Kemikali Zinapofanya Uwe Mgonjwa
Kemikali Zinapofanya Uwe Mgonjwa
MAMBO mengi yanayohusiana na hali ya kuathiriwa na kemikali mbalimbali (MCS) hutatanisha. Kuna maoni mengi ambayo hutofautiana miongoni mwa matabibu kuhusu kisababishi cha tatizo hilo. Baadhi ya madaktari waamini kwamba MCS ni tatizo la afya ya mwili, huku wengine waamini ni tatizo la akili, nao wengine wadhani ni tatizo la afya ya mwili pamoja na la akili. Baadhi ya madaktari wadokeza kwamba MCS huenda ni jamii ya magonjwa kadhaa. *
Wagonjwa wengi wenye MCS wasema kwamba tatizo lao lilitokea wakati ambapo, kwa kipindi kimoja tu, walikuwa katika mazingira yenye sumu nyingi kama vile dawa za kuua wadudu; wengine wasema kwamba kukaa katika mazingira yenye kiasi kidogo cha sumu kwa ukawaida au mara kwa mara kumesababisha hali yao. Baada ya kupata MCS, wenye tatizo hilo huathiriwa na kemikali mbalimbali ambazo hazikuwaathiri hapo kwanza, kama vile marashi au sabuni za maji za namna mbalimbali. Kwa hiyo, jina “kuathiriwa na kemikali mbalimbali” lafaa. Ebu fikiria kisa cha Joyce.
Joyce alipata chawa kichwani alipokuwa shuleni. Kichwa chake kikanyunyiziwa dawa ya kuua wadudu. Afya ya Joyce iliharibika, naye akaanza kuathiriwa na kemikali nyingi ambazo hazikuwa zimemwathiri hapo kwanza. Baadhi ya kemikali hizo ni sabuni za maji, viondoa-harufu
vya nyumbani, marashi, sabuni za nywele, na petroli. “Macho yangu huvimba hadi yafumbe,” asema Joyce, “nami napata mchochota wa uwazi wa mfupa wa fuvu unaosababisha kichefuchefu na maumivu ya kichwa ambayo ni makali sana hata nawa mgonjwa kwa siku kadhaa. . . . Nimeshikwa na nimonia mara nyingi hadi mapafu yangu yamekuwa na makovu mengi kama ya mtu ambaye amevuta sigara kwa miaka 40—nami sijawahi kuvuta sigara kamwe!”Kukaa kwa ukawaida katika mazingira yenye kiasi kidogo cha sumu, ama ndani ya nyumba ama nje, pia kumedhaniwa kusababisha MCS. Katika miaka ya karibuni visa vingi vya ugonjwa vilivyosababishwa na uchafuzi wa hewa ya nyumbani vimesababisha kutungwa kwa msemo “nyumba zisababishazo ugonjwa.”
Nyumba Zisababishazo Ugonjwa
Nyumba zisababishazo ugonjwa zilizuka katika miaka ya 1970 wakati nyumba, shule, na ofisi zenye visafisha hewa zisizoruhusu hewa kuingia au kutoka kwa njia ya kawaida, zilijengwa ili kuokoa nishati, nayo majengo hayo yalichukua nafasi ya majengo yaliyopitisha hewa kwa njia ya kawaida. Majengo hayo yalijengwa kwa mbao zilizopakwa dawa, gundi vukivu, na vikinza-baridi vya kioo-nyuzi na vinginevyo, nayo yalikuwa na mazulia na vitambaa vya sanisia.
Hasa, wakati vitu hivi ni vipya vinatoa kemikali zinazoweza kudhuru, mojawapo ya kemikali hizo ni formaldehyde. Mazulia huzidisha tatizo kwa kufyonza viyeyushi na sabuni za maji, kisha kwa muda mrefu kuzitoa polepole katika hewa. “Mivuke ya viyeyushi ni vichafuzi vya hewa vya nyumbani ambavyo ni vya kawaida zaidi,” chasema kitabu kiitwacho Chemical Exposures—Low Levels and High Stakes. “Viyeyushi ni aina za kemikali ambazo wagonjwa wengi hutaja kuwa kisababishi cha hali yao,” chasema kitabu hicho.
Huku wengi waweza kukaa katika majengo kama hayo bila kuathiriwa, watu kadhaa hupatwa na dalili za ugonjwa wa pumu na magonjwa mengine ya mfumo wa kupumua, au maumivu ya kichwa na uchovu. Kwa kawaida dalili hizo hutoweka wakati mtu mwenye matatizo hayo atokapo katika majengo hayo. Hata hivyo, “baadhi ya wagonjwa waweza kupatwa na hali ya kuathiriwa na kemikali mbalimbali,” yaani MCS, lasema jarida la kitiba la Uingereza liitwalo The Lancet. Lakini kwa nini kemikali zadhuru baadhi ya watu huku wengine haziwadhuru? Hilo ni swali muhimu kwa kuwa huenda baadhi ya wale ambao yaonekana haziwadhuru wakashindwa kuelewa tatizo la wale ambao zawadhuru.
