Hamia kwenye habari

© Kim, Hyun-tae/iNaturalist. Licensed under CC-BY-4.0

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Mlio wa Chura wa