Ngazi Inayoelekea Angani
Ngazi Inayoelekea Angani
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA FILIPINO
UREFU wake wasemekana kuwa mara kumi zaidi ya urefu wa Ukuta Mkubwa wa China. Watu fulani husema kwamba ikiwa sehemu zake zingeunganishwa, ingefika umbali wa kilometa 20,000—au nusu ya dunia! Wengine hata huiita ajabu ya nane ya ulimwengu. Hata hivyo, watu wengi hawajapata kusikia juu ya mandhari hii yenye kutisha huko Filipino. Ni nini? Ni ngazi inayoelekea angani, matuta ya mpunga katika Safu ya Milima ya Kati. Matuta hayo yaliyochimbwa katika milima ya Luzon, ni mandhari yenye uzuri na ubunifu wa kustaajabisha.
Mbona yalijengwa? Safu ya Milima ya Kati yenye mvua nyingi ina miinuko mikubwa sana hivi kwamba kwa kawaida haitumiwi kwa kilimo. Mwinamo wa miteremko fulani huzidi asilimia 50. Lakini wakulima wa kale hawakuzuiwa na jambo hilo. Walichimba maelfu ya matuta kwenye pembe za milima hiyo yenye rutuba katika kimo cha meta 1,200 au zaidi. Nyakati nyingine matuta 25, 30, au zaidi hupangwa kama ngazi inayoelekea angani. Na kila tuta ni shamba lililofurika maji, lenye maboma ya ardhi na lenye kuimarishwa kwa kuta za mawe. Matuta mengi yamepandwa mpunga nayo hufuata kontua za milima; miteremko fulani imebonyea, mingine imebinuka.
Bila shaka, matuta ya kilimo hayapatikani tu Filipino. Mashamba yenye matuta hupatikana katika nchi nyingine pia, hasa katika Kusini-Mashariki ya Asia, Amerika Kusini, na sehemu nyingine za Afrika. Lakini matuta ya mpunga ya Filipino ni ya pekee katika njia nyingi. Mario Movillon, wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga, aliliambia Amkeni!: “Matuta ya mpunga ya Filipino ni makubwa zaidi ya matuta katika nchi nyinginezo. Huenea sehemu kubwa ya Safu ya Milima ya Kati.” Sehemu kubwa iko katika Jimbo la Ifugao. Mtu huvutiwa sana na idadi kubwa mno ya matuta. Huongezea uzuri wa mandhari ya asili ya milima hiyo.
Je, Ni Ajabu ya Ulimwengu
Je, ni kutilia chumvi kuyaita ajabu ya nane ya ulimwengu? Hebu fikiria jambo hili hakika: Huenda yawe mradi pekee wa kilimo ulio mkubwa zaidi katika historia yote ya wanadamu. Mnamo Desemba mwaka wa 1995, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni liliamua kutia ndani matuta ya mpunga ya Ifugao katika Orodha ya Mirathi ya Ulimwengu. Kama tokeo, sasa matuta hayo yanalinganishwa na mahali pengine pa kihistoria na kitamaduni, kama vile Taj Mahal huko India, Visiwa vya Galapagos huko Ekuado, Ukuta Mkubwa wa China, na Angkor Wat ya Kambodia. Lakini tofauti na miradi mingine ya kale, kama vile piramidi za Misri, ni wazi kwamba matuta hayo yalijengwa kwa ushirikiano wa jumuiya—si kazi ya watumwa. Pia, hayajaachiliwa tu bali yangali yanalimwa sana na Waifugao.
Unapozuru matuta hayo, unaweza kuvutiwa sana na uzuri wake wa kustaajabisha. Utawaona watu wakifanya kazi kwenye matuta, yenye ukubwa wa meta chache hadi meta 10,000 za mraba. Baadhi ya wafanyakazi wanadukua mashimo kwa vijiti ili kuwezesha udongo ufyonze maji, huku wakiimba. Wengine wanapanda mpunga, wanahamisha miche, au wanavuna mazao yao. Unapozuru wakati mpunga unapochipuka, matuta hayo hufanyiza picha maridadi ya rangi mbalimbali za kijani-kibichi.
Aina fulani ya mpunga huhitaji maji mengi sana ili ukue. Kwa hiyo, kuna mfumo tata wa kumwagilia mashamba maji. Maji ya vijito vya milimani hukusanywa, kisha husambazwa kwenye matuta kwa mfumo tata wa mifereji na mabomba ya mwanzi. Maji hayo yanayoelekezwa na nguvu za uvutano, husambaza maji kutoka kwa tuta moja hadi jingine kwa ukawaida. Kwa kweli matuta
hayo ni ajabu halisi wala si nguzo ya kale ya ukumbusho!Ni Nani Walioyajenga?
Bila shaka, maelfu haya ya matuta hayakujengwa kwa siku moja, au hata kwa miaka michache. Kumbuka, ujenzi huu ulifanywa pasipo vifaa vyovyote vya kisasa au mashine. Kwa hiyo, yaaminika kwamba ujenzi wa matuta ulianza angalau maelfu kadhaa ya miaka iliyopita.
Waakiolojia fulani hata wanaamini kwamba ujenzi ulianza miaka 2,000 iliyopita. Wanaanthropolojia wanadokeza kwamba wajenzi walitoka kaskazini mwa Indochina au kutoka Indonesia na wakahamia Luzon, wakianzisha kilimo cha mpunga kwenye matuta yaliyofurika. Baada ya matuta hayo kujengwa, matuta mapya yaliongezwa hatua kwa hatua.
