Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Hatari za Kunenepa Kupita Kiasi
Ugonjwa wa kisukari, maradhi ya moyo, na maradhi mengine yanatarajiwa kuongezeka sana kwa sababu ya “tatizo linaloenea Ulaya la kunenepa kupita kiasi,” laripoti The Independent la London. Mwenyekiti wa kikundi cha International Obesity Task Force alisema hivi alipohutubia wataalamu wa tiba kutoka nchi 26 waliokutanika Milan, Italia: “Hili ni tatizo la tufeni pote na sharti hatua ya haraka ichukuliwe sasa ili kuuzuia ugonjwa huu mbaya usiojulikana unaoenea na kuongeza gharama za kitiba. Tunakabili msiba wa kiafya tusipochukua hatua.” Nchi zote za Ulaya zinahusika, na katika maeneo mengine kati ya asilimia 40 na 50 ya idadi ya watu wameathiriwa. Tangu 1980, idadi ya wanawake wanene kupita kiasi huko Uingereza imeongezeka kutoka asilimia 8 hadi 20 na wanaume kutoka asilimia 6 hadi 17. Sababu zilizotajwa zatia ndani mtindo-maisha wa uzembe na milo yenye mafuta mengi—zinazohusiana na kupata ufanisi zaidi. Jambo linalohangaisha zaidi ni idadi ya watoto walio wazito kupita kiasi. Kulingana na Profesa Jaap Seidell, msimamizi wa Shirika la Ulaya la Kuchunguza Unene wa Kupita Kiasi, “ishara zaonyesha kwamba watu wengi wa kizazi kijacho wananenepa na kuwa wazito kupita kiasi wanapokuwa wangali wachanga.”
Hasara ya Uchumi wa Tufeni Pote
Uchumi wa tufeni pote unatokeza soko la dunia linaloandaa fursa bora kwa wengi, lakini pia unaongeza hatari, laripoti gazeti la The Guardian la Uingereza. Uhusiano wa mataifa katika uchumi unaoibuka wa ulimwengu hufanya tukio moja tu—kama lile la kupoteza thamani kwa baht ya Thailand mnamo 1997—lizushe hofu kubwa ya kiuchumi ulimwengu pote. “Miaka 30 iliyopita,” lasema The Guardian, “uwiano kati ya moja kwa tano ya watu matajiri zaidi ulimwenguni na moja kwa tano ya watu maskini zaidi ulikuwa 30 kwa 1. Kufikia mwaka wa 1990 uwiano huo uliongezeka na kuwa 60 kwa 1 na leo ni 74 kwa 1. . . . Miongoni mwa watu wanaonufaika zaidi na biashara ya tufeni pote ni wahalifu, ambao sasa wanaweza kuendeleza biashara ya dawa za kulevya, silaha na ukahaba katika masoko ya dunia.”
Je, Waweza Kuepuka Mafua?
Huenda usiweze kuepuka kabisa mafua, lakini waweza kuzingatia tahadhari fulani, lasema gazeti la The New York Times. Zifuatazo ni baadhi ya tahadhari muhimu zaidi: Epuka umati iwezekanapo, jaribu sana kuepuka kuwasalimu kwa mkono watu wenye mafua. Kwa kuongezea, epuka kusugua macho na pua yako, nawa mikono mara nyingi. Tahadhari hizo husaidia kwa kuwa mikono hutia virusi vya mafua machoni na katika utando wa pua unaoathiriwa kwa urahisi. Virusi vya mafua vilivyo juu ya kitu au mikononi vyaweza kudumu kwa muda wa saa kadhaa, na mtu aliye na mafua anaweza kuambukiza wengine kwa muda kabla na baada ya kuona dalili za ugonjwa. Tahadhari nyingine zatia ndani kula mlo kamili na kuwa mwangalifu hasa unapokuwa kati ya watoto. Kwa nini? Kwa kuwa wao huambukizwa mafua mara tano hadi nane kwa mwaka!
Afya ya Akili Katika Afrika
“Takriban watu milioni 100, kati ya wakazi milioni 600 wa Afrika wanaoishi kusini ya Sahara, wana matatizo ya kiakili,” laripoti gazeti la The Star la Afrika Kusini. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, vita na umaskini ndivyo visababishi vya idadi hiyo kubwa. Sababu nyingine ni kupungua kwa utegemezo wa jamaa. Profesa Michael Olatawura, wa Nigeria, alisema, “desturi hii ya Afrika inayotoa utegemezo” inaharibiwa na maadili ya Magharibi, matumizi mabaya ya dawa za kulevya, na jeuri ya kijamii. Kwa kuongezea, washiriki wa familia wanasafiri ng’ambo ili kutafuta kazi ya kuajiriwa. “Matatizo ya kiuchumi ya serikali za Afrika yametatanisha uwezo wetu wa kutunza afya ipasavyo,” asema Profesa Olatawura.
