Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ubaguzi​—Je, Umekuathiri?

Ubaguzi​—Je, Umekuathiri?

Ubaguzi ni kama ugonjwa wa kuambukiza. Unaweza kumwathiri mtu bila hata yeye mwenyewe kutambua.

Watu wanaweza kuwabagua wengine kwa sababu ya taifa, rangi, kabila, lugha, tofauti za kidini, jinsia, au hali ya kiuchumi. Baadhi ya watu huwabagua wengine kwa sababu ya umri, elimu, ulemavu, au mwonekano wao. Huenda mtu akawabagua wengine kwa sababu ya mambo hayo, lakini bado asihisi kwamba ana ubaguzi.

Je, wewe umeathiriwa na ubaguzi? Ni rahisi kuona wengine wana ubaguzi. Lakini inaweza kuwa vigumu sana kutambua kwamba sisi wenyewe tuna ubaguzi. Ukweli ni kwamba, kila mmoja wetu ameathiriwa na ubaguzi kwa kiwango fulani. David Williams, profesa wa masuala ya jamii alisema kwamba watu wanapokuwa na maoni yasiyofaa kuhusu watu fulani, na kisha wakutane na mtu kutoka kwenye jamii hiyo, “mara nyingi watamtendea kwa njia tofauti na watafanya hivyo bila wao wenyewe kutambua.”

Kwa mfano, katika mojawapo ya nchi za kusini-mashariki mwa Ulaya ambako Jovica anaishi, kuna jamii fulani yenye watu wachache ambayo hubaguliwa. Jovica anasema: “Nilifikiri watu wote katika jamii hiyo ni wabaya. Lakini sikufikiri kwamba nilikuwa na ubaguzi. Isitoshe nilikuwa nikijifariji kwa kudai kwamba huo ni ukweli.”

Serikali nyingi zimetunga sheria za kupambana na ubaguzi wa rangi na aina nyingine za ubaguzi. Hata hivyo, bado ubaguzi unaendelea. Kwa nini? Kwa sababu sheria zinazowekwa zinalenga tu matendo ya watu lakini haziwezi kudhibiti mawazo na hisia za watu. Ubaguzi unaanzia kwenye akili na moyo wa mtu. Je, inawezekana kuushinda na kuukomesha kabisa ubaguzi?

Makala zinazofuata zitazungumzia kanuni tano ambazo zimewasaidia watu wengi kushinda mawazo na hisia za ubaguzi.