Kuyalinda Meno Dhaifu
Kuyalinda Meno Dhaifu
MENO yako yalianza kuota lini? Labda utashangaa kujua kwamba yalianza kuota ukiwa bado tumboni—yawezekana hata kabla ya mama yako kutambua alikuwa mjamzito! Kwa hivyo ni muhimu kwa mama mjamzito kula chakula chenye virutubishi vya kutosha, kutia ndani kalisi, fosforasi, protini, na vitamini.
Vipi vitoto vichanga? Wataalamu wanasema kwamba vitoto vinavyolishwa kupitia chupa viko katika hatari ya kuoza meno, hasa meno yaliyoko mbele upande wa juu. Hilo hutukiaje? Baadhi ya vitoto vichanga vina kawaida ya kulala vikiwa na chupa mdomoni yenye maziwa, maji ya matunda, maji yenye sukari, au soda. Vinywaji hivyo vinavyochachuka upesi vina kabohidrati ambamo bakteria husitawi. Nazo bakteria hutokeza asidi inayoweza kuozesha meno ya vitoto—hasa vinywaji hivyo vikibaki mdomoni usiku kucha. Baadhi ya vitoto vyenye meno yaliyooza sana hupoteza meno mapema, jambo ambalo huathiri vibaya ukuzi wa meno ya utu uzima.
Wazazi waweza kulindaje meno dhaifu ya kitoto chao? Inapendekezwa kunyonyesha kitoto, kwa kuwa maziwa ya mama ni safi na yana fingo chungu nzima. Hata hivyo, iwapo chupa itatumika, wataalamu wanasema kwamba inapasa kuacha kutumiwa mtoto afikiapo umri wa miezi 18. Pia wanapendekeza kwa mkazo kwamba, chupa itumiwe tu kumlishia mtoto—wala si kama mbinu ya kumtuliza mtoto. Zaidi ya hilo, iwapo kitoto kitatumia chupa kinapolala, inafaa iwe na maji pekee. Kila mara baada ya mlo, safisha meno ya kitoto kwa kitambaa safi, chororo.
Kuoza meno mapema kwaweza kuzuiwa. Kutunza meno ifaavyo—hata ya kitoto—ni muhimu sana!