Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Maktaba Mpya ya Aleksandria Haina Vitabu
Jarida la The Wall Street Journal lasema kwamba ile maktaba maarufu ya Aleksandria, “inayojulikana kwa kuwa na vitabu vingi vyenye hekima yote ya wanadamu wakati wa Kristo, . . . iliteketezwa na moto mwaka wa 47 K.W.K. na hatimaye kutoweka katika karne ya 7 W.K.” Ikishirikiana na nchi nyingine za Kiarabu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, Misri imeanzisha maktaba mpya huko Aleksandria na inatumaini kwamba maktaba hiyo itakuwa maarufu kuliko ile ya zamani. “Jengo hilo lina ghorofa nne chini ya ardhi. Maktaba hiyo imezingirwa na kidimbwi cha maji yenye kung’aa na ina lifti 17, madirisha yote yanajisafisha yenyewe na kuna mfumo tata unaoweza kuzima moto bila maji kuathiri vitabu vilivyo nadra.” Hata hivyo, jarida la Journal laendelea kusema kwamba “maktaba hiyo imepungukiwa na jambo moja muhimu. Vitabu.” Jarida hilo laongeza kusema kwamba baada ya mamilioni ya dola kutumika wakati wa miaka mingi ya ujenzi, “pesa zilizotengwa kwa minajili ya kununua vitabu ni chache sana hivi kwamba inambidi msimamizi wa maktaba, . . . Mohsen Zahran, kuomba vitabu ambavyo hutolewa bila malipo.” Tumeshindwa kuajiri msimamizi mkuu wa maktaba kwa sababu “hatuna uwezo wa kumlipa,” asema Bw. Zahran. Maktaba hiyo mpya ina nafasi ya mabuku milioni nane.
Maumivu Bandia
“Watu ambao wamepoteza kiungo huhisi maumivu makali kana kwamba yanatoka kwa kiungo kilichokatwa, au wanahisi msisimko katika kiungo kilichokatwa wanapoguswa uso,” laripoti gazeti la New Scientist. Utando wa nje wa ubongo unapokosa kupokea habari ya utendaji—kwa sababu ya kiungo kukatwa au jeraha la uti wa mgongo—neva zilizo karibu hujikusanya palipokuwa na kiungo na kuanza kutenda kama kiungo hicho,” laeleza gazeti hilo. Gazeti hilo laongeza kusema hivi: “Jambo hilo huwafanya watu kuhisi wana kiungo chao kilichopotea, au kuhisi maumivu daima.”
Harufu Mbaya Mdomoni na Kuajiriwa
“Si kutilia chumvi kusema kwamba kazi-maisha ya watu wengi imeharibiwa na harufu mbaya mdomoni,” asema daktari wa meno Ana Cristina Kolbe katika gazeti la Brazili la mambo ya kibiashara, Exame. “Katika visa visivyo vya kawaida,” asema mwajiri mkuu Leandro Cerdeira, “watu hupoteza kazi moja baada ya nyingine bila hata kufahamu kisababishi.” Katika uchunguzi uliofanywa katika miji miwili mikubwa huko Brazili, asilimia 40 ya watu waliohojiwa walikuwa na tatizo la kutoa harufu mbaya mdomoni (halitosis). Miongoni mwa visababishi vikuu ni mkazo na milo isiyo na makapi. Ili kupunguza tatizo hilo, Dakt. Kolbe apendekeza wenye kunuka mdomo wachukue likizo ya siku chache na wale mboga zaidi. Wafanyakazi wenye harufu mbaya mdomoni wanaweza kupunguza harufu hiyo kwa muda mfupi kwa kusukutua na maji yenye hidrojeni-peroksaidi hafifu.
Kukata Tamaa Kwaongezeka
Ripoti moja ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) yasema kwamba kati ya mwaka wa 1950 na 1995, wastani wa watu waliojiua katika nchi 105 uliongezeka kwa asilimia 60, laripoti gazeti la Le Monde la Ufaransa. Mratibu wa idara ya WHO ya afya ya akili, Dakt. José-Maria Bertolote alikadiria kwamba watu milioni moja wangejiua katika mwaka wa 2000 na wengine milioni 10 hadi milioni 20 wangejaribu kujiua. Lakini idadi kamili huenda ikawa kubwa zaidi. Kulingana na ripoti hiyo, watu wanaojiua kila mwaka ni wengi kuliko watu wanaokufa katika mapigano yote duniani. Miongoni mwa watu wenye umri wa kati ya miaka 15 na miaka 35, kujiua kumekuwa “mojawapo ya visababishi vitatu vikubwa vya vifo,” asema Dakt. Bertolote.
