Kula Mboga!
Kula Mboga!
Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Brazili
“Ni chungu.” “Zina ladha mbaya sana.” “Sijawahi kamwe kuzila.”
HIZO ni baadhi tu ya sababu chache zinazowafanya wengi wakatae kula mboga. Vipi wewe? Je, wewe hula mboga kila siku? Amkeni! liliwahoji watu kadhaa ili kutafuta sababu inayowafanya watu fulani wapende mboga ilhali wengine wasizipende.
Wale wanaokula mboga walisema kwamba wazazi wao waliwafunza umuhimu wa kula mboga, jamiikunde, na matunda. Kinyume chake, wengi ambao hawapendi mboga hawakuzoezwa kula mboga walipokuwa watoto. Badala yake, walipendelea kula chakula kisichojenga mwili. Hata hivyo, hata hao walikubali kwamba mboga ni muhimu katika kudumisha afya njema.
Wazazi wazoezeni watoto wenu kula mboga! Jinsi gani? Kichapo Ukweli Kuhusu Maisha, kilichochapishwa na Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, chapendekeza kwamba angalau mara moja kwa siku baada ya kuwanyonyesha matiti au kuwalisha kwa chupa, watoto wachanga wenye umri wa miezi sita hivi wapasa kulishwa mboga zilizochemshwa, kumenywa, na kisha kupondwa. Kadiri mtoto alavyo vyakula mbalimbali, ndivyo anufaikavyo. Dakt. Vagner Lapate, mtaalamu Mbrazili wa mambo ya watoto, asema kwamba ingawa maziwa ni mlo mkuu kwa miaka miwili ya kwanza, kuanza kumlisha vyakula vingine “humchochea mtoto mchanga kupenda vyakula vipya.”
Katika kitabu Medicina—Mitos y Verdades (Dawa—Ngano na Ukweli), Carla Leonel adokeza kwamba kiasi kidogo cha maji ya machungwa, rojo ya matunda (kama vile ndizi, matofaa, na mapapai), nafaka, na mchuzi wa mboga waweza kuongezwa kwa chakula cha mtoto mchanga mapema kuliko inavyopendekezwa hapo juu. Bila shaka, kwa sababu kuna maoni mbalimbali kuhusu suala hilo, ingekuwa vyema kuwasiliana na daktari wa mtoto wako.