Sisi Sote Twatofautiana
Inafaa kukumbuka kwamba twatofautiana na hatuathiriwi sawa na wengine na vitu mbalimbali, iwe ni kemikali, viini vya maradhi, au virusi. Jinsi tunavyoathiriwa yategemea maumbile yetu, umri, jinsia, afya, dawa tunazotumia, ugonjwa tulio nao tayari, na maisha yetu kama vile utumizi wa kileo, tumbaku, na dawa za kulevya.
Gazeti liitwalo New Scientist lasema kwamba “ikiwa dawa fulani [ya kitiba] itakusaidia kupona au la, na pia jinsi inavyokuathiri,” yategemea hali yako binafsi. Baadhi ya athari za dawa zaweza kuwa zenye hatari, hata zisababishe kifo. Kwa kawaida, protini ziitwazo vimeng’enya huondoa kemikali zisizotakikana mwilini, kama vile kemikali zilizomo katika dawa au vichafuzi viingiavyo mwilini katika shughuli za kila siku. Lakini *
ikiwa vimeng’enya hivyo vya “kusafisha” vina kasoro ya kinasaba, au vimeharibiwa kwa sababu mtu hajala chakula chenye lishe ifaayo, au vimeharibiwa na sumu, kemikali zisizotakikana zaweza kuongezeka mwilini, zifikie kiasi cha kudhuru.Ugonjwa wa MCS umelinganishwa na magonjwa ya damu yanayohusisha vimeng’enya mbalimbali yaitwayo porphyria. Mara nyingi watu wenye ugonjwa wa porphyria huathiriwa na kemikali katika vitu vingi tofauti-tofauti kama vile moshi wa magari au marashi, sawa na vile walio na MCS wanavyoathiriwa.
Hata Akili Inaathiriwa
Mgonjwa mmoja mwenye MCS alimwambia mwandishi wa Amkeni! kwamba kemikali fulani humduwaza. Alisema hivi: “Utu wangu hubadilika—ninakasirika, ninapatwa na wasiwasi au hofu, ninaudhika, au kusikia uchovu. . . . Naweza kuwa na dalili hizo kwa muda wa saa chache hadi siku kadhaa.” Baadaye, asikia uchovu kana kwamba alikuwa amelewa sana, na kushuka moyo.
Athari hizo ni za kawaida kwa watu wenye MCS. Dakt. Claudia Miller asema kwamba “nchi zaidi ya 12 zatoa habari kwamba watu waliokaa katika mazingira yenye kemikali, ama ya dawa za kuua wadudu ama katika nyumba isababishayo ugonjwa, wamepatwa na matatizo ya akili. . . . Twajua kwamba wanaofanya kazi katika mazingira yenye viyeyushi mbalimbali waweza kupatwa na hofu ya ghafula na kushuka moyo. . . . Kwa hiyo, twapaswa kuwa wenye kufikiria wengine na kukumbuka kwamba huenda ikawa ubongo ndio kiungo cha mwili kinachoathiriwa zaidi na kemikali.”
Ijapokuwa mazingira yenye kemikali yaweza kusababisha matatizo ya akili, kwa upande mwingine madaktari wengi waamini kwamba matatizo ya akili yaweza kusababisha hali ya kuathiriwa na kemikali. Dakt. Miller aliyetajwa juu na Dakt. Nicholas Ashford ambao huamini kabisa kwamba ugonjwa wa MCS husababishwa na hali zisizo za kiakili, wakubali kwamba “matukio yanayotuathiri kihisia na kiakili, kama vile kifo cha mwenzi wa ndoa au talaka, yaweza kuzuia mfumo wa kinga wa mwili wa watu fulani usifanye kazi kikamili. Matukio kama hayo huenda yakafanya baadhi ya watu waathiriwe zaidi na kiasi kidogo tu cha kemikali. Kwa hakika, uhusiano kati ya mifumo ya mwili na mifumo ya akili na ya hisia ni tata sana.” Dakt. Sherry Rogers aaminiye pia kwamba ugonjwa wa MCS wasababishwa na hali zisizo za kiakili, asema kwamba “mkazo wa akili hufanya mtu aathiriwe zaidi na kemikali.”
