Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kasoro Yenye Gharama Kubwa
Wahandisi wa kompyuta waliterema kwa sababu mifumo mingi ya kompyuta ilivuka mwaka wa 1999 na kuingia mwaka wa 2000 bila matatizo. Wachunguzi fulani walikuwa wamebashiri kwamba mifumo mingi ya kompyuta, kwa kushindwa kutofautisha 1900 na 2000 kwa sababu ya utaalamu fulani wa kutayarisha programu ulioacha herufi mbili za kwanza za tarehe za mwaka, ingeacha kufanya kazi kwa ghafula na kusababisha mvurugo mkubwa. (Ona toleo la Amkeni! la Februari 8, 1999, ukurasa wa 21-23.) Ili kuzuia jambo hilo, wataalamu wa kompyuta walitia bidii kurekebisha mifumo hiyo kabla ya tarehe hiyo muhimu. Iligharimu kiasi gani? Kulingana na makala moja katika gazeti la kila siku la Ufaransa, Le Monde, shirika moja la kifedha lilikadiria gharama hiyo kuwa “kati ya dola bilioni 300 na dola bilioni 600 za Marekani ulimwenguni pote.” Marekani ilitumia takriban dola bilioni 100; nayo Ufaransa ikatumia dola bilioni 20 za Marekani. Kwa kulinganisha, Vita vya Ghuba viligharimu jeshi la muungano “kati ya dola bilioni 46 na dola bilioni 60 za Marekani.” Hata hivyo, jarida la The Wall Street Journal lasema kwamba “hali hiyo itatokea tena . . . kukiwa na matatizo mapya chungu nzima yenye kuhusiana na nambari katika kompyuta yatakayohitaji kushughulikiwa.” Lakini “hakuna tatizo hata moja kati ya hayo linaloweza kufikia kiwango cha Kasoro ya Kompyuta ya Mwaka wa 2000.”
Matatizo ya Neno la Siri
Maneno ya siri yaliyosahauliwa hugharimu makampuni mengi katika Marekani mamilioni ya dola kila mwaka kupitia kupoteza wakati na uhitaji wa kupata msaada wa kiufundi. Gazeti la The New York Times lasema kwamba “miaka 20 iliyopita, watu walihitaji tu kukumbuka Social Security number [namba ya kitambulisho] na labda pia namba moja au mbili za simu.” Lakini sasa, matumizi ya maneno ya siri ili kufungua faili za kompyuta na E-mail mahali pa kazi limekuwa jambo la kawaida kwa watu wengi. Kwa kweli, ni jambo la kawaida watu kuwa na maneno mengi ya siri, alama za siri, na namba za kujitambulisha. Yaripotiwa kwamba msimamizi mmoja wa mifumo ya kompyuta anatumia maneno ya siri zaidi ya 129 kwa sasa. Makampuni fulani yanatupilia mbali mifumo yenye kuhitaji maneno ya siri na badala yake kutumia mifumo yenye kuchunguza alama za vidole na vifaa vingine vya ulinzi vya tekinolojia ya juu zaidi.
Hasira na Moyo Wako
Ripoti moja katika gazeti la Globe and Mail yasema kwamba “watu wenye kukasirika upesi wanaelekea kupatwa na mshtuko wa moyo mara tatu zaidi ya watu wasio wepesi wa hasira.” Takriban watu 13,000 walishiriki katika uchunguzi wa miaka sita wa kukadiria hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo. Washiriki wote hawakuwa na ugonjwa wa moyo mwanzoni mwa uchunguzi huo. Kila mmoja wao aliulizwa maswali kadhaa ili kuamua kama ana kiwango cha chini, cha kadiri, au cha juu cha hasira. Wakati wa kipindi hicho cha miaka sita, watu 256 miongoni mwao walikuwa wamepatwa na mshtuko wa moyo. Uchunguzi huo ulifunua kwamba watu wenye kiwango cha kadiri cha hasira walikuwa na uwezekano wa asilimia 35 wa kupatwa na matatizo ya moyo. Mwandikaji mkuu wa uchunguzi huo, Dakt. Janice Williams, wa Chuo Kikuu cha North Carolina, asema hivi: “Hasira inaweza kusababisha mshtuko wa moyo, hasa katika wanaume na wanawake wa makamo wenye msukumo wa kawaida wa damu.” Kwa hiyo, wachunguzi hao walipendekeza kwamba watu wenye kukasirika upesi wapaswa kufikiria kutumia mbinu za kupunguza mkazo.
