Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Endelea Kujifunza Unapozeeka
Kujifunza tekinolojia mpya za kazini, kama vile mifumo ya kompyuta na ya mawasiliano, kwaweza kuwaletea mikazo wafanyakazi fulani wazeewazee, laripoti gazeti la Toronto Star. Mtaalamu wa mielekeo ya kazi, Ann Eby, asema kwamba mara nyingi tatizo ni jinsi wanavyojifunza wala si mambo wanayojifunza. “Tunapozeeka,” asema msimamizi wa Taasisi ya Mafunzo na Usitawi ya Axiom, Julia Kennedy, “utendaji wetu wa neva hupungua, lakini ubongo wetu hubaki ukiwa na afya nzuri.” Tofauti na watoto ambao hujifunza kwa urahisi kwa kukariri bila kufikiri sana maana ya mambo, Kennedy asema kwamba, “watu wazima hulinganisha mambo wanayojifunza na mambo wanayofahamu (kutoka maishani).” Ingawa huenda wafanyakazi wazeewazee wakatumia muda mrefu zaidi kujifunza ustadi tata, bado wanaweza kufanya hivyo. Kennedy atoa madokezo yafuatayo kwa wafanyakazi wazeewazee wanaotaka kujifunza ustadi mpya na ulio tata: Inapowezekana, panga mafunzo yako yaanze asubuhi, jaribu kuelewa mambo makuu badala ya vijambo vidogo-vidogo na uepuke kujilinganisha na wengine.
Akiba ya Mafuta Ulimwenguni Yachanganuliwa Upya
“Baada ya uchunguzi wa miaka mitano, Taasisi ya Uchunguzi wa Kijiolojia ya Marekani [USGS] iliongeza kadirio lake la awali la akiba ya mafuta ulimwenguni pote kwa asilimia 20, kufikia pipa bilioni 649,” laripoti gazeti la Scientific American. “Tulikisia tu na kubashiri kiasi cha [mafuta] ambacho kitagunduliwa katika miaka 30 ijayo,” asema Suzanne Weedman, mratibu wa mpango wa USGS wa Makadirio ya Kiwango cha Mafuta Ulimwenguni wa mwaka wa 2000. Zaidi ya kugunduliwa kwa hifadhi mpya za mafuta, mbinu mpya za kuchimba mafuta zimeongeza kiwango cha mafuta ulimwenguni kwa kuwezesha kampuni za mafuta “kuchimba mafuta zaidi katika hifadhi za sasa,” lasema gazeti hilo.
Kuvaa Nguo Zisizofaa —Je, Kunaathiri Kazi?
Uchunguzi mmoja wa kitaifa huko Australia uligundua kwamba wafanyakazi wa ofisini wanaamini kwamba kuvaa nguo zisizofaa kazini hufanya watu kuzembea, laripoti gazeti la The Sunday Telegraph. Takriban asilimia 42 ya wafanyakazi wa kampuni za kompyuta nchini Australia sasa wanavaa nguo zisizofaa nyakati zote na asilimia 40 ya kampuni katika Australia zina “Ijumaa za kuvaa nguo zisizofaa,” ambapo kila mfanyakazi ana uhuru wa kuvaa apendavyo. Ingawa kuvaa nguo zisizofaa kazini kumetia fora miongoni mwa wafanyakazi, asilimia 17 ya mabosi waliohojiwa waliamini kwamba kuvaa nguo zisizofaa huathiri ubora wa kazi. Wastani huo walandana na maoni ya wafanyakazi wenyewe, asilimia 21 ya wanawake na asilimia 18 ya wanaume wanasema kwamba kuvaa nguo zisizofaa huathiri ubora wa kazi.
Uharibifu wa Mafuriko Msumbiji
Mwezi huu mwaka jana, mafuriko yaliwaacha watu zaidi ya nusu milioni bila makao huko Msumbiji, yaliharibu thuluthi ya zao la mahindi na kuangamiza ng’ombe zaidi ya 20,000. Huku taifa hilo likijaribu kurekebisha madhara ya mafuriko hayo ambayo yametajwa kuwa mabaya zaidi tangu mwaka wa 1948, wengi walitaka kujua kwa nini yalitokea. Jarida la African Wildlife lilisema kwamba ukuzi wa miji, ulimaji wa nyika na kulisha mifugo kupita kiasi katika sehemu za mto katika nchi jirani za Msumbiji kumeharibu uwezo wa asili wa nyika na vinamasi wa kuhifadhi maji ya mafuriko. Kwa hiyo, maji ya mvua kali hugeuka haraka kuwa kijito kinachokwenda kasi. Mratibu wa mradi mmoja wa vinamasi huko Afrika Kusini, David Lindley, asema hivi: “Kile ambacho wanadamu wamefanya kwa kiburi na upumbavu wao usio na kifani, ni kuchafua vinamasi na kuharibu hali ya asili ya mito yetu.”