Je, kuna chochote ambacho wenye MCS waweza kufanya ili wawe na afya nzuri zaidi au angalau kupunguza matatizo yao?
Msaada kwa Watu Wenye MCS
Ijapokuwa ugonjwa wa MCS hauna dawa, wengi wamefaulu kupunguza matatizo yao, nao wengine wameweza kurudia maisha ya kawaida. Ni nini kilichowasaidia? Baadhi yao wasema kwamba wamefaidika kwa kufuata mapendekezo ya madaktari wao ya kuepuka kwa kadiri iwezekanavyo kemikali zinazofanya wawe wagonjwa. * Judy aliye na MCS ameona kwamba kuepuka kemikali kwamsaidia. Alipokuwa akipata nafuu baada ya kuugua ugonjwa uliosababishwa na virusi vya Epstein-Barr, nyumba ya Judy ilinyunyiziwa dawa ya kuua wadudu, naye alikaa sana katika mazingira yenye kemikali hiyo, hatimaye akapata ugonjwa wa MCS.
Judy anaathiriwa na kemikali nyingi za nyumbani kama vile wengi wenye MCS. Kwa hiyo, anatumia tu sabuni na magadi ya kuumulia anapofanya usafi. Yeye hutumia siki kulainisha nguo. Nguo zake zote, vitambaa na vitu vinginevyo vyote vya chumba chake cha kulala vimetengenezwa kwa nyuzi na vitambaa vya asilia.
Mume wake huweka nguo zake zilizofuliwa na dobi mahali penye hewa nyingi kwa majuma kadhaa kabla ya kuziweka katika kabati.Bila shaka, katika ulimwengu wa leo huenda wenye MCS wasiweze kuepuka kabisa kemikali zote zinazowaathiri. Kichapo American Family Physician chasema hivi: “Tatizo kubwa kwa mtu mwenye MCS ni upweke na kutoweza kushirikiana na wengine kwa sababu anajitahidi kuepuka mazingira yenye kemikali.” Makala hiyo yapendekeza kwamba hatua kwa hatua wagonjwa waanze kufanya kazi na kuwa pamoja na wengine, huku wakiangaliwa na daktari. Wakati uo huo wapaswa kujitahidi kujifunza jinsi ya kupumzisha akili, kustarehe, na kupumua ifaavyo ili waepuke kupatwa na hofu ya ghafula na kupigapiga kwa moyo. Lengo ni kusaidia wagonjwa wazoee mazingira yenye kemikali badala ya kuondoa kabisa kemikali zote katika mazingira yao.
Matibabu mengine mazuri ni kupata usingizi wa kutosha. David ambaye karibu amepona MCS, asema kuwa kulala katika chumba chenye hewa nyingi safi kumemsaidia kupona. Ernest na mke wake Lorraine, walio na ugonjwa wa
MCS wasema pia kwamba “kupata usingizi wa kutosha husaidia sana kuepuka athari zinazotokana na kukaa mchana wote katika mazingira yenye kemikali.”Sikuzote chakula chenye lishe bora ni chenye maana tunapojitahidi kudumisha afya njema au kupona ugonjwa wowote ule. Hilo limetangazwa kuwa “jambo muhimu sana kwa kudumisha afya njema.” Bila shaka ili mwili urudie afya nzuri, angalau kwa kiasi fulani, mifumo yote mwilini lazima ifanye kazi bila vizuizi. Huenda lishe ya ziada kama vile vitamini na kadhalika ikasaidia pia.
Mazoezi ya mwili pia huongeza afya njema. Nawe unapotoa jasho wasaidia mwili wako kuondosha sumu mwilini kupitia ngozi yako. Jambo muhimu pia ni kuwa na mtazamo unaofaa, ucheshi pamoja na kupendwa na kuwaonyesha wengine upendo. “Upendo na kicheko” ni dawa ambayo daktari mmoja huwapendekezea wagonjwa wote wenye MCS. Naam, “moyo uliochangamka ni dawa nzuri.”—Mithali 17:22.
Hata hivyo, kuwa na ushirikiano wenye upendo na furaha pamoja na wengine kwaweza kuwa tatizo kubwa sana kwa watu wenye ugonjwa wa MCS ambao huathiriwa na marashi, sabuni za maji, viondoa-harufu, na kemikali nyinginezo ambazo zimo katika mazingira yetu ya kila siku. Watu wenye MCS wafanyaje katika hali kama hizo? Nao wengine waweza kuwasaidiaje wale wenye MCS? Makala yanayofuata yatazungumzia mambo hayo.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Amkeni! si gazeti la kitiba, nayo makala haya kuhusu MCS hayakusudiwi kuendeleza mtazamo fulani wa kitiba. Makala haya yatoa tu habari juu ya matokeo ya uchunguzi wa karibuni, na pia juu ya kile ambacho baadhi ya madaktari na wagonjwa wameona kuwa chenye manufaa katika kutibu ugonjwa huo. Amkeni! latambua kwamba madaktari hawakubaliani kuhusu kile kinachosababisha MCS, wala juu ya matibabu au mipango ya matibabu iliyopo na inayotumiwa na wenye tatizo hilo.