Habari Mpya Juu ya Kuvuta Sigareti
Toleo la Worldwatch Issue Alert laripoti kwamba “baada ya karne nzima ya kuimarika kwa uvutaji wa sigareti, ulimwengu sasa unageuzia sigareti kisogo.” Kuanzia mwaka wa 1990 hadi mwaka wa 1999, uvutaji wa sigareti ulishuka kwa asilimia 11 ulimwenguni pote. Mwelekeo huo umeendelea katika Marekani kwa miongo miwili hivi, huku idadi ya sigareti zinazovutwa Marekani ikiwa imepungua kwa asilimia 42 katika mwaka wa 1999 ikilinganishwa na mwaka wa 1980. Ripoti hiyo inataja kwamba upungufu huo umesababishwa na kampeni za kupinga uvutaji wa sigareti, kuenea kwa habari zinazoeleza hatari zinazohusiana na uvutaji wa sigareti, na kupanda kwa bei ya sigareti. Kwa kuongezea, ripoti hiyo inasema kwamba, “idadi ya sigareti zinazovutwa na mtu mmoja-mmoja zimepungua kwa asilimia 19 kutoka kilele cha juu zaidi cha 1985 katika Ufaransa, asilimia 8 tangu 1990 katika China, na asilimia 4 tangu 1992 katika Japani.”
Ugonjwa Wapuuzwa na Wasio na Bima
Uchunguzi wa hivi karibuni katika Marekani waonyesha kwamba watu wasio na bima ya tiba wanaelekea kupuuza dalili za ugonjwa na hupuuza kwenda hospitalini, laripoti shirika la habari la
Reuters. Uchunguzi huo uliochapishwa kwanza katika jarida la Archives of Internal Medicine, ulitokana na habari iliyokusanywa na Kituo cha Kitaifa cha Takwimu za Afya. Uchunguzi ulionyesha kwamba hata waonapo dalili za ugonjwa mbaya, kama vile matatizo ya kuona au kutokea kwa uvimbe katika titi, watu wasio na bima ya tiba walielekea kupuuza kwenda hospitalini kuliko watu waliokuwa na bima. Ripoti hiyo ilisema hivi: “Inashangaza kwamba wakati taifa letu linaimarisha ‘Mswada wa Haki za Mgonjwa’ bado hatujaimarisha haki ya kuwa mgonjwa.”Bustani ya Wanyama ya London ya Enzi za Kati
Uchimbaji chini ya Mnara mashuhuri wa London umefunua mambo mapya kuhusu “bustani ya wanyama ya enzi za kati iliyokuwa na wanyama mbalimbali wasio wa kawaida,” laripoti gazeti la The Sunday Times la London. Wachunguzi wanasema upo uthibitisho kwamba aina 100 za wanyama walihifadhiwa wakati mmoja kwenye eneo ambalo sasa ni Mnara wa Magharibi, wanyama hao walitia ndani kifaru, paa, simbamarara, mbuni, nyoka, na aligeta. Wataalamu wamejua kuwapo kwa bustani hiyo kwa muda fulani, lakini uchunguzi mpya kwenye hifadhi za kifalme za nyaraka, chuo kikuu, na hifadhi za kanisa, kutia ndani habari kutoka chimbo hilo, umefanya mambo kadhaa yaeleweke wazi. Bustani hiyo ilianzishwa mwaka wa 1210 na Mfalme John na kufungwa mwaka wa 1835 wakati Bustani ya Wanyama ya London ilipoanzishwa katika Mbuga ya Regent. Baadhi ya wanyama walihamishwa wakati huo hadi bustani hiyo mpya ilhali wengine walipelekwa Marekani. Kuendelea kuwepo kwa bustani hiyo kulitegemea wafalme na waandamizi wao pamoja na amani ya kadiri iliyokuwa nchini wakati huo. Mweka-nyaraka mkuu katika Mnara huo, Geoffrey Parnell, asema hivi: “Kwa wazi bustani hiyo ilikuwa sarakasi iliyodumu kwa muda mrefu zaidi katika London, iliyowafurahisha wafalme na watu wa kawaida kwa karne nyingi.”
