Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wahitaji Bima?

Je, Wahitaji Bima?

Je, Wahitaji Bima?

BIMA fulani ni za lazima katika nchi fulani. Katika nchi nyingine, bima nyingi hata hazijulikani. Isitoshe, gharama ya bima na fidia inayotolewa hutofautiana sana nchi hadi nchi. Lakini kanuni ya msingi ya bima—kushiriki hatari—haibadiliki.

Kwa kawaida, mtu anayemiliki mali nyingi huwa katika hatari ya kupata hasara kubwa. Vivyo hivyo, athari zinakuwa kubwa zaidi wakati mtu aliye na wajibu mkubwa zaidi wa kifamilia anapokufa au kulemaa. Kuwa na bima kwaweza kuondoa mahangaiko kuhusu hatari ya kupoteza mali au kulemazwa na aksidenti.

Lakini, je, ni hekima kukata bima ingawa huenda mtu asidai kamwe malipo? Je, kubeba gurudumu la ziada garini ni kupoteza fedha kwa kuwa huenda gurudumu hilo lisitumiwe? Dereva aweza kuchochewa kununua gurudumu la ziada kwa sababu linamfanya ajihisi akiwa salama. Ijapokuwa malipo ya kifedha hayawezi kugharimia hasara fulani, huenda yakagharimia hasara nyinginezo.

Bima hugharimia hasara zipi?

Aina za Bima

Bima nyingi zinazokatwa na watu huainishwa chini ya bima za mali, wajibu, afya, ulemavu, na bima ya maisha.

Bima ya mali: Kukata bima kwa uharibifu wa mali—nyumba, biashara, gari, au mali nyinginezo—ni miongoni mwa mipango maarufu sana ya kudhibiti hasara. Hiyo ndiyo bima ambayo John, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, aliamua kutokata kwa ajili ya karakana na vifaa vyake vya useremala.

Bima fulani za nyumbani hutia ndani bima ya vifaa fulani vilivyo nyumbani. Endapo unakata bima hii, ni hekima kwako kuorodhesha vifaa vyako vya nyumbani vyenye bima, na uvipige picha au kuvirekodi kwenye video ikiwezekana. Orodha hiyo pamoja na makadirio yoyote au risiti za ununuzi wa vifaa hivyo yapasa kuhifadhiwa mahali salama wala si nyumbani mwako. Madai ya bima yaweza kushughulikiwa haraka zaidi ukiwa na rekodi hizo.

Bima ya wajibu: Mtu yeyote anayeendesha gari, anayemiliki nyumba au mali nyingine isiyohamishika, anayeendesha biashara, au kuajiri wengine ana wajibu wa kulipia hasara ya aksidenti. Aksidenti hiyo yaweza kusababisha uharibifu wa mali, majeraha au kifo cha mtu mwingine. Dereva wa gari au mmiliki wa mali au biashara aweza kuwajibika kulipa gharama ya urekebishaji wa mali au ya matibabu au hata kwa ajili ya maumivu na mateso yanayompata mwingine. Katika nchi nyingi waajiri na madereva wanatakiwa na sheria kuwa na bima ya wajibu ili kulipia gharama hizo. Hata mahali ambapo bima si takwa la kisheria, dereva, mmiliki wa mali, au mwajiri aweza kuwa na wajibu wa kisheria au wa kiadili wa kuwasaidia wahasiriwa wa aksidenti au familia zao.

Bima ya afya: Nchi nyingi zina bima fulani inayogharimiwa na serikali ambayo inaandaa malipo kama vile malipo ya uzeeni na kulipia matibabu ya wazeewazee. Lakini, hata katika nchi zenye mpango huo, bima hiyo yaweza kulipia tu sehemu ya gharama za matibabu au yaweza kulipia tu matibabu fulani. Kwa hiyo, baadhi ya watu hukata pia bima binafsi ili kuwasaidia kulipia gharama zinazosalia. Katika sehemu nyingi wafanyakazi wanaweza kukatiwa bima ya afya wanapoajiriwa.