^ fu. 12 Mojawapo ya vimeng’enya ambavyo watu wengi hukosa mwilini ni laktasi. Wanaokosa kimeng’enya hicho hawawezi kulishiza laktosi katika maziwa, nao huwa wagonjwa wanapokunywa maziwa. Watu wengine wana upungufu wa kimeng’enya kinachomeng’enya tyramine mwilini, kemikali inayopatikana katika jibini na katika vyakula vinginevyo. Wanapokula vyakula vya aina hiyo, wanapatwa na ugonjwa wa kipandauso.
^ fu. 20 Wale wanaofikiri wana ugonjwa wa MCS wapaswa kumwona daktari anayeaminika. Si jambo la hekima kufanya mabadiliko makubwa maishani mwako, ambayo huenda yakakugharimu fedha nyingi, kabla hujachunguzwa kikamili na daktari. Huenda uchunguzi ukaonyesha kwamba mabadiliko madogo tu katika maisha yako au kile unachokula yahitajika ili kupunguza, au hata kuondoa matatizo yako.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Je, Wahitaji Kemikali Nyingi Hivi?
Sisi sote twapaswa kupunguza utumizi wa kemikali ziwezazo kudhuru. Hilo latia ndani kemikali tulizo nazo nyumbani. Kitabu kiitwacho Chemical Exposures chasema hivi: “Vichafuzi vya hewa vya nyumbani vyaonekana kuwa visababishi vikuu vya hali ya kuathiriwa na kemikali. Michanganyo tata yenye kiasi kidogo cha mamia ya kemikali fukivu zenye kaboni inapatikana nyumbani.” *
Ujiulize ikiwa kwa kweli wahitaji kutumia kemikali nyingi hivi, hasa sumu za kuua wadudu au vitu vyenye viyeyushi fukivu. Je, umejaribu kutumia vitu visivyo na sumu? Hata hivyo, ikiwa ni lazima utumie kemikali inayoweza kudhuru, hakikisha kwamba u mwangalifu sana. Pia, hakikisha kwamba umeiweka kemikali hiyo, mahali salama ambapo watoto hawawezi kuichukua na mahali ambapo mivuke yake haitadhuru. Kumbuka kwamba hata kemikali katika vyombo vyenye vifuniko yaweza kufukiza.
Kujihadhari na kemikali kwatia ndani kufikiria kile ambacho twajipaka au kinachomwagika ngozini. Kemikali nyingi, kutia ndani marashi, zaingia katika damu kupitia ngozi. Kwa hiyo, kuna dawa za kitiba zinazowekwa juu ya ngozi tu, nazo huingia mwilini. Ukimwagikiwa na kemikali yenye sumu ngozini, “matibabu ya kwanza ni kuosha sehemu hiyo kabisa,” chasema kitabu kiitwacho Tired or Toxic?
Watu wengi wenye hali ya kuathiriwa na kemikali mbalimbali huathiriwa na marashi. Asilimia 95 ya kemikali zinazotumiwa katika marashi yote hutia ndani vitu vya sanisia ambavyo vimetokana na petroli. Asetoni, kafuri, benzaldehyde, ethanol, g-terpinene, na vitu vinginevyo vingi vya kemikali hutumiwa. Kwa mfano, nchini Marekani, Shirika la Kuhifadhi Mazingira limejulisha umma kwamba kemikali hizo zadhuru afya. Hali kadhalika kemikali zipatikanazo katika viondoa-harufu za hewa vilevile. Wanasayansi wa mazingira wachunguzapo viondoa-harufu za hewa “waviona kuwa vichafuzi wala si vitu vinavyoboresha hewa,” chasema kichapo University of California at Berkeley Wellness Letter. Viondoa-harufu za hewa haviondoi hewa mbaya bali vyaificha kwa harufu nzuri.
Kitabu kiitwacho Calculated Risks chasema kwamba “mojawapo ya dhana muhimu katika taaluma ya sumu ni kuwa kemikali zote hudhuru katika hali fulani.”
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 33 Njia mbalimbali za kuzuia sumu zisiingizwe nyumbani mwako zilizungumziwa katika toleo la Amkeni!, la Desemba 22, 1998.