Mwanzo 16:1-16
-
Hagari na Ishmaeli (1-16)
16 Sasa Sarai mke wa Abramu hakuwa amemzalia mtoto yeyote,+ lakini alikuwa na mtumishi Mmisri aliyeitwa Hagari.+
2 Basi Sarai akamwambia Abramu: “Sasa tafadhali! Yehova amenizuia nisizae watoto. Tafadhali, lala na mtumishi wangu. Huenda nikapata watoto kupitia yeye.”+ Kwa hiyo Abramu akasikiliza maneno ya Sarai.
3 Baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani kwa miaka kumi, Sarai mke wa Abramu akamchukua Hagari, mtumishi wake Mmisri na kumpa Abramu mumewe awe mke wake.
4 Basi Abramu akalala na Hagari, naye akapata mimba. Alipogundua kwamba ana mimba, alianza kumdharau bimkubwa wake.
5 Ndipo Sarai akamwambia Abramu: “Ni wewe uliyesababisha madhara ninayotendewa. Ni mimi niliyemweka mtumishi wangu mikononi mwako,* lakini alipogundua kwamba ana mimba, alianza kunidharau. Yehova na awe mwamuzi kati yangu na wewe.”
6 Basi Abramu akamwambia Sarai: “Tazama! Mtumishi wako yuko chini ya mamlaka yako. Mtendee lolote unaloona ni jema.” Kisha Sarai akamfedhehesha Hagari, naye akamkimbia.
7 Baadaye malaika wa Yehova akamkuta kwenye chemchemi ya maji nyikani, chemchemi iliyo njiani kuelekea Shuri.+
8 Naye akamuuliza: “Hagari, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi na unaenda wapi?” Ndipo akajibu: “Ninamkimbia Sarai, bimkubwa wangu.”
9 Basi malaika wa Yehova akamwambia: “Rudi kwa bimkubwa wako na ujinyenyekeze chini ya mkono wake.”
10 Kisha malaika wa Yehova akasema: “Nitawazidisha sana wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi sana wasiweze kuhesabiwa.”+
11 Malaika wa Yehova akaendelea kusema: “Sasa una mimba, nawe utazaa mwana, nawe unapaswa kumpa jina Ishmaeli,* kwa maana Yehova amesikia mateso yako.
12 Atakuwa mtu aliye kama pundamwitu.* Mkono wake utapigana na kila mtu, na mkono wa kila mtu utapigana naye, naye atakaa akielekeana na ndugu zake wote.”*
13 Ndipo akaliitia jina la Yehova, aliyekuwa akizungumza naye: “Wewe ni Mungu anayeona,”+ kwa kuwa alisema: “Je, ni kweli kwamba nimemwona hapa yeye ambaye huniona?”
14 Ndiyo sababu kisima hicho kiliitwa Beer-lahai-roi.* (Kiko kati ya Kadeshi na Beredi.)
15 Basi Hagari akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwanawe ambaye Hagari alimzaa, Ishmaeli.+
16 Abramu alikuwa na umri wa miaka 86 Hagari alipomzaa Ishmaeli.
Maelezo ya Chini
^ Tnn., “kifuani pako.”
^ Maana yake “Mungu Husikia.”
^ Baadhi ya watu hudhani ni pundamilia. Yaelekea ametumiwa kurejelea mtazamo wa kujitegemea.
^ Au labda, “naye ataishi kwa uhasama na ndugu zake wote.”
^ Maana yake “Kisima cha Aliye Hai Ambaye Huniona.”