Watu Wenye Kubakwa Afrika Kusini
“Watu milioni moja hubakwa kila mwaka huko Afrika Kusini,” lasema gazeti la World Press Review. Hilo lamaanisha kwamba mtu mmoja hubakwa kila nusu dakika. Makala hiyo yasema kwamba “Afrika Kusini ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ulimwenguni ya watu wenye kubakwa kisha kuuawa.” Ijapokuwa idadi ya watu Afrika Kusini ni milioni 40 tu, ina visa vya ubakaji mara 12 ya visa vinavyotokea huko Marekani ambayo ni nchi ya pili katika orodha ya nchi zenye tatizo
hilo. Makala hiyo yaongezea kusema hivi: “Katika nchi nyingine huenda ukabakwa, ukanyang’anywa mali, au kuuawa. Sivyo ilivyo Afrika Kusini. Huko, utabakwa popote ulipo kabla ya kuuawa. Vitendo vya ubakaji hufanywa sambamba na uhalifu mwingine.” Pia, “watu wanaotaka kujiunga na vikundi vya wahalifu hutakiwa kwanza kumbaka mtu,” na kisha kumuua. Kulingana na gazeti hilo, idadi kubwa ya watoto wanaosumbuliwa kingono na maoni yenye kuenea ya kutojali uhai ni miongoni mwa sababu zinazosababisha hali hiyo. Isitoshe, uchunguzi uliofanywa huko Johannesburg mwaka wa 1998 “ulipata kwamba, wavulana wanaamini kwamba wanawake hufurahia kubakwa ingawa huwa hawaonyeshi na kwamba unapokuwa na mwanamke una haki ya kudai kufanya ngono naye,” yasema makala hiyo.Upasuaji Bila Damu Huko Afrika Kusini
“Kutokana na takwimu zenye kushtua za UKIMWI, mojawapo ya makundi maarufu ya hospitali za watu binafsi huko Afrika Kusini limebadilisha sera yake ya kutoa huduma ya tiba na kuanza kuwatolea wateja wake ‘tiba na upasuaji bila damu,’” laripoti gazeti la The Mercury la Afrika Kusini. “Madhumuni yetu ni kuwachochea madaktari watoe tiba na upasuaji kwa wagonjwa bila kuwatia damu mishipani,” akasema mkurugenzi wa mradi huo, Daktari Efraim Kramer. Ingawa angalau madaktari 800 katika Afrika Kusini hutoa kibinafsi tiba na upasuaji bila damu, hii ni mara ya kwanza kwa kundi la hospitali kuchukua hatua ya kutekeleza mpango huo kote nchini. Daktari Kramer alisema kwamba madaktari “waliitikia vizuri sana.” Gazeti la The Mercury lasema hivi: “Kutokana na madai ya vikundi vya kidini kama vile Mashahidi wa Yehova wanaokataa kutiwa damu, mbinu zenye matokeo za kutoa matibabu bila damu zimetokezwa.”
Vidonge Asili vya Vitamini C
Tunda la azarole, linalojulikana pia kama cheri-mwitu, lina kipenyo cha sentimeta mbili hivi tu. Lakini, kiasi cha vitamini C katika tunda hilo ni mara 50 zaidi ya kile kilicho katika chungwa na mara 100 kuliko limau. Uchunguzi katika Chuo Kikuu cha San Martín huko Tarapoto, Peru, ulionyesha kwamba gramu 100 za limau lenye asidi nyingi kupindukia zina miligramu 44 za vitamini C ilhali tunda la azarole lenye uzito huohuo lina miligramu 4,600 za vitamini hiyo. Yanapoliwa kila siku, matunda manne tu ya “vidonge” hivyo vya asili humudu mahitaji ya mtu mzima ya vitamini C. Kulingana na gazeti la El Comercio, juhudi zinafanywa ili kuona kama inawezekana kukuza tunda la azarole, “linaloharibika kwa urahisi,” kwa madhumuni ya kibiashara ili lichukue mahali pa koka.
Shauri Linalodhuru
“Vyombo vya habari na wanasaikolojia mashuhuri wanapendekeza kwamba inafaa ‘kuonyesha’ hasira,” lasema gazeti la Psychology Today. “Lakini shauri hilo linadhuru badala ya kufaidi.” Kulingana na Brad Bushman, mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Iowa, “kuonyesha hasira hasa huzidisha jeuri.” Uchunguzi ulionyesha kwamba watu ambao “walionyesha hasira” kwa kupiga ngumi mfuko wa mazoezi walikuwa wakaidi na wakatili kuliko watu ambao hawakuonyesha hasira yao. “Watu waliokuwa wamesoma makala iliyozungumzia faida ya kuonyesha hasira kabla ya kuanza kupiga ngumi mfuko wa mazoezi, walionyesha nia ya kutaka kupiga mfuko huo zaidi ya wengine,” yasema makala hayo. Bushman asema kwamba, “badala ya kujaribu kupunguza hasira, ondoa hasira kabisa. Hesabu 1 hadi 10—au hadi 100, ikihitajika—na hasira itapoa.”
Shimo Kubwa Zaidi Katika Ozoni
Mnamo Septemba 2000, setilaiti ya NASA yenye kuchunguza ozoni iligundua kwenye anga la Antaktiki shimo kubwa zaidi kuwahi kuonekana katika tabaka la ozoni. Ndivyo linavyoripoti gazeti la Clarín la Buenos Aires, Argentina. Shimo hilo lilikuwa juu ya eneo lenye ukubwa wa takriban kilometa milioni 28.3 za mraba na lilivunja rekodi ya mapema kwa zaidi ya kilometa 1,000,000 za mraba. Wanasayansi walishangazwa na ukubwa wa shimo hilo. Dakt. Michael Kurylo wa NASA alisema kwamba jambo hilo “limetia nguvu maoni ya wale wanaohangaikia hali dhaifu ya tabaka la juu la ozoni.” Mwanafizikia Rubén Piacentini wa Kamati ya Kitaifa ya Shughuli za Anga ya Argentina, alisema kwamba ingawa shimo hilo kwa sasa liko juu ya Antaktika iliyo ukiwa, “huenda likaenea hadi eneo la kusini mwa [Argentina].” Gazeti la Clarín lasema kwamba ozoni huwa kinga yenye kupunguza athari hatari za mnururisho wa urujuanimno wa jua.