Mipango fulani ya huduma ya afya, kutia ndani mipango ya utunzaji wa afya na mashirika ya huduma ya afya (HMO), huandaa utunzaji muafaka wa kitiba kwa ada fulani ya kila mwezi au mwaka. Mashirika hayo hujitahidi kupunguza gharama kwa kuandaa huduma za kitiba za gharama ya chini na kwa kuzuia magonjwa. Hata hivyo, katika shirika la HMO, mgonjwa huweza tu kuhudumiwa na madaktari fulani tu au kupokea tiba fulanifulani tofauti na bima ya kawaida ya afya.

Bima ya ulemavu na bima ya maisha: Bima ya ulemavu humpa marupurupu fulani mtu aliyejeruhiwa kiasi cha kutoweza kufanya kazi. Bima ya maisha huwasaidia kifedha wale wanaomtegemea mtu fulani endapo anakufa. Bima hizo zimesaidia familia nyingi kulipa madeni na kujiruzuku maishani baada ya mkimu wa familia kujeruhiwa au kufa.

Kupata Watoa-Bima Wenye Kutegemeka

Bima hutegemea mpango wa kulipa fedha sasa ili kupata ulinzi wa kifedha wakati ujao, kwa sababu hiyo biashara ya bima huvutia walaghai wengi sana. Ndivyo ilivyo katika nchi zinazositawi na zile zilizositawi kiuchumi. Kwa hiyo, ni hekima kujihadhari na zile zinazoitwa eti bima za malipo nafuu na mipango mingine ya bima yenye kutiliwa shaka. Wateja wengi sana wenye matumaini wameambulia patupu wakati makampuni hayo yanaposhindwa kulipa madai yao—au yanapotokomea ghafula!

Kama ilivyo na ununuzi mwingineo muhimu, ni hekima kulinganisha malipo ya makampuni mbalimbali ya bima, na mara nyingi kufanya hivyo huokoa fedha. Mathalani, makampuni fulani hutoza malipo ya chini ya bima ya afya kwa wale wasiovuta sigareti na ya bima ya gari kwa wale waliofaulu mtihani wa udereva. Mteja anayetafuta bima anaweza kupataje kampuni ya bima inayotegemeka?

Hatua ya kwanza yaweza kuwa kujua maoni ya watu wengine kuhusiana na makampuni na mawakala mbalimbali wa bima. Huenda marafiki na majirani wakajua ubora wa huduma zinazotolewa na kampuni fulani au unyoofu na upendezi binafsi kuelekea wateja wa wakala fulani. Ni vizuri kuwa chonjo kusikia habari zinazotaja makampuni ya bima yenye matatizo.

Isitoshe, rekodi ya kampuni na hali yake ya kifedha yaweza kuchunguzwa kwa kusoma miongozo ya kutathmini makampuni ya bima inayopatikana katika maktaba au maduka ya vitabu au kwenye Internet. Miongozo hiyo yaweza kujibu maswali kama vile: Je, kampuni hiyo ni salama kifedha? Je, imekuwa ikitoa bima kwa mafanikio kwa miaka mingi? Je, yajulikana kwa kushughulikia madai himahima na kwa njia ya kirafiki?

Hata hivyo, miongozo ya kutathmini makampuni ya bima haipasi kuonwa kuwa haiwezi kukosea. Kampuni moja ya bima yenye rasilimali za mabilioni ya dola na iliyodumu kwa muda mrefu, ilichukuliwa na serikali juma moja tu baada ya kusifiwa kuwa bora zaidi na kitabu kimoja maarufu!

Kazi ya Mawakala wa Bima

Kwa kawaida wakala wa bima huwakilisha kampuni mahususi ya bima. Dalali, au wakala aliyejiajiri, aweza kuwasiliana na makampuni mbalimbali ya bima ili kujua bima bora iliyopo kwa malipo fulani hususa. Wote wanahitaji kudumisha uhusiano mzuri na wateja ili biashara yao ifaulu. Wakala wa bima anaweza kuwasaidia sana wateja wake akiwa mwenye kutumainika na akipendezwa nao kibinafsi.

