Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Pengo Kati ya Matajiri na Maskini Laongezeka

Pengo Kati ya Matajiri na Maskini Laongezeka

Pengo Kati ya Matajiri na Maskini Laongezeka

“Katika muda wa miaka mitano iliyopita, maendeleo mengi yamefanywa ili kupunguza umaskini tufeni pote kuliko yaliyofanywa katika karne tano zilizopita,” chasema kichapo UNDP Today, kinachochapishwa na Programu ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Maendeleo. “Katika nchi zinazoendelea vifo vya watoto vimepungua kwa asilimia 50 tangu 1960, utapiamlo umepungua kwa thuluthi moja na idadi ya watoto wanaoenda shule imeongezeka kwa robo moja.” Lakini chanzo hichohicho chakiri kwamba licha ya maendeleo hayo, umaskini wa tufeni pote “ungali umeenea sana.”

Mbaya hata zaidi, ni ukosefu wa haki katika jamii na kati ya jamii mbalimbali unaoendelea kukua. “Kwa kulinganisha na mwaka mmoja uliopita,” asema Catherine Bertini, mkurugenzi mkuu wa Programu ya Chakula Ulimwenguni ya UM, “watu wengi zaidi ulimwenguni wanateseka kutokana na utapiamlo na njaa.” Kwa hakika, leo watu wapatao milioni 840 katika nchi zinazoendelea huishi kwa njaa daima, watu wanaozidi bilioni moja hawawezi kupata maji ya kunywa yaliyo salama, na karibu watu bilioni 1.5 huendeleza maisha kwa pesa zinazopungua dola moja kwa siku. Mary Robinson, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa UM, aonya kwamba “tuko katika hatari ya kufikia wakati ambapo ulimwengu utagawanyika si kuwa mataifa yanayoendelea na yaliyoendelea, bali kuwa mataifa yaliyoendelea kupita kiasi na mataifa ambayo hayataendelea kamwe.”

Ingegharimu nini kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini katika jumuiya ya ulimwenguni ya leo yenye watu bilioni sita? Kiasi kidogo kuliko vile ungefikiri. UM unapiga hesabu kwamba dola bilioni 9 (dola 1.5 kwa mtu mmoja) za ziada zingehitajiwa kwa mwaka ili kuandaa usafi wa kutunza afya na maji safi ulimwenguni pote na kwamba dola za ziada bilioni 13 (karibu dola 2.00 kwa mtu mmoja) kwa mwaka zingehitajika kuhakikisha kwamba kila mtu duniani anapata utunzaji wa afya wa msingi na lishe. Hata ingawa hiki ni kiasi kikubwa kwa kulinganisha, kikilinganishwa na pesa zinazotumika ulimwenguni kwa mambo mengine ni kiasi kidogo sana. Kwa kielelezo, katika mwaka mmoja wa karibuni, ulimwengu ulitumia dola bilioni 435 (zaidi ya dola 70 kwa mtu mmoja) katika utangazaji na dola 780 (dola 130 kwa mtu mmoja) kwa mambo ya kijeshi. Kwa wazi, kupunguza pengo kati ya walio navyo na wasio navyo katika ulimwengu si kutafuta fedha za kutosha bali ni kutanguliza mambo ya maana.