Jinsi Unavyoweza Kuyafurahia
Acheni tusafiri kimawazo kwenye matuta hayo. Kwanza twapanda basi lililoyoyozwa kutoka Manila hadi kwenye mji wa Banaue, Ifugao. Twasafiri kwa muda wa saa tisa hivi. Sasa twahitaji kufanya uchaguzi fulani. Huenda tukaamua kwenda kwa miguu, kwa baiskeli ya magurudumu matatu, au kwa basi aina ya jeep tuzurupo sehemu zenye kuvutia. Na tukiwa na nia na nguvu, huenda tukafuata mojawapo ya vijia vya miguu vielekeavyo mlimani. Huwa mandhari nzuri ajabu ya matuta nayo humsaidia mtu kuona ukubwa wa ajabu hiyo iliyofanyizwa na mwanadamu.
Twaamua kusafiri kwa basi aina ya jeep hadi kijiji cha Batad. Twasafiri umbali wa kilometa 12 kwa zaidi ya muda wa saa moja kwenye barabara zenye mashimo-mashimo za mlimani. Kuanzia hapo na kuendelea twapanda kupitia kijia cha miguu. Twapenya vichaka vya mlimani vya aina mbalimbali na hatimaye twafika kwenye mgongo wa sehemu mbili zilizoinuka. (Kuna njia ya mkato, lakini imeinuka sana na haipendekezwi kwa wale wasiozoea upandaji mgumu sana.) Kutoka kwenye mgongo huo twapanda taratibu hadi Batad kwa kijia chembamba.
Baada ya kutembea kwa muda wa saa kadhaa, huku tukifurahia hewa safi ya mlimani, hatimaye twafikia kikomo cha safari yetu. Matuta yavutia sana kutoka hapa. Kwa kuwa Batad uko kwenye mteremko uliobonyea wa mlima, matuta yana umbo la uwanja-duara mkubwa wa maonyesho. Yanafanyiza mpangilio wa mistari wenye kupendeza, mmoja juu ya mwingine, kama ngazi inayoelekea angani. Tukaribiapo kijiji, twaona nyumba za Ifugao zenye muundo wa kale, zimesambaa kijijini kama viyoga vikubwa vilivyofunikwa kwa nyasi.
Watu ni wenye urafiki nao watuamkua tunapowapita wakifanya kazi kwenye matuta. Huenda ukashangaa kuona wenyeji wakitembea kwa wepesi kutoka sehemu moja hadi nyingine, kwenye pembe ya ukuta wa mawe wa matuta. Baadhi yao hupanda tuta moja baada ya jingine kwa uangalifu sana kama mbuzi wa milimani, huku wakitumia miamba iliyowekwa pafaapo kama vidato vya kupandia. Unapowakaribia utaona kwamba wako miguu mitupu. Wanazingirwa pande zote na mandhari yenye kuvutia sana ya matuta ya mlimani—ni nadra sana kuona kazi ya mwanadamu ikifaana na kukamilisha mazingira.
Je, lasikika kuwa jambo la kupendeza? Hivyo basi, hakikisha kwamba unapozuru Filipino hukosi kuona ngazi inayoelekea angani, ni ajabu halisi usiyoweza kusahau upesi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
Kuhifadhi Matuta
Licha ya uzuri wa sasa wa matuta hayo, yako katika hatari ya kutoweka. Wakazi wapya wa milimani hawapendi kuwa wakulima wa mpunga nao wanatafuta kazi ya kuajiriwa penginepo. Hilo laweza kutokeza upungufu wa wakulima stadi wanaoweza kudumisha matuta hayo.
Aurora Ammayao, mwenyeji wa Ifugao aliye mwanachama wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga, aliliambia Amkeni! hatari nyingine: “Matuta yapaswa kuwa na maji sikuzote, lakini sasa kuna upungufu wa maji kwa sababu ya ufyekaji wa misitu.” Kukausha eneo linalohifadhi maji kutaharibu matuta hayo.
Mara kwa mara misiba ya asili husababisha hasara pia. Mnamo mwaka wa 1990 tetemeko la ardhi liliharibu sehemu kadhaa za matuta hayo wakati pande nzima-nzima za milima zilipoporomoka.
Hata hivyo, hatua zinachukuliwa ili kukomesha uharibifu wa matuta hayo. Amri ya serikali ya kufanyiza Tume ya Kuchunguza Matuta ya Ifugao ilitangazwa mnamo mwaka wa 1996. Itafanya kazi gani? Kudumisha matuta, pamoja na mfumo wake wa maji na utamaduni wa eneo hilo, vilevile kukarabati maeneo yoyote yaliyoharibika.
Kuorodheshwa kwa matuta hayo katika Orodha ya Mirathi ya Ulimwengu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kunaiwajibisha zaidi serikali ya Filipino ihifadhi eneo hilo. Na kwa mujibu wa Jean Tuason, naibu mkurugenzi mkuu katika ofisi ya UNESCO huko Manila, “huenda UNESCO ikaandaa pia msaada wa kiufundi na wa kifedha kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi matuta hayo ya mpunga.”
[Ramani katika ukurasa wa 16]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Safu ya Milima ya Kati
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 17]