Wanaweza Kutumia Vibaya Vitambulisho Vyako!
Wanaweza Kutumia Vibaya Vitambulisho Vyako!
KIJANA mmoja mwanamke alianza kupokea ujumbe wenye kukera kutoka kwa wanaume kadhaa kupitia kwa mashine yake ya kujibu simu. Halafu akapigiwa simu na mwanamume mmoja, aliyesema kwamba alipendezwa na matangazo yasiyo ya kiadili ambayo mwanamke huyo alikuwa ameweka kwenye Internet. Lakini mwanamke huyo hakuwa hata na kompyuta. Baada ya muda aligundua kwamba mtu fulani alikuwa akitumia jina lake kwenye mtandao wa kompyuta na alikuwa akiweka matangazo kwenye Internet. Isitoshe, mlaghai huyo asiyejulikana alikuwa akiwapa wengine anwani yake, na kuwaelekeza mahali alipoishi, na hata kuwapa mashauri kuhusu jinsi ya kukwepa king’ora cha tahadhari ya wizi nyumbani mwake!
Wengi wetu hatukazii maanani vitambulisho vyetu. Twajijua, na tunaweza kujitambulisha endapo tutaombwa kufanya hivyo. Lakini vifaa vya utambulisho tunavyotumia mara nyingi—cheti cha kuzaliwa, nambari ya utambulisho, * leseni ya udereva, pasi ya kusafiria, vitambulisho vya kitaifa, na vinginevyo—huibiwa kwa urahisi na hata vingine bandia hutengenezwa hivi kwamba uhalifu huo umezua jina jipya, “wizi wa vitambulisho.”
Ulaghai Uliosambaa
Uhalifu wa aina hiyo ni tata sana, hufanywa kisirisiri, na ni hatari sana. Wahasiriwa hugundua ghafula kwamba mtu fulani amekuwa akirundika madeni, kuibia wakopeshaji, na kusababisha hasara nyingine kwa jina lao. Katika nchi fulani sheria huzuia wahasiriwa kulipa madeni hayo, lakini madeni hayo yanaweza kuharibu sifa yao.
Mashirika yanayotekeleza sheria, wataalamu wa mambo ya mikopo, na mashirika mengi ya wateja yanakiri kwamba wizi wa vitambulisho unasababisha hasara ya mabilioni ya dola kila mwaka. Ni vigumu kabisa kujua idadi kamili ya watu wanaoibiwa kupitia wizi wa vitambulisho. Mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ni kwamba mtu anaweza kugundua kitambulisho chake kimeibiwa baada ya miezi mingi kupita. Mashirika fulani yanayotekeleza sheria hufafanua wizi wa vitambulisho kuwa uhalifu unaositawi kwa kasi mno nchini Marekani. Matatizo kama hayo huripotiwa katika nchi nyingine.
Jambo baya hata zaidi ni kwamba wezi hao wanajua kwamba si rahisi kupeleleza wizi wa vitambulisho na kwamba wezi wengi wa vitambulisho hawashtakiwi. “Wahalifu hawadhani kwamba huo ni uhalifu unaowaathiri watu binafsi,” asema Cheryl Smith, mpelelezi wa pekee. “Benki au duka kubwa ndilo linalopata hasara. Hawanuii kumdhuru mtu binafsi.”
Hutaka Sana Kujua Jina Lako
Kwa kawaida wezi wa vitambulisho huiba habari fulani muhimu kukuhusu, kama vile nambari ya utambulisho au leseni ya udereva. Kisha wao hujifanya kuwa wewe na kutumia habari hiyo kufungua akaunti za mikopo kwa jina lako. Kisha wao, huelekeza hati zote zinazohusika kwa anwani yao. Wao hutumia fedha nyingi wawezavyo na haraka iwezekanavyo. Wakusanyaji wa malipo ya mikopo wanapoanza kukupigia simu ndipo unapogutuka.
Walaghai hao huibaje habari za kibinafsi? Ni rahisi sana. Kwanza wao hukusanya habari za kibinafsi ambazo kwa kawaida watu wengi huandika kwenye maombi ya mikopo au huwapa wale wanaofanya biashara kwa njia ya simu. Wahuni fulani huchokora mapipani—na kutafutatafuta rekodi zako za benki, za rehani, au za mikopo. Wengine huiba barua zenye habari za kifedha kutoka kwenye masanduku ya posta. ‘Wanyemeleaji’ ni wezi wanaotumia kamera au darubini kuchungulia wahasiriwa wanapobonyeza nambari kwenye mashine za kutunza na kutoa fedha (ATM) au simu za umma. Katika nchi nyingine habari chungu nzima za kibinafsi hupatikana kwa urahisi kortini, katika rekodi za umma, au kwenye Internet.
Kuharibu Sifa Yako Njema
Mhuni huyo akisha pata nambari yako ya utambulisho, huenda akahitaji pia habari nyingine za utambulisho, kama vile tarehe yako ya kuzaliwa na anwani na nambari yako ya simu. Akiwa na habari hizo, na labda akiwa na leseni bandia ya udereva yenye picha yake, mwizi huyo aweza kuanza uhalifu. Mwizi mwenyewe huomba mkopo moja kwa moja au kupitia kwa barua, huku akijifanya kuwa wewe. Mara nyingi yeye hupeana anwani yake mwenyewe, akidai kwamba amehama. Wachunguzi wa mikopo hutoa mikopo haraka-haraka na mara nyingi hawaangalii kama habari au anwani za waombaji ni za kweli au la.
Mara tu mlaghai huyo anapofungua akaunti ya kwanza, anaweza kuitumia akaunti hiyo mpya pamoja na habari nyingine za utambulisho ili kuthibitisha uaminifu wake. Jambo hilo hurahisisha harakati zake za ulaghai. Sasa mwizi huyo anaelekea kuwa tajiri huku akiharibu sifa yako njema.