Ng’ombe na Gesi Inayoongeza Joto Ulimwenguni
Gesi ya methani imetajwa kuwa yenye uwezo mkubwa zaidi ya mara 20 wa kuongeza joto ulimwenguni pote kuliko kaboni dioksidi. Inakadiriwa kwamba tani milioni 100 za methani hutokezwa ulimwenguni pote kila mwaka na ng’ombe, kondoo na mbuzi wapatao bilioni mbili. Kwa mujibu wa gazeti la The Canberra Times, mifugo hutokeza asilimia 13 ya gesi zinazoshirikishwa na ongezeko la joto huko Australia, ilhali katika New Zealand hutokeza asilimia 46 hivi. Vijiumbe
katika tumbo la wanyama-wacheuzi humeng’enya nyasi na kutokeza methani ambayo hutoka nje kupitia kinywa cha mnyama. Katika jitihada za kupunguza ongezeko hilo la joto ulimwenguni pote linalosababishwa na wanyama, wanasayansi wanafanya majaribio ya kuzidisha kiasi cha maziwa yanayokamuliwa kwa kila mnyama na wakati uleule wakipunguza methani inayotokezwa na wanyama.Uwongo Kuhusu Uvutaji-Sigareti Wafichuliwa
“Wazo la kwamba wavutaji sigareti si mzigo wa kiuchumi kwa mashirika yanayotoa huduma za afya kwa kuwa wao hufa mapema si kweli,” laripoti gazeti la Globe and Mail la Kanada. Watafiti Waholanzi waliochunguza hali ya afya ya Waholanzi na Wamarekani wapatao 13,000, waligundua kwamba wavutaji sigareti waliishi muda mrefu zaidi wakiwa walemavu kuliko watu wasiovuta sigareti. Dakt. Wilma Nusselder wa kitengo cha afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Erasmus, huko Rotterdam aandika hivi: “Kutupilia mbali uvutaji-sigareti kutaongeza muda wa kuishi bila ulemavu na pia kupunguza muda wa kuishi na ulemavu.” Kwa mujibu wa gazeti la Globe, “kuna wavutaji sigareti wapatao bilioni 1.15 ulimwenguni pote, idadi hiyo ni thuluthi moja ya watu wazima duniani. Wavutaji sigareti wapatao milioni 943 wanaishi katika nchi zinazositawi.”
Watoto na Magonjwa Yanayoambukizwa Kingono
“Watoto wenye umri wa miaka 11 wanatibiwa magonjwa yanayoambukizwa kingono,” laripoti gazeti la The Times la London. Mji mmoja huko Uingereza una maradufu ya wastani wa kitaifa wa ugonjwa wa kisonono, na msichana 1 kati ya 8 ana ugonjwa wa klamidia. Maambukizo ya klamidia huko Uingereza yameongezeka karibu maradufu tangu mwaka wa 1995 na yameongezeka mara moja kwa tano miongoni mwa vijana katika mwaka uliopita pekee. Ongezeko la kitaifa la ugonjwa wa kisonono la asilimia 56 kwa miaka mitano limewaathiri vijana hasa.
Atumia Kichwa Chake
Malkia wa chungu aina ya Blepharidatta conops wanaopatikana katika nyika za Brazili ana kichwa kikubwa kilicho bapa na mviringo. Kulingana na toleo moja la jarida la National Geographic, la Brazili, chungu hao hutumia kichwa hicho cha ajabu kufunika tundu linaloelekea kwenye chumba cha kuhifadhia mayai, mabuu na viluwiluwi ili adui wasiingie. Kuta za chumba cha malkia zimetengenezwa na miili mifu ya wadudu iliyokusanywa na chungu wafanyakazi. Baada ya kufyonza umajimaji na kuondoa misuli yote kutoka miili hiyo, chungu wafanyakazi hujengea malkia chumba na kuacha tundu lenye saizi sawa na kichwa chake. Chungu wafanyakazi hupata kibali cha kuingia katika chumba hicho cha pekee kwa kugota kichwa cha malkia kwa njia fulani.
Wezi wa Umeme
Kampuni za umeme kotekote Marekani zimeanza harakati za kukomesha tatizo lenye kuongezeka—wizi wa umeme. Zamani umeme ulionwa kuwa wa gharama nafuu sana usiweze kuibiwa, lakini gharama ya umeme imepanda kwa kiwango kikubwa katika miaka ya karibuni ikisababisha wizi wa umeme kuwa jambo la kawaida, lasema jarida la The Wall Street Journal. Kwa mfano, Edison Company ya Detroit yakadiria kwamba katika mwaka wa 1999 wezi waliiba umeme wa thamani ya dola milioni 40. Wezi hao, bila kutambua hatari iliyopo, wameonekana wakitumia vifaa duni sana kama vile nyaya za kuwashia magari, nyaya za soketi, na bomba la shaba. Wezi wengine wamechimba chini ili kuiba umeme kwenye kebo kuu za ardhini za kampuni ya umeme.
Je, Hakuna Mtu Aliyemkosa?
Hivi majuzi mwili uliokauka wa mwanamume mmoja ulipatikana ndani ya chumba kimoja huko Helsinki, Finland. Fundi mmoja aliyekuwa akiunganisha king’ora cha moto aliona rundo kubwa la barua mlangoni na kupigwa na uvundo. Polisi walioitikia mwito wake walipata kwamba mwenye nyumba mstaafu mwenye umri wa miaka 55, aliyeishi mle peke yake, alikuwa amekufa yapata miaka sita iliyopita. Kama lilivyoripoti gazeti la Helsingin Sanomat, kwa muda huo wote Taasisi ya Bima ya Jamii ilikuwa ikilipa malipo yake ya uzeeni nayo ofisi ya kutoa huduma za jamii ilikuwa ikilipa kodi ya chumba chake, ingawa hakuna mtu yeyote kutoka kwa mashirika hayo aliyewahi kumtembelea. Hata watoto wake wakubwa wanaoishi mjini hawakumkosa. “Kwa muda wa miaka sita mtu anaishi katika jumuiya—si katika kisiwa jangwani, bali katikati ya jumuiya ya mjini—wala hakuna mtu hata mmoja anayemkosa na kutaka kujua mahali alipo mtu huyo au lililompata,” alistaajabu Bi. Aulikki Kananoja, mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Jamii huko Helsinki.