Mzambarausime Ua Lisilo la Kawaida Lenye Uzuri wa Kupendeza
Mzambarausime Ua Lisilo la Kawaida Lenye Uzuri wa Kupendeza
Karibu kila mtu huvutiwa na uzuri wa kupendeza wa mimea yenye maua, mfano wenye kutokeza ukiwa ni mzambarausime. Kwa sababu unapendwa sana, mzambarausime hukuzwa katika nchi kadhaa kwa madhumuni ya kibiashara, kutia ndani Israel na Uholanzi. Pia kuna mashamba ya mzambarausime huko Marekani ambayo hupeleka maua hayo kwa wapenzi wa kukuza maua ulimwenguni pote.
Jamii isiyo ya kawaida ya mzambarausime imeongezeka na kutia ndani namna mbalimbali 200, zenye kila namna ya rangi na umbile unaloweza kuwazia. Wakuzaji-maua wameweza kusitawishaje namna nyingi kupindukia za ua lilelile?
Kubuni Namna Mpya
Mkuzaji hutumia zana kama vile brashi ya singa za ngamia, kuondoa chavua kutoka kwenye stameni, sehemu ya kiume ya ua na kuihamisha hadi kwenye stigma, sehemu ya kike ya ua tofauti. Kwa kawaida chavua huwekwa kwenye maua ya chini zaidi yanayochanua, ya mmea utakaopokea chavua. Baada ya hilo, ua hufungwa ili kuzuia wachavushaji wa asili, kama vile nyuki au nzi, wasivuruge matokeo hayo. Ili kupata rangi au sura hususa, aina moja ya mzambarausime huzalishwa kwa kuchanganya mbegu yake na ya ua jingine lenye sura inayotakikana.
Hii haimaanishi kwamba namna mpya, au mahuluti, ni aina mpya ya ua. Uwezekano wa kutokeza namna hizo mbalimbali umekuwepo kwa muda wote, katika msimbo-jeni ulio tata wa mzambarausime. Kwa kuteua uzalishaji, waweza kupata mzambarausime wa rangi nyeupe hadi nyeusi-nyekundu au wa zambarau iliyokoza. Pia kuna mzambarausime wenye madoa, mikunjo na maua madogo maradufu. Mengine hata yana harufu nzuri kiasi.
Uzuri wa Kupendeza
Tazama kwa ukaribu maua yaliyo kwenye picha hii, na uone namna nyingi za mzambarausime. Lile linaloitwa Pulchritude linaloonekana hapa linavutia kama nini! Petali zake zinapochomoza, huwa nyororo, zinakuwa na mikunjo, kingo za rangi ya zambarau na ncha za zambarau iliyokoza. Petali zilizo sehemu ya chini, kuelekea kwenye kitundu cha kila ua dogo, zina rangi ya waridi iliyokoza na zambarau.
Namna nyingine inayoitwa Orchid Lace, ambayo pia yaonekana hapa, hutoa wazo la kwamba ni laini sana kiasi cha kwamba inaweza kuchubuka kwa kuguswa kidogo. Maua yake madogo huegemea shina, huku stameni ndefu zikichomoza kwenye sehemu ya kati ya kila kitundu chenye rangi ya kuvutia. Namna nyingine zina majina yanayoamsha hisia kama vile Dream’s End, Red Alert, Peerless na Silver Moon.
Kukuza Mizambarausime
Mbali na kupata mbegu kutoka kwenye maua, wakulima wa mzambarausime huvuna shinagimbi, sehemu ya chini ya shina la ua yenye umbo la kitunguu. Pia hukusanya shinagimbi ndogo, ambazo hukua kwenye shinagimbi kuu.
Mizambarausime iliyokuzwa imesitawishwa hasa kutokana na aina za Kiafrika. Hivyo, ilianzia sehemu za kitropiki, na huathiriwa kwa urahisi sana na tabia ya nchi. Huenda isisitawi katika nchi fulani zenye majira ya baridi kali, lakini hunawiri katika miezi ya kiangazi.
Katika sehemu zenye tabia ya nchi iliyo na baridi
kali zaidi shinagimbi lapaswa kuchimbwa mwishoni mwa majira ya kupanda na kusafishwa kwa uangalifu. Shinagimbi jipya litakuwa limefanyizwa, na shinagimbi zee lililokuwa kwenye sehemu ya chini ya shina linapotolewa, inakuwa rahisi zaidi kwa shinagimbi jipya kupenyeza mizizi. Kwa kuongezea, kichomozo chenye ukubwa wa dengu ambacho huzunguka kila shinagimbi lazima kiondolewe. Wakati wa majira ya baridi kichomozo na shinagimbi vyapasa kuwekwa mahali pakavu, penye baridi palipo na halijoto isiyoweza kugandisha vitu.Kile kichomozo kinapopandwa hutokeza majani membamba, na mwishoni mwa majira ya kupanda, kichomozo kitakuwa shinagimbi lililokomaa. Shinagimbi linapopandwa msimu unaofuata, litakua na kuwa mimea iliyokomaa yenye maua mengi.
Katika nchi zenye tabia ya nchi ya kadiri, kupanda kwaweza kuanza mwanzoni mwa masika. Hakuwi na tatizo kubwa kuhusu wakati wa kupanda katika nchi zenye tabia ya nchi iliyo na joto zaidi. Ili kupata matokeo bora, kichomozo na shinagimbi vyapasa kupandwa kwenye udongo wenye unyevunyevu, na asidi ya kiasi. Yapasa kuwa mahali ambapo litapata nuru angavu ya jua, kwa kuwa mizambarausime hainawiri kivulini.
Huenda shinagimbi dogo likapandwa mbalimbali kwenye tuta la sentimeta nane na kisha kufukiwa udongo. Kwa upande mwingine, shinagimbi lapasa kupandwa kwenye kina cha sentimeta 13. Ili kuzuia msongamano kwenye bustani ya nyumbani, shinagimbi la ukubwa wa kadiri lapasa kupandwa likiwa limeachana kwa sentimeta 12 na kichomozo kikiwa kimeachana kwa sentimeta 8 hadi 10. Ukisafisha na kupanda shinagimbi lako la mzambarausime kwa uangalifu, baada ya miezi michache, utathawabishwa na uzuri usioweza kufafanuliwa—uzuri wa rangi nyingi za kupendeza za mzambarausime.
[Picha katika ukurasa wa 16]
“Orchid Lace”
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
“Coral Dream”
“Monet”
“Dream’s End”
“Sunsport”
[Picha katika ukurasa wa 17]
“Pulchritude”