Kurekebisha madhara hayo si kazi rahisi, kwaweza kuchukua muda, na kuvunja moyo. Mari Frank, wakili kutoka California, aligundua ugumu wa kufanya hivyo wakati mlaghai mmoja aliporundika deni la takriban dola 100,000 za Marekani kwa jina lake. Asema hivi: “Ilinibidi kuandika barua 90 na kutumia muda wa saa 500 nikijaribu kujiondolea lawama.” “Unapambana kudumisha sifa yako njema na hali yako njema. . . . Mara nyingi hujui yule anayefanya hivyo, na wahalifu hao huwa hawashikwi kamwe.”
Hatua za Kuchukua
Iwapo umeibiwa vitambulisho, kuna hatua kadhaa unazoweza kuchukua. Kwanza, inapendekezwa kwamba upigie simu idara zinazoshughulikia ulaghai katika mashirika ya kwenu ya mikopo. Kisha waandikie wakopeshaji kuhusu wizi huo na uwaombe wakufahamishe kuhusu maombi yoyote ya mikopo watakayopokea wakati ujao.
Halafu, piga ripoti kwenye kituo cha polisi. Hakikisha kwamba unapata nakala ya ripoti
ya polisi kwa sababu huenda ukaitumia unapowajulisha wakopeshaji.Lazima pia ujulishe benki na makampuni ya kadi za mikopo unayoshirikiana nayo kibiashara. Hata ikiwa mwizi huyo anatumia habari iliyoibiwa kutengeneza kadi mpya za mikopo, utakuwa salama ukiomba kadi nyingine mpya za mikopo. Na ikiwa pesa zimeibiwa pia kutoka kwa akaunti zako za hundi na akiba, huenda ukahitaji kufungua akaunti nyingine mpya. Zaidi ya hayo, huenda ukahitaji kupokea kadi mpya za ATM na nambari mpya za vitambulisho.
Je, Utatuzi U Karibu?
Serikali, mashirika ya kutekeleza sheria, na mashirika ya mikopo yanafanya juu chini kuzuia wizi wa vitambulisho. Katika sehemu nyingine, miswada imepitishwa ili kufanya uhalifu huo kuwa kosa la jinai na kulinda ifaavyo habari za kibinafsi. Hatua nyingine za kitekinolojia zimependekezwa. Zatia ndani kuchapa alama za vidole kwenye kadi kwa kutumia kompyuta, kadi za ATM zinazotambua alama za vidole au sauti ya mtu, kadi ndogo ya kompyuta inayoweza kuhifadhi habari za kibinafsi kama vile aina ya damu na alama za vidole, na kadi zenye nafasi ya kutiwa sahihi isiyofutika.
Mbali na hatua hizo tata za kuzuia wizi huo, kuna tahadhari fulani madhubuti unazoweza kuchukua. (Ona sanduku “Jinsi ya Kujilinda Dhidi ya Wizi wa Vitambulisho.”) Kwa kufikiria kimbele na kupanga mambo kwa uangalifu, yamkini utapunguza hatari ya kuibiwa vitambulisho!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Raia na wakazi wa nchi nyingi huwa na nambari fulani ya utambulisho. Nambari hiyo inaweza kutumiwa si tu kwa ajili ya kujitambulisha kibinafsi bali pia kwa ajili ya utozaji wa kodi na utunzaji wa afya. Huko Marekani, raia huwa na ile inayoitwa Social Security number. Nchi mbalimbali zina majina mbalimbali kwa nambari za utambulisho.
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
Jinsi ya Kujilinda Dhidi ya Wizi wa Vitambulisho
● Julisha wengine nambari yako ya utambulisho inapokuwa lazima tu.
● Usibebe kadi za ziada za mikopo, kitambulisho chako, cheti za kuzaliwa, au pasi yako ya kusafiria kwenye kibeti au pochi yako, isipokuwa iwe lazima.
● Rarua kabisa maombi ya mikopo yaliyokubaliwa kabla ya kuyatupa. Rarua pia taarifa za benki, bili za simu, risiti za kadi za mikopo, na kadhalika.
● Unapotumia mashine ya kutunza na kutoa fedha au unapopiga simu mbali kwa kutumia kadi ya simu, funika mashine hizo kwa mkono wako. ‘Wanyemeleaji’ wenye darubini au kamera waweza kuwa karibu.
● Funga sanduku lako la barua kwa ufunguo ili kuzuia wizi wa barua.
● Chukua hundi mpya kwenye benki badala ya kutumiwa hundi kwa posta.
● Hifadhi orodha au nakala ya nambari zote za akaunti za mikopo, na uziweke mahali salama.
● Usimpe kamwe mtu yeyote nambari yako ya kadi ya mkopo au habari nyingine za kibinafsi kupitia simu ila tu unapokuwa na uhusiano mwaminifu wa kibiashara na kampuni hiyo na umeomba kupigiwa simu.
● Weka akilini nambari yako ya siri ya utambulisho (password). Usiandike nambari hizo na kuzihifadhi kwenye kibeti au pochi yako.
● Omba nakala ya ripoti yako ya mkopo kwa kawaida ikiwezekana.
● Ondoa jina lako kwenye orodha za matangazo ya mashirika yanayotayarisha ripoti za mikopo na za wakopeshaji.
[Picha katika ukurasa wa 20]
‘Wanyemeleaji’ huchungulia wahasiriwa wanapobonyeza nambari kwenye simu za umma au mashine za kutunza na kutoa fedha
[Picha katika ukurasa wa 21]
Wahuni wanaochokora mapipa hutafuta-tafuta kuiba habari ya kibinafsi