Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kupanda Mazao Kwenye Msitu wa Amazon

Kupanda Mazao Kwenye Msitu wa Amazon

Kupanda Mazao Kwenye Msitu wa Amazon

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

KATIKA miaka ya 1990, mamilioni ya eka za misitu ya kiasili ziliharibiwa ulimwenguni pote kila mwaka, likaripoti Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa. Katika Amazon peke yake nchini Brazili, mioto mikubwa ya misitu na ukataji wa miti kwa misumeno ya minyororo tayari imebadili sehemu kubwa ya msitu huo wa mvua iliyo kubwa kupita Ujerumani, kuwa uwanja tu. Badala ya mandhari ya msitu ulioshikamana, sasa msitu huo umejaa mapengo yenye udongo mkavu uliopasuka na kufunikwa na magugu na visiki vinavyopigwa na jua kali.

Ingawa uharibifu huo unaoendelea wa misitu unatisha sana, kuna matumaini. Mradi mmoja unaoleta matumaini tayari umefaulu kwa njia fulani. Unaitwa agroforestry, na kichapo kimoja chaueleza kuwa “mpango ambamo miti inapandwa miongoni mwa mazao au nyasi kwa njia inayonufaisha . . . mazingira na viumbe.” Mradi wa kupanda miti miongoni mwa mazao hufanyaje kazi? Umekuwa na matokeo gani? Tunaweza kutarajia nini wakati ujao? Ili kupata jawabu, Amkeni! lilizuru Taasisi ya Taifa ya Utafiti Katika Amazon (INPA) huko Manaus, mji mkuu wa Jimbo la Amazonas nchini Brazili.

Uhamaji Wenye Kuvunja Moyo

Mtaalamu Mholanzi wa kilimo katika Idara ya Kilimo ya INPA, Johannes van Leeuwen, amekuwa akishirikiana na wakulima katika Amazon kwa miaka 11. Kwanza, wakulima wengi hivyo walikujaje katika msitu wa Amazon? Wakulima wa mashamba madogo walioishi katikati na kusini ya Brazili waliamua kuhama kwa sababu ya ukosefu wa riziki baada ya mashamba yao kunyakuliwa kwa minajili ya ulimaji wa mashamba makubwa kwa kutumia mashine. Wakulima wengine wa zao la kitani, linalotumiwa kutengenezea magunia ya turubai, walipoteza riziki yao wakati mifuko ya plastiki ilipochukua mahali pa magunia hayo. Na bado wengine, walioishi katika maeneo yenye ukame, walilazimika kuhama ili kutafuta maeneo yenye udongo wenye rutuba zaidi. Lakini wangehamia wapi? Walipoahidiwa ardhi, nyumba, na mashamba yenye rutuba katika msitu wa Amazon, walifunga safari na kuingia kwenye msitu huo wa mvua.

Hata hivyo, wakulima hao waligundua upesi kwamba walikuwa wamehamia kwenye eneo lenye mvua nyingi, mvuke mwingi, tabia ya nchi ya joto, na udongo usio na rutuba. Baada ya muda wa miaka miwili hadi minne, udongo ulikuwa umepoteza rutuba kabisa na tatizo lilelile likazuka: watu fukara kwenye udongo usio na rutuba. Wakulima hao wenye kukata tamaa walitatua tatizo hilo kwa kukata miti mingi zaidi na zaidi ili waweze kulima.

Ni kweli kwamba wakulima wa mashamba madogo si kisababishi kikuu cha uharibifu wa msitu wa Amazon. Mashamba makubwa ya mifugo, biashara kubwa za kilimo, uchimbaji wa madini na makampuni yanayokata miti, na miradi ya ujenzi wa mabwawa ya uzalishaji wa umeme wa nguvu za maji vimeharibu sehemu kubwa zaidi. Ijapokuwa hivyo, kuongezeka kwa wakulima wa mashamba madogo na zoea lao la kukata na kuchoma miti kwa ajili ya kilimo kumechangia uharibifu wa msitu huo.

Kupata Habari kwa “Maktaba Zilizo Hai”

“Haidhuru wameharibu msitu huo kadiri gani,” asema Van Leeuwen, “wakulima hao fukara wanaishi hapa na hawana pengine pa kwenda. Kwa hivyo ili kupunguza ukataji wa miti, ni sharti tuwasaidie kupata riziki kutokana na mashamba yao bila uhitaji wa kukata miti zaidi msituni.” Mradi wa kupanda miti miongoni mwa mazao huwa muhimu katika kuwafunza wakulima mbinu ya kilimo inayorutubisha udongo na kuwawezesha kutumia shamba lilelile kwa miaka mingi. Watafiti walibunije mbinu bayana za mradi huo?

