Ukimwi Katika Afrika—Kuna Tumaini Gani kwa Milenia Mpya?
Ukimwi Katika Afrika—Kuna Tumaini Gani kwa Milenia Mpya?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ZAMBIA
SEPTEMBA uliopita wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za Afrika walikusanyika Lusaka, Zambia, kwa ajili ya Mkutano wa 11 wa Kimataifa Kuhusu UKIMWI na Maradhi Yanayoambukizwa Kingono katika Afrika. Kusudi moja la mkutano huo lilikuwa kuimarisha ushirikiano wa kimkoa katika kujibu swali, Twaweza kupambanaje na kuenea kwa UKIMWI katika Afrika?
Profesa Nkandu Luo, aliyekuwa waziri wa afya wa Zambia wakati huo, alisema kwamba hali katika Afrika na sehemu nyingine za nchi zinazositawi ni “mbaya kupindukia,” akaongezea kwamba “inazuia na kutangua maendeleo makubwa yaliyofanywa katika nyanja za afya, kijamii na kiuchumi.”
Mfululizo wa hotuba kuhusu usalama wa damu ulikiri kwamba UKIMWI umeambukizwa kupitia kutiwa damu mishipani. Daktari mmoja, mwakilishi wa Kitengo cha Usalama wa Damu cha Shirika la Afya Ulimwenguni, alisema kwamba ingawa kufanya ngono na mtu aliye na maradhi hayo hakuambukizi sikuzote, watu wanaopokea damu yenye UKIMWI wataambukizwa—katika kila kisa! Kwa hiyo akiwa na sababu nzuri, daktari huyo alisema kwamba katika kisa kama hicho “damu iliyo salama zaidi ni ile ambayo haijatiwa kwenye mishipa ya mtu mwingine.”
Mkutano huo ulikazia kwamba gharama kubwa sana ya matibabu hufanya iwe vigumu au isiwezekane kwa wale walio na UKIMWI kugharimia tiba hiyo. Kwa mfano, kwa wastani, raia wa Uganda anayeishi mjini hupata takriban dola 200 za Marekani kwa mwezi. Lakini tiba ya kufisha viini hivyo yaweza kugharimu dola 1,000 za Marekani kwa mwezi!
Mkutano wa Lusaka ulionyesha kwamba mwanzo wa milenia mpya hautaleta utatuzi wowote sahili kuhusu kuenea kwa UKIMWI. Hata hivyo, wanafunzi wa Biblia wanatambua kwamba mwishowe utatuzi wa magonjwa yote wamtegemea Muumba, Yehova Mungu, anayeahidi kwamba katika ulimwengu wake mpya, “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Profesa Nkandu Luo
[Hisani]
Photograph by permission of E. Mwanaleza, Times of Zambia