Mikeka Yenye Picha za Vita
Mambo yenye kuchukiza ya vita yanaonyeshwa na usanii wa pekee huko Afghanistan, laripoti gazeti The News la Mexico City. Kwa muda wa miaka 20 iliyopita, wasanii Waafghan wamefuma picha za zana za kivita kwenye mikeka yao mashuhuri. Pamoja na picha za kawaida za ndege, misikiti, na maua pia kuna picha za bunduki mimina-risasi, gruneti, na vifaru. Mtaalamu wa ufumaji-mikeka
Barry O’ Connell asema kwamba ijapokuwa picha hizo haziwi wazi sikuzote, picha nyingi “ni sahihi sana” hivi kwamba mara nyingi inakuwa rahisi “kutofautisha bunduki aina ya AK-47 na AK-74.” Inasemekana kwamba wengi wa wafuma-mikeka hao ni wanawake waliohasiriwa na vita. Kwao, kufuma mikeka hiyo ya pekee ni njia ya werevu ya kudhihirisha hisia zao.Mvua Iliyochafuliwa
Baadhi ya maji ya mvua huko Ulaya hayafai kunywewa kwa sababu ya kiasi kikubwa cha viuadudu vilivyomo, laripoti gazeti la New Scientist. Huko Uswisi wanakemia wamegundua kwamba sampuli za maji ya mvua yanayotekwa dakika chache za kwanza za dhoruba mara nyingi huwa na kiasi kikubwa sana cha viuadudu kinachopita kile kinachokubaliwa ama na Muungano wa Ulaya ama na Uswisi. Uchafuzi huo husababishwa na viuadudu, na kiasi kikubwa zaidi cha kemikali hizo zenye sumu hutukia mvua kubwa inaponyesha baada ya ukame wa muda mrefu. Wakati uleule, watafiti Wasweden wameonyesha kwamba matumizi yaliyoenea ya viuadudu kadhaa ndiyo yanayosababisha ongezeko kubwa la kansa ya non-Hodgkin’s lymphoma. Kemikali zinazozuia kuota kwa mimea kwenye paa zaweza pia kuchafua maji ya mvua yanayotiririka kutoka kwenye majengo.
Vifo Vinavyohusiana na Ukulima
Zaidi ya mtu mmoja hufa kila juma kwenye mashamba ya Uingereza, hali inayofanya ukulima uwe mojawapo ya kazi hatari zaidi nchini, laripoti The Times la London. Mnamo mwaka wa 1998 mhasiriwa mchanga zaidi, mwenye umri wa miaka minne tu, alipondwa na magurudumu ya trekta, na watu wengine saba wakafa trekta zilipopinduka kwenye miteremko. Wakulima wanaonywa wafikiri sana kabla ya kutekeleza kazi hatari na kuchunguza hali kabla ya kuendesha trekta kwenye miteremko. David Mattey, mkaguzi mkuu wa kilimo wa Halmashauri Kuu ya Afya na Usalama, alisema: “Misiba mingi ingeepukwa kama watu wangetua kidogo, na kufikiria mambo yanayohusika na kutekeleza kazi hiyo kwa njia tofauti kidogo.”
Vyanzo vya Umeme Visivyo vya Kawaida
▪ Kisiwa cha Ouvéa, New Caledonia, hakina petroli, lakini kinazalisha umeme kwa mafuta ya nazi, laripoti gazeti la Sciences et avenir la Kifaransa. Mhandisi Mfaransa Alain Liennard alitumia muda wa miaka 18 akibuni injini inayotumia mafuta ya nazi. Injini hiyo huendesha jenereta, inayotoa umeme kwa kiwanda cha kuondoa chumvi kwenye maji na kusambaza maji safi kwa familia 235 za kisiwa hicho. Liennard asema kwamba mfumo huo wake wenye kilowati 165 unatoa umeme na kutumia fueli sawa na injini za dizeli.
▪ Wakati huohuo, fahali walitumiwa kuzalisha umeme katika jaribio lililofanywa kwenye kijiji cha Kalali katika Jimbo la Gujarat, India. Gazeti Down to Earth, la New Delhi, laripoti kwamba mwanasayansi mmoja na mpwaye wa kike walibuni njia ya kuzalisha umeme. Fahali wanne huzungusha mtaimbo uliounganishwa kwa giaboksi inayoendesha jenereta ndogo. Jenereta hiyo imeunganishwa na betri, zinazoendesha kisagio cha nafaka na bomba la kuvutia maji. Gharama ya kizio cha umeme huo ni karibu senti 10, ikilinganishwa na dola 1 kwa kila kizio cha umeme wa kinu-upepo au dola 24 kwa kila kizio cha umeme wa paneli za jua, chasema kichapo Down to Earth. Hata hivyo, kwa kuwa wanakijiji wanahitaji kulima mashamba yao miezi mitatu kwa mwaka kwa kutumia fahali hao, wabuni wanatafuta njia bora ya kuhifadhi umeme utakaotumiwa wakati fahali hawapo.
Ulaji wa Busara
Kwa wastani, wasichana hurefuka kwa sentimeta 25 na huongeza uzito wa kilogramu 18 hadi 22 wanapokuwa na umri wa miaka 10 hadi 14, ilhali wavulana hurefuka kwa sentimeta 30 na kuongeza uzito wa kilogramu 22 hadi 27 wanapokuwa na umri wa miaka 12 hadi 16. Wakati huo wa ukuzi wa haraka, ni jambo la kawaida kwa vijana kuhangaikia uzito wao na kujaribu kuupunguza. “Lakini kufuata utaratibu maalum wa kula na kujizuia kula ni mambo yasiyofaa kwa afya na hayapendekezwi,” aandika Lynn Roblin katika gazeti la The Toronto Star. Hatua hizo zaweza kuunyima mwili virutubishi, asema Robin. Pia, kufuata utaratibu maalum wa mlo “husababisha mazoea ya ulaji yaliyo hatari kwa afya na kwaweza kuleta matatizo makubwa sana ya ulaji.” Matineja, yeye asema, wanahitaji kuwa na maoni yanayofaa kuhusu umbo lao na kuwa na uzito unaofaa kwa “kula kwa busara, kutokuwa wazembe na kuridhika na umbo lao.”