Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vasa—Kutoka Katika Msiba Hadi Kuwa Kivutio

Vasa—Kutoka Katika Msiba Hadi Kuwa Kivutio

Vasa—Kutoka Katika Msiba Hadi Kuwa Kivutio

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA SWEDEN

AGOSTI 10, 1628, ilikuwa siku nzuri ya kiangazi huko Stockholm, jiji kuu la Sweden. Umati wa watu ulisongamana kwenye magati ya bandarini wakati meli kubwa ya kifalme ya kivita, Vasa, iliyojengwa kwa miaka mitatu, ilipoanza safari yake ya kwanza ya kujiunga na jeshi la majini la Sweden.

Vasa haikuwa meli ya kivita ya kawaida. Mfalme Gustavus Adolphus Vasa wa Pili alitaka iwe meli yenye nguvu zaidi ulimwenguni. Baadhi ya watu husema kwamba aliamuru sitaha nyingine ya mizinga ijengwe aliposikia kwamba Wadenmark walikuwa wakijenga meli yenye sitaha mbili za mizinga. Alitaka meli iliyowakilisha jina la familia yake iwe bora zaidi ya meli zote.

Ilitarajiwa kwamba safari yake ya kwanza ingeonyesha watu nguvu na utukufu wake wa kifalme. Ilikuwa na mizinga 64 na ilipambwa kwa sanamu zaidi ya 700 na madoido. Gharama yake ilikuwa zaidi ya asilimia 5 ya jumla ya pato la kitaifa la Sweden. Huenda meli hiyo ya kivita yenye nguvu sana na umaridadi usio na kifani ikawa ndiyo meli bora zaidi iliyopata kujengwa wakati huo. Si ajabu kwamba kulikuwa na nderemo na vifijo vya kuisifu ilipoanza safari kutoka kwenye magati ya Stockholm!

Msiba na Aibu

Hata hivyo, baada tu ya Vasa kusafiri kwa kilometa moja hivi, upepo mkali ulizuka na kuifanya ipinduke ghafula. Maji yakaingia ndani kupitia madirisha ya mizinga yaliyokuwa wazi, ikazama. Labda ndiyo safari ya kwanza iliyokuwa fupi zaidi katika historia yote ya meli!

Watazamaji walifadhaika. Fahari ya Jeshi la Majini la Sweden ilizamishwa, si vitani wala katika dhoruba kali baharini, bali na upepo tu, katika bandari yao wenyewe. Watu walifadhaishwa hata zaidi na vifo vya abiria 50 hivi waliokuwamo. Badala ya kuwa chombo cha fahari ya taifa, Vasa ilitamausha na kuaibisha.

Kulikuwa na kikao cha korti ili kubaini aliyesababisha msiba huo wenye kuaibisha. Lakini hakuna mtu aliyeshtakiwa, huenda ni kwa sababu ushuhuda uliotolewa ulimhusu mfalme na Naibu-Mkuu wa kamanda wa jeshi la majini la Sweden, Klas Fleming.

Madai ya mfalme yaliwafanya wajenzi watumie mbinu za ujenzi wasizozoea. Hivyo, Vasa ikakosa usawaziko kabisa. Muda mfupi kabla ya kupinduka, Naibu-Mkuu Fleming, alikuwa amepanga kuchunguza uthabiti wake. Wanaume 30 walikimbia pamoja kutoka upande mmoja wa meli hadi mwingine. Baada ya kukimbia mara tatu mkuu huyo aligundua kwamba iwapo wangeendelea, meli ingepinduka papo hapo. Kwa hiyo, akakomesha uchunguzi huo bila kukomesha safari ya kwanza ya meli hiyo. Mashtaka yalifutwa baada ya watu mashuhuri kama vile mfalme na mkuu wa wanamaji kuhusishwa na msiba huo.

Katika mwaka wa 1664 hadi 1665, ofisa mstaafu wa jeshi la Sweden alipata nyingi za bunduki za Vasa zilizozama kwa kutumia chombo sahili cha mpiga-mbizi. Pole kwa pole Vasa ilisahauliwa ilipozidi kuzama kwenye matope yenye kina cha meta 30.

Yatolewa Matopeni

Mnamo Agosti 1956, mwakiolojia asiye stadi, Anders Franzén, alitumia kifaa cha pekee ili kuvuta kipande cha mwaloni kutoka chini ya bahari. Kwa miaka mingi amekuwa akichunguza hati za kale na kutafuta Vasa baharini. Sasa alikuwa ameipata. Kwa kutumia njia tata ya uokoaji, Vasa ilinyanyuliwa kutoka matopeni na kusafirishwa taratibu majini kisha ikapandishwa gudani.

Siku ya Aprili 24, 1961, magati ya Stockholm yalifurika tena watazamaji walipokuwa wakishangilia. Baada ya kukaa chini ya bahari kwa miaka 333, Vasa iliibuka tena—lakini ikiwa kitu cha thamani kwa waakiolojia wa baharini na cha kuwavutia watalii. Vyombo vya kale zaidi ya 25,000 vilifunua mambo yenye kuvutia kuhusu meli hiyo ya kivita ya karne ya 17 na habari za pekee kwa ujenzi wa meli za kisasa na sanaa ya uchongaji.

Kwa nini Vasa na vyombo hivyo vya kale vilihifadhiwa vyema? Baadhi ya sababu ni kwamba ilizama ingali mpya, matope yaliihifadhi, na minyoo wa baharini wanaoharibu mbao hawawezi kuishi katika maji yasiyo na chumvi ya kutosha.

Vasa ilibeba tani 120 za kokoto. Wataalamu hukadiria kwamba ilihitaji kubeba zaidi ya maradufu ya uzito huo ili iwe thabiti, lakini haikuwa na nafasi. Pia, uzito huo wa ziada ungeyazamisha madirisha ya chini ya mizinga. Ilikuwa maridadi ajabu, lakini ilikabili hatari kwa sababu ya kukosa usawaziko.

Sasa, ikiwa meli ya kale zaidi ulimwenguni iliyo kamili na iliyotambuliwa, imehifadhiwa katika jumba la pekee la maonyesho. Kila mwaka wageni wapatao 850,000 huja kuona meli hiyo ya kifalme na ya fahari ya karne ya 17, ambayo imedumu tangu msiba wa mwaka wa 1628. Hiyo hutukumbusha upumbavu wa watu wenye mamlaka ambao walipuuza kimakusudi mbinu bora za ujenzi wa meli kwa sababu ya kiburi na kutojali.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mfalme Gustavus Adolphus Vasa wa Pili

[Hisani]

Foto: Nationalmuseum, Stockholm

[Picha katika ukurasa wa 25]

Baada ya kukaa kwa zaidi ya miaka 300 chini ya bahari, sasa “Vasa” ni kivutio cha ulimwengu

[Hisani]

Genom tillmötesgående från Vasamuseet, Stockholm

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Målning av det kapsejsande Vasa, av konstnär Nils Stödberg