Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Useja wa Kidini Sikubaliani na habari iliyo katika “Kuutazama Ulimwengu” yenye kichwa “Useja wa Kidini—Wa Nini?” (Septemba 22, 1999) Mnasema kwamba hoja ya Kanisa “haina msingi wa Maandiko.” Kupatana na Mathayo 19:10-12 na 1 Wakorintho 7:8, 26, 27, lazima nikate kauli kwamba kuna msingi wa useja wa kidini.
M. T., Marekani
Ni kweli kwamba Biblia hupendekeza useja kuwa mwendo wenye kupendeza kwa wengine. Hata hivyo, si takwa la Biblia kwamba wahudumu Wakristo wawe waseja wa kidini. Mtume Petro na wanaume wengine wenye madaraka katika kutaniko la mapema la Kikristo walikuwa wameoa. (1 Wakorintho 9:5; 1 Timotheo 3:2) Kwa hiyo, useja wa sharti hauna msingi wa Maandiko.—Mhariri.
Ushirikina Nikiwa mjuzi wa lugha, lazima niwaonyeshe kosa lililo katika gazeti Amkeni! la Oktoba 22, 1999. Katika mfululizo “Ushirikina—Kwa Nini Ni Hatari Sana?” mlitaja kwamba neno la Kijerumani gesundheit ni njia ya kusema “Mungu akubariki” mtu anapopiga chafya. Tafsiri ya Kiingereza ya neno hilo ni “afya.”
C. C., Marekani
Hatukumaanisha kwamba “gesundheit” ni tafsiri kamili ya usemi huo wa Kiingereza. Uliorodheshwa, pamoja na mitajo mingine miwili ya lugha za kigeni, kuwa “semi sawa” na matumizi ya mtajo wa Kiingereza “Mungu akubariki.”—Mhariri.
Cystic Fibrosis Nimetoka tu kumaliza kusoma makala “Kuishi na Maradhi ya Cystic Fibrosis.” (Oktoba 22, 1999) Niliguswa moyo sana na jinsi Jimmy Garatziotis anavyokabiliana na maradhi hayo mabaya sana. Pia uthamini wake kwa mke wake ulikuwa jambo lenye kutia moyo sana. Natambua jinsi ambavyo sisi huchukulia kijuujuu—hata uwezo wetu wa kupumua kwa kawaida!
D. A., Uingereza
Sina tatizo hilohilo lakini nina kasoro ya mapafu na ya tundu katika moyo. Nilifarijika kusoma simulizi hilo. Mimi pia nahisi kama Jimmy anaposema kwamba angependa kuwa na uwezo wa kukimbia viwanjani, tamaa ambayo twatumaini itatimizwa katika ulimwengu mpya unaokuja ulioahidiwa na Mungu.
F . A., Italia
Danube Ningependa kuwashukuru kwa makala bora kabisa “Mto Danube—Laiti Ungeweza Kuzungumza!” (Oktoba 22, 1999) Nilipokuwa msichana mdogo, niliishi karibu na chanzo cha Mto Danube nami nikaupenda sana. Nikiwa mtaalamu wa sayansi ya maji, mimi hupata fursa ya kuchunguza mito, nami nahisi kwamba mito hasa ni maumbile ya ajabu sana ya Mungu.
D. O., Kroatia
Mlisema kwamba Chuo Kikuu cha Vienna, kilichoanzishwa mwaka wa 1365, ndicho cha kale zaidi katika nchi zinazozungumza Kijerumani. Ikiwa mwamaanisha mahali ambapo Kijerumani chaongewa kwa sasa—Ujerumani, Austria, na sehemu ya Uswisi—habari hiyo ni sahihi. Lakini, chuo kikuu cha kale zaidi chenye kuongea Kijerumani kilifunguliwa mwaka wa 1348 huko Prague, jiji kuu la Jamhuri ya Cheki ya siku hizi. Wakati huo kilikuwa cha Austria.
M. E., Ujerumani
Kwa kweli, Prague lilikuwa jiji kuu la Bohemia. Ijapokuwa lugha zote mbili Kijerumani na Kicheki ziliongewa huko, lugha kuu ya chuo kikuu hicho ilikuwa Kilatini.—Mhariri.
Haya Asanteni sana kwa makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Nisiwe Mwenye Urafiki Zaidi?” (Oktoba 22, 1999) Hiki kimekuwa chakula kwa wakati unaofaa. Nimekuwa mwenye haya kwa maisha yangu yote. Nina umri wa miaka 17 nami naona ugumu kukutana na watu wapya na kushirikiana na wapya kwenye mikusanyiko ya Kikristo. Kwa sababu hiyo, nimekosa fursa nyingi za kuongeza na kufurahia ushirika na akina ndugu na dada. Makala yenu imenisaidia nitambue kwamba haya ni jambo la kawaida na kwamba ni jambo ninaloweza kushinda.
B. H., Marekani