ULIMWENGU WENYE MISUKOSUKO
1 | Linda Afya Yako
KWA NINI NI MUHIMU?
Afya ya mtu inaweza kuathiriwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja na misukosuko au majanga.
-
Matatizo huwaletea watu mkazo, na mara nyingi mkazo usioisha husababisha matatizo ya afya.
-
Majanga yanaweza kusababisha mifumo ya afya kulemewa na kuzuia upatikanaji wa huduma za afya.
-
Majanga huathiri hali ya uchumi wa mtu na kufanya ashindwe kulipia huduma muhimu kama vile, chakula chenye lishe au huduma ya afya.
Unachopaswa Kujua
-
Ugonjwa mbaya na mkazo, unaweza kuathiri uwezo wako wa kufanya maamuzi hivi kwamba ukaanza kupuuza kufanya mambo yanayoweza kuboresha afya yako. Hilo linaweza kufanya uwe mgonjwa zaidi.
-
Usipotibiwa, afya yako itakuwa mbaya zaidi na huenda uhai wako ukawa hatarini.
-
Ukiwa na afya njema utaweza kufanya maamuzi mazuri unapokabili matatizo.
-
Hata uwe na hali gani ya kiuchumi, chukua hatua zinazofaa kulinda afya yako.
Unachoweza Kufanya Sasa
Kadiri inavyowezekana, mtu mwenye hekima hufikiria hatari anazoweza kukabili na kuchukua hatua zinazofaa ili kuziepuka. Unaweza kutumia ushauri huo inapohusu afya yako. Mara nyingi unaweza kupunguza hatari ya kupatwa na magonjwa kwa kudumisha usafi. Kinga ni bora kuliko tiba.
“Tumepunguza gharama ya kwenda kumwona daktari na kununua dawa kwa kudumisha usafi.”—Andreas. *
^ Baadhi ya majina katika gazeti hili yamebadilishwa.