Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Malengo ni kama ramani; ukijitahidi, utayafanya kuwa kitu halisi

KWA VIJANA

12: Malengo

12: Malengo

MAANA YAKE

Kujiwekea lengo ni zaidi ya kuwa tu na ndoto—jambo unalotamani litokee. Malengo halisi yanahusisha kupanga mambo, kunyumbulika, na kutia bidii ili kuyafikia.

Malengo yanaweza kuwa ya muda mfupi (yanayofikiwa ndani ya siku au wiki kadhaa), ya kati (miezi), na ya muda mrefu (mwaka au zaidi). Malengo ya muda mrefu yanaweza kufikiwa kwa kutimiza malengo madogo-madogo.

KWA NINI NI MUHIMU

Kufikia malengo kutakuwezesha ujiamini zaidi, uimarishe urafiki na wengine, na kufanya uwe na furaha zaidi.

Kujiamini: Unapojiwekea malengo madogo na kuyafikia, unapata ujasiri wa kufuatilia malengo makubwa zaidi. Pia, unapata ujasiri wa kukabiliana na changamoto za kila siku, kama vile kutoruhusu wengine wakushinikize kufanya mambo unayoamini kuwa si sahihi.

Urafiki: Watu hupenda kushirikiana na wale walio na malengo maishani, yaani, watu wanaojua kile wanachotaka na wanajitahidi kukipata. Kwa kuongozea, njia moja ya kuimarisha urafiki ni kushirikiana na mtu mwingine ili mfikie lengo fulani.

Furaha: Unapojiwekea lengo na kulifikia, unahisi vizuri kwamba umetimiza jambo.

“Ninapenda kujiwekea malengo. Yananiwezesha kuwa na mambo mengi ya kufanya na sikuzote kuwa na kitu ninachotaka kutimiza. Na unapofikia lengo lako, unahisi vizuri na kujiambia kwa shangwe, ‘Nimefanikiwa! Nimetimiza lengo langu.’”—Christopher.

KANUNI YA BIBLIA: “Anayeangalia upepo hatapanda mbegu, na anayetazama mawingu hatavuna.”—Mhubiri 11:4.

MAMBO YA KUFANYA

Chukua hatua zifuatazo ili ufanikiwe kujiwekea malengo na kuyatimiza.

Teua. Andika orodha ya malengo unayotaka kuyafikia kuanzia la kwanza, la pili, la tatu, na kuendelea.

Panga. Katika kila lengo, fanya mambo yafuatayo:

  • Jiwekee muda hususa unaotosha kukamilisha lengo lako.

  • Panga hatua utakazochukua ili kufikia lengo hilo.

  • Fikiria changamoto unazoweza kukabili, na upange jinsi utakavyozishughulikia.

Tenda. Usisubiri hadi uwe na kila kitu ili kuanza kufuatilia lengo lako. Jiulize hivi, ‘Ni jambo gani la kwanza ninalopaswa kufanya ili nifikie lengo langu?’ Kisha chukua hatua. Chunguza maendeleo yako kila unapopiga hatua.

KANUNI YA BIBLIA: “Mipango ya wenye bidii hakika huleta mafanikio.”—Methali 21:5.