara chache sana.—Mhariri.
Asanteni sana kwa mfululizo huo. Sipingi matibabu yasiyo ya asili, lakini viuavijasumu hunidhuru sana. Nyakati nyingine, madaktari wanaotumia matibabu yasiyo ya asili hawawezi kutambua magonjwa yangu, basi ninalazimika kutafuta matibabu mengine. Makala hizo zimenitia moyo sana kwa kuwa hata watu fulani wamenicheka kwa sababu ya uchaguzi wangu.
S. H., Antigua
Kwenye sanduku lililo kwenye ukurasa wa 8, daktari mmoja alinukuliwa akisema kuwa mitishamba kama ginkgo biloba na feverfew yaweza kuvuruga kuganda kwa damu inapotumiwa pamoja na dawa zilizoagizwa na daktari. Mimi hutumia mitishamba hiyo pamoja na dawa. Nilifikiri kuwa mitishamba yote ilikuwa sawa kabisa! Huenda hilo likanilinda nisipate matatizo wakati ujao.
G. G., Marekani
Kosa Kuhusu Siku Makala zenu hufanyiwa utafiti sana na zinasadikisha; makosa hupatikana mara haba. Hata hivyo, niliposoma makala “Maharamia wa Skandinavia—Washindi na Wakoloni” (Desemba 8, 2000), niliona kosa dogo. Mlisema kwamba majina ya Kiingereza ya siku fulani yalitokana na hekaya za Waskandinavia. Ijapokuwa Waskandinavia waliabudu Tyr, Odin, Thor, na Frigga, Wajerumani walifanya vivyo hivyo kwa kutumia majina tofauti kidogo. Waliingiza ibada hiyo nchini Uingereza walipoivamia katika karne ya tano na ya sita. Basi asili ya majina ya siku za juma katika Kiingereza ni ya Wajerumani waliovamia Uingereza.
A. C., Uingereza
Kichapo “The World Book Encyclopedia” na vichapo vingine vyaonyesha kwamba majina ya siku hizo “yametokana na majina ya miungu ya Waskandinavia.” Hata hivyo, kichapo “The Encyclopædia Britannica” chasema kwamba yalibuniwa “kutokana na maneno ya Kijerumani kwa ajili ya miungu ya hekaya za Wajerumani wa kale.” Wasomi fulani wanaamini kwamba maneno hayo ya Wajerumani waliovamia Uingereza yanapatana na lugha ya wenyeji wa kale wa Norway. Vyovyote iwavyo, wasomi wataendelea kubishana kuhusu suala hilo.—Mhariri.
Mshuko wa Moyo Asanteni sana kwa makala “Vijana Huuliza . . . Je, Nimwambie Mtu Fulani Kwamba Nimeshuka Moyo?” (Oktoba 22, 2000) Makala hiyo ilitokea wakati ambapo nilikuwa nimeshuka moyo sana na sikujua la kufanya. Kusoma makala hiyo kulinifanya nihisi kuwa kuna mtu anayenielewa. Nilizungumza na wazazi wangu, rafiki yangu mkubwa, na hasa Yehova. Yehova alinisaidia sana. Sitaki kamwe kuvunja uhusiano wangu wa karibu pamoja na Yehova.
A. P., Ujerumani