Mradi wa INPA wa kupanda miti miongoni mwa mazao ulianzishwa baada ya uchunguzi wa miaka mingi, mahoji, na uchunguzi wa udongo na mimea iliyokusanywa kutoka kwa maeneo hususa. Habari muhimu sana zilikusanywa kwa kuhoji “maktaba zilizo hai”—Wahindi Wekundu na Wakaboklo, jamii ambayo ni mchanganyiko wa weupe, weusi, na Wahindi, ambao mababu zao wa kale walihamia katika bonde la Amazon.

Wakazi hao wa Amazon wana ujuzi maridhawa. Wanaelewa tabia ya nchi ya eneo hilo na udongo wake mbalimbali—mweusi, mwekundu, mweupe, mwekundu-mweusi, na mchanganyiko wa mchanga na udongo—vilevile idadi kubwa ya matunda, vikolezo, na mitishamba iliyo katika msitu huo. Wataalamu wa kilimo na wakulima walishirikiana kufanya utafiti kwa kutegemea ujuzi huo—ushirikiano huo uliboresha utekelezaji wa mradi huo.

Msitu Si Mgodi wa Madini

Mradi wa kupanda miti miongoni mwa mazao ulitekelezwa hatua kwa hatua. Hatua ya kwanza ilikuwa kuwasadikisha wakulima kutoona msitu huo kama mgodi wa madini—wa kuchimbwa na kuachwa tu—bali kuuona kuwa rasilimali inayoweza kurejeshwa upya. Pili, walishauriwa kupanda miti pia badala ya kupanda tu mihogo, ndizi, mahindi, mpunga, maharagwe, na mazao mengine yanayokua upesi. “Miti?” wakauliza wakulima hao. “Kwa nini?”

Iliwabidi watafiti kueleza waziwazi manufaa ya kupanda miti kwa sababu, kwa kawaida wakulima hutoka kwenye maeneo ambako miti si sehemu ya kilimo, na pia hawakufahamu jamii za miti iliyo katika Amazon. Walieleza kwamba udongo wa msituni hauhifadhi virutubishi vinavyohitajiwa na mazao ya chakula. Kwa mfano, maji ya mvua huondoa virutubishi kabla havijafyonzwa na mazao ya chakula kama vile mahindi. Kinyume chake, miti hufaulu kufyonza na kuhifadhi virutubishi na kudumisha rutuba ya udongo. Isitoshe, miti huandaa mlo na kivuli kwa wanyama. Wakulima pia wanaweza kutumia miti kuwa ukigo wa mashamba yao. Na bila shaka, miti ya matunda yaweza kuandaa matunda na kuni ziwezazo kuwaletea riziki.

Wakulima walitiwa moyo pia kupanda miti mbalimbali. Kwa nini? Ili waweze kupata matunda mbalimbali na mbao pia. Kwa kufanya hivyo, mkulima huepuka kuvuna matunda mengi ya aina moja au mbili tu hali inayomlazimu kuyauza kwa bei ya chini kwa sababu kila mtu anauza bidhaa zilezile wakati uleule.

Mradi Mpya Watia Fora

Ni miti gani inayopandwa? “Kwa sasa tunapanda miti ya matunda 30 hadi 40 inayotajwa hapa,” asema mtaalamu wa kilimo Van Leeuwen huku akitupatia orodha ya miti 65 yenye majina yasiyo ya kawaida. Ili kuthibitisha kwamba mradi huo unatia fora, Van Leeuwen aonyesha picha kadhaa zilizopigwa pindi mbalimbali za shamba lililokatwa miti.—Ona sanduku “Jinsi Msitu Unavyoweza Kupandwa Upya.”

Kuzuru masoko ya chakula katika Manaus kwaonyesha kwamba mradi huo mpya wa kupanda miti miongoni mwa mazao unatia fora. Zaidi ya aina 60 za matunda yaliyokuzwa sehemu hii tayari yanauzwa kwenye masoko hayo. Kuhusu wakati ujao, wataalamu wa kilimo wanatarajia kwamba kadiri kilimo cha kupanda miti miongoni mwa mazao kinavyoenea, ndivyo ukataji wa miti utakavyopungua. Kwani, mkulima anapojifunza kulima upya shamba lililotumika, yamkini ataacha kukata miti kwa minajili ya kuanza shamba jipya.

