Kulingana na Mathayo 2:1-23

  • Wanajimu wamtembelea Yesu (1-12)

  • Kukimbilia Misri (13-15)

  • Herode awaua wavulana wadogo (16-18)

  • Kurudi Nazareti (19-23)

2  Baada ya Yesu kuzaliwa huko Bethlehemu+ ya Yudea katika siku za Mfalme Herode,*+ tazama! wanajimu* kutoka Mashariki walikuja Yerusalemu,  wakisema: “Yuko wapi yule aliyezaliwa awe mfalme wa Wayahudi?+ Kwa maana tuliiona nyota yake tulipokuwa Mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”*  Mfalme Herode aliposikia jambo hilo, yeye na watu wote huko Yerusalemu wakafadhaika.  Akawakusanya wakuu wote wa makuhani na waandishi wa watu na kuwauliza mahali ambapo Kristo* alipaswa kuzaliwa.  Wakamwambia: “Katika Bethlehemu+ ya Yudea; kwa maana nabii aliandika hivi:  ‘Na wewe, ewe Bethlehemu ya nchi ya Yuda, wewe si mji mdogo zaidi miongoni mwa magavana wa Yuda, kwa maana kutoka kwako atakuja kiongozi, atakayewachunga watu wangu Israeli.’”+  Ndipo Herode akawaita wale wanajimu kwa siri na kuhakikisha kwa uangalifu kutoka kwao wakati ambapo ile nyota ilionekana.  Akawatuma Bethlehemu na kuwaambia: “Nendeni mkamtafute kwa uangalifu huyo mtoto, na baada ya kumpata mniletee habari, ili mimi pia niende kumsujudia.”  Baada ya kumsikiliza mfalme, wakaondoka, na tazama! nyota waliyokuwa wameona walipokuwa Mashariki+ ikawaongoza mpaka iliposimama juu ya mahali alipokuwa yule mtoto. 10  Walipoiona ile nyota wakashangilia sana. 11  Walipoingia ndani ya nyumba wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake, wakapiga magoti na kumsujudia* mtoto. Pia, wakafungua hazina zao na kumpa yule mtoto zawadi—dhahabu, ubani, na manemane. 12  Hata hivyo, kwa sababu Mungu aliwaonya kupitia ndoto+ wasirudi kwa Herode, wakarudi nchini kwao kupitia njia nyingine. 13  Baada ya kuondoka, tazama! malaika wa Yehova* akamtokea Yosefu katika ndoto+ na kumwambia: “Simama, mchukue huyo mtoto na mama yake mkimbilie Misri, mkae huko mpaka nitakapokwambia, kwa maana Herode yuko karibu kumtafuta huyo mtoto ili amuue.” 14  Basi Yosefu akaamka usiku, akamchukua Maria pamoja na yule mtoto wakaenda Misri. 15  Wakakaa huko mpaka Herode alipokufa. Basi yakatimia maneno haya yaliyosemwa na Yehova* kupitia nabii wake: “Nikamwita mwanangu atoke Misri.”+ 16  Herode alipoona ameshindwa akili na wale wanajimu, akakasirika sana, akaamuru wavulana wote huko Bethlehemu na wilaya zake zote wauawe, kuanzia umri wa miaka miwili kwenda chini, kulingana na wakati aliokuwa amehakikisha kwa uangalifu kutoka kwa wale wanajimu.+ 17  Ndipo yakatimia maneno haya yaliyosemwa kupitia nabii Yeremia: 18  “Sauti ilisikika kule Rama, kilio na kuomboleza kwingi. Raheli+ akiwalilia watoto wake, naye hakutaka kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.”+ 19  Herode alipokufa, tazama! malaika wa Yehova* akamtokea Yosefu katika ndoto+ huko Misri 20  akamwambia: “Simama, umchukue mtoto na mama yake, nanyi mrudi katika nchi ya Israeli, kwa sababu wale waliotaka kumuua* mtoto wamekufa.” 21  Basi akaamka akamchukua mtoto na mama yake, wakarudi katika nchi ya Israeli. 22  Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa akitawala Yudea baada ya Herode baba yake, akaogopa kwenda huko. Zaidi ya hayo, alionywa na Mungu kupitia ndoto,+ basi akaenda katika eneo la Galilaya.+ 23  Akaenda kuishi katika jiji liitwalo Nazareti,+ ili kutimiza maneno haya yaliyosemwa kupitia manabii: “Ataitwa Mnazareti.”*+

Maelezo ya Chini

Angalia Kamusi.
Au “wataalamu wa nyota.”
Au “kumwinamia.”
Au “Masihi; Mtiwa-mafuta.”
Au “kumwinamia.”
Au “wakiitafuta nafsi ya.”
Inaelekea ni kutokana na neno la Kiebrania “chipukizi.”