Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Georgette Douwma/​Stone via Getty Images

JE, DUNIA YETU ITAOKOKA?

Bahari

Bahari

BAHARI hutokeza chakula tunachokula na vitu tunavyohitaji ili kutengeneza dawa. Bahari zetu huzalisha zaidi ya nusu ya oksijeni iliyo duniani, na hufyonza gesi ya kaboni inayotokana na shughuli za wanadamu. Kwa kuongezea, bahari hudhibiti hali ya hewa.

Kwa Nini Tunahitaji Kulinda Bahari Zetu

Mabadiliko ya hali ya hewa huathiri matumbawe, samaki gamba, na viumbe wengine baharini. Wanasayansi wanatabiri kwamba karibu matumbawe yote—yanayotegemeza angalau robo ya viumbe wote wanaojulikana kuwa baharini—yako katika hatari ya kutoweka ndani ya miaka 30 ijayo.

Wataalamu wanakadiria kwamba karibu asilimia 90 ya ndege wanaopata chakula chao kutoka baharini, wamekula plastiki, na inasemekana kwamba kiwango cha plastiki kilicho baharini huua mamilioni ya viumbe baharini kila mwaka.

Katika mwaka wa 2022, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alisema hivi: “Tumeacha kuithamini bahari na leo tunakabili kile ambacho ninaweza kukiita kuwa ‘Hali ya Dharura Katika Bahari.’”

Dunia Yetu Imeumbwa Ikiwa na Uwezo wa Kuokoka

Bahari isipochafuliwa na wanadamu, ina uwezo wa kujisafisha na kudumisha uhai wa viumbe walio ndani yake. Kitabu Regeneration: Ending the Climate Crisis in One Generation kinasema kwamba bahari isipochafuliwa na viwanda vya wanadamu, “ina uwezo wa asili wa kujisafisha yenyewe.” Fikiria mifano michache:

  • Miani humeng’enya na kuhifadhi kaboni dioksidi—hewa inayoaminiwa kusababisha kuongezeka kwa joto duniani. Miani pekee huhifadhi kiwango cha kaboni dioksidi kinachokaribia kile kinachohifadhiwa na miti, majani, na mimea mingine inayopatikana duniani.

  • Bakteria hula samaki waliokufa ambao huenda wangeichafua bahari. Kisha bakteria hao huliwa na viumbe wengine wa baharini. Kulingana na Smithsonian Institution Ocean Portal, utaratibu huo “hudumisha bahari ikiwa safi na maridadi.”

  • Viumbe wengi wa baharini hutumia mifumo yao ya kumeng’enya ili kubadili maji ya bahari yenye asidi—yanayoathiri matumbawe, samaki gamba, na viumbe wengine —na kuwa maji ya chumvi yanayofaa.

Hatua Zinazochukuliwa Sasa

Tukitumia mifuko na chupa za maji tunazoweza kutumia zaidi ya mara moja, tunaweza kupunguza kiasi cha takataka za plastiki baharini

Takataka zisizoingia baharini hazihitaji kusafishwa. Hivyo, wataalamu wanawashauri watu kutumia tena mifuko, vifaa, na vyombo badala ya kutumia vifaa vya plastiki mara moja na kuvitupa.

Lakini jitihada zinahitajika. Hivi karibuni, kwa kipindi cha mwaka mmoja, shirika moja linaloshughulika na kutunza mazingira lilikusanya tani 9,200 za takataka zilizotupwa kwenye fuo za bahari katika nchi 112. Hata hivyo, hiyo ni asilimia ndogo sana ikilinganishwa na takataka zote zinazoingia baharini kila mwaka.

Gazeti la National Geographic liliripoti kwamba “kuongezeka kwa asidi [katika bahari] kulikotokea kufikia sasa huenda kusiweze kurekebishwa.” Linaendelea kusema, “wanadamu wanatumia mafuta mengi sana hivi kwamba viumbe wa baharini hawawezi kudumisha bahari zikiwa safi kama walivyofanya zamani.”

Sababu za Kuwa na Tumaini—Biblia Inasema Nini

“Dunia imejaa vitu ulivyoumba. Kisha kuna bahari, ni kubwa sana na pana, imejaa viumbe walio hai wasio na idadi, wadogo kwa wakubwa.” —Zaburi 104:​24, 25.

Muumba wetu ameumba bahari na uwezo wake wa kujisafisha. Fikiria hili: Ikiwa anajua mambo yote kuhusu bahari na viumbe walio ndani yake, bila shaka anaweza kurekebisha madhara yanayosababishwa na wanadamu. Ona makala yenye kichwa “Mungu Anaahidi Kwamba Dunia Yetu Itaokoka,” katika ukurasa wa 15.