Jitihada hizo zenye kusifika huenda zisikomeshe tisho la ulimwenguni pote la kuangamiza mimea na wanyama wa dunia. Lakini zaonyesha hatua inayoweza kuchukuliwa wakati rasilimali muhimu zinapostahiwa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Machungwa na Acerola Yashindwa

Machungwa, ambayo yajulikana kuwa na vitamini C, hayawezi kufua dafu yalinganishwapo na tunda linaloitwa “malkia mpya wa vitamini C.” Hata acerola, tunda linaloongoza katika utoaji wa vitamini C, haliwezi kufua dafu. Mfalme mpya ni nani? Tunda dogo sana lenye rangi ya zambarau, ambalo lakaribia kutoshana na zabibu na linalokua kiasili katika nyanda za Amazon. Laitwaje? Laitwa Camu-camu. Je, lastahili kuongoza? Gazeti moja la Brazili lasema kwamba gramu 100 za chungwa zina miligramu 41 za vitamini C, ilhali gramu 100 za acerola zina miligramu 1,790 za vitamini C. Lakini, kiasi hicho-hicho cha camu-camu kina miligramu 2,880 za vitamini C—mara 70 zaidi ya kile kilicho katika machungwa!

[Hisani]

Acerola na camu-camu: Silvestre Silva/Reflexo

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

Ustadi wa Kupanda Miti kwa Mpangilio

Baada ya wakulima kukubali kutekeleza kwa sehemu mradi wa kupanda miti miongoni mwa mazao, mtaalamu wa kilimo Johannes van Leeuwen huwapa pendekezo madhubuti zaidi—plani inayoonyesha jinsi shamba litakavyokuwa wakati ujao. Badala ya kuchagua na kuchanganya ovyoovyo miti yoyote tu, picha za kompyuta za mipangilio mbalimbali ya mazao hutumiwa ili kuamua miti inayofaa kupandwa na jinsi inavyopasa kupangwa. Kuna ustadi au mpangilio wa kuipanda kwa vikundi, vikundi vya miti midogo, miti ya wastani, na miti mikubwa.

Kwa mfano, kikundi cha kwanza, chenye mipera, guarana, na cupuaçu, hupandwa karibu-karibu. Miti hiyo haienei sana nayo huanza kuzaa matunda mapema. Kikundi cha pili, cha miti ya wastani kama vile biribá, miparachichi, na michikichi aina ya murumuru, yahitaji nafasi zaidi. Miti iliyo kwenye kikundi hiki huzaa matunda muda mrefu zaidi kuliko miti ya kikundi cha kwanza. Kikundi cha tatu, chenye miti mikubwa kama vile kokwa ya Brazili, piquia, na mikangazi, yahitaji nafasi kubwa hata zaidi. Baadhi ya miti katika kikundi hiki cha mwisho huzaa matunda, mingine hutokeza mbao zenye thamani, na mingine matunda na mbao. Vikundi vyote vitatu vya miti vinapokua pamoja, shamba hushabihi msitu wa kiasili.

[Picha]

Johannes van Leeuwen (kulia mwisho)

Soko lililoko Manaus lenye matunda yaliyokuzwa huko

[Hisani]

J. van Leeuwen, INPA, Manaus, Brazil

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

Jinsi Msitu Unavyoweza Kupandwa Upya

1. Februari 1993—Miti katika shamba hili katika msitu wa Amazon ya kati ilikatwa na kuchomwa mwezi wa Septemba 1992. Mwezi wa Januari 1993, nanasi zikapandwa. Mwezi mmoja baadaye, miti ya matunda ilipandwa pia.

2. Machi 1994—Nanasi zimekua, na miti ya matunda iliyopandwa sasa imeanza kurefuka. Vijiti vyenye vipande vya plastiki vyenye rangi vilivyo karibu na miti hiyo vyatambulisha miti hiyo kuwa mibiringanya, kokwa ya Brazili, na michikichi aina ya pichi, na kadhalika. Upaliliaji wa nanasi uliofanywa na wakulima ulinufaisha miti pia. Kana kwamba inaonyesha shukrani, miti hiyo imeanza kurutubisha udongo tena.

3. Aprili 1995—Mazao hayo yanayokua kasi yamevunwa na kuliwa au kuuzwa, na miti mbalimbali ya matunda yaendelea kukua.

[Hisani]

Picha 1-3: J. van Leeuwen, INPA-CPCA, Manaus, Brazil