Kwanza, wakala au dalali mzuri anaweza kumsaidia mteja kuchagua bima inayofaa kati ya orodha ndefu ya bima zilizopo. Atamweleza pia mteja wake kinaganaga kuhusu bima hiyo. Kama wengi wajuavyo, hati za bima huwa na mambo mengi sana. Msimamizi wa kampuni moja ya bima alikiri kwamba hakufahamu masuala mengine ya bima ya nyumba yake!

Maelezo ya wakala yanaweza kumsaidia mteja aepuke kutamauka. Kwa mfano, bima nyingi za mali na afya zinatozwa ada fulani. Hicho ni kiasi fulani hususa ambacho lazima mteja wa bima alipe—tuseme, kwa ajili ya urekebishaji wa gari au gharama za matibabu—kabla kampuni ya bima haijalipa fungu lake la madai. Wakala anaweza pia kumtetea mteja wake endapo mteja huyo anakosa kulipwa na kampuni ya bima.

Bima na Wakristo

Je, Mkristo anayetumaini kupata msaada wa Mungu na ambaye anatarajia mwisho wa mfumo wa mambo anahitaji bima? Huko nyuma katika mwaka wa 1910, watu fulani walimwuliza swali hilo Charles Taze Russell, mhariri wa gazeti ambalo leo linajulikana kama Mnara wa Mlinzi, na gazeti-jenzi lake la Amkeni! Russell alikiri kwamba Biblia hutabiri mwisho wa mfumo wa sasa wa kiuchumi, lakini akaongezea kwamba yeye binafsi hakuwa na bima ya maisha.

“Lakini hali za watu zinatofautiana,” akasema Russell. “Baba anayetegemewa na mke na watoto—ikiwa watoto hao ni wachanga mno kujiruzuku—ana wajibu kuwaelekea.” (1 Timotheo 5:8) Mwanamume anaweza kutenga fedha kwa ajili ya familia yake, akasema Russell. “Na kama hawezi kufanya hivyo, anaweza kutimiza wajibu wake kuwaelekea kwa kuwawekea bima ya maisha.”

Yule mwenye wajibu wa familia anaweza pia kuwaandalia washiriki wake bima ya afya, ulemavu, na bima nyinginezo. Waseja wengi hukata bima ili kuweza kupokea huduma muhimu vilevile kuepuka kuwa na deni kwa sababu ya aksidenti au ugonjwa.

Unyoofu ni muhimu sana kwa habari ya bima. Mkristo wa kweli hatadanganya kamwe kampuni ya bima, ama anapojaza ombi la bima au anapodai malipo. (Waebrania 13:18) Atakumbuka kwamba kusudi la bima ni kugharimia hasara. Si tiketi ya bahati nasibu—fursa ya kuishi raha mustarehe.—1 Wakorintho 6:10.

Wakristo hutii sheria zote zinazohusiana na matakwa kama vile kukata bima. Wao hutii wakati ambapo sheria husema kwamba lazima wawe na bima inayofaa ili kuendesha biashara au kuendesha gari. (Waroma 13:5-7) Mtu mnyoofu na mwenye hekima inayotumika hulipa pia malipo yote ya bima. Kampuni yaweza kufutilia mbali bima na kukataa kulipa madai ikiwa bima hailipiwi. Ni jambo la busara kuhakikisha mara kwa mara kwamba bima inalipiwa kwa kuwasiliana moja kwa moja na kampuni hiyo na kuhifadhi hati ya malipo, kama vile nakala ya hundi ulizolipa.

Iwe bima yapatikana unakoishi au la, kuna tahadhari za msingi zinazoweza kukusaidia uepuke hasara na hivyo kujilinda na kuwalinda wapendwa wako kutokana na maumivu ambayo hayawezi kuponywa na madai yoyote ya bima. Sasa tutachunguza baadhi ya tahadhari hizo.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wakala anayetumainika anaweza kukusaidia kufanya maamuzi kuhusu bima

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wengi wana bima, iwe ni takwa la kisheria au la