Hukumu ya Papo Hapo
Mahakimu watatu katika jimbo la Espírito Santo, Brazili, wanafanya majaribio ya programu ya kompyuta ambayo imekusudiwa kutoa hukumu ya papo hapo, laripoti gazeti la New Scientist. Programu hiyo inayoitwa Hakimu wa Kielektroni, hutumia kompyuta ndogo. Aksidenti ndogo itokeapo, polisi watamleta hakimu pamoja na karani wa mahakama palipotokea aksidenti. Programu hiyo imekusudiwa kumsaidia hakimu mwanadamu kukadiria uthibitisho uliopo na kutoa hukumu papo hapo. Inatoa usaidizi huo kwa kumwuliza hakimu huyo mfululizo wa maswali, kama vile “Je, dereva alisimama penye taa?” au “Je, dereva ametumia kileo kupita kiwango kinachoruhusiwa kisheria?” Kisha itachapisha hati ya uamuzi ikionyesha sababu za uamuzi huo. Kwa mujibu wa New Scientist, programu hiyo yaweza pia kutoza “faini, kuamuru hasara ilipwe na hata kupendekeza hukumu ya kifungo gerezani.” Inatazamiwa kwamba programu hiyo ya kompyuta itawasaidia mahakimu wanadamu kufanya kazi kwa wepesi zaidi na hivyo kusaidia kupunguza mzigo unaolemea mfumo wa mahakama nchini Brazili.
Maji Yavutia Wateja
Wafanya-biashara fulani huko India wametumia kwa faida yao ukame wa hivi karibuni kuwavutia wateja. Wanawapa maji ya bure wale wanaonunua vifaa vya nyumbani vinavyotumia umeme. Gazeti The Times of India liliripoti kwamba mwenye-duka mmoja aliahidi kumpa mteja yeyote atakayenunua oveni, friji, mashine ya kufulia, au televisheni lita 500 za maji kwa siku nne kila juma kwa miezi miwili ya kiangazi. Duka jingine ‘liliahidi kumpa maji ya bure kwa kiangazi chote’ mtu yeyote anayenunua friji au televisheni. Likiwa na ukosefu mbaya zaidi wa maji, eneo la kaskazini-magharibi la Jimbo la Gujarat, limegundua kwamba maji huvutia wateja zaidi kuliko zawadi za dhahabu, fedha, au safari za likizo bila malipo. Katika mji wa Rajkot, wafanya-biashara walisema kwamba kuwavutia wateja kwa maji kumeongeza mauzo yao mara tatu.
Fumbo la Almasi Latatuliwa
Kitu kigumu zaidi cha asili kijulikanacho na wanadamu, almasi, hufanyizwa kaboni inapokuwa kwenye halijoto na kanieneo inayopita kiasi. Lakini ni nini kinachotukia wakati almasi yenyewe inapowekwa kwenye kanieneo inayopita kiasi? Wanasayansi wamekuwa wakijaribu kujibu swali hilo kwa miaka 40—yaani, hadi kufikia hivi karibuni. “Yaonekana kwamba kanieneo inapoelekezwa kwa pembe muafaka ya almasi,” laripoti The Buffalo News, “kitu hicho kigumu zaidi kiasili hugeuka na kuwa grafati, kaboni . . . ileile inayoifanyiza.” Wanasayansi wanasema kwamba wanatarajia kutumia yale ambayo wamejifunza kutokana na uchunguzi huo ili kutokeza vifaa bora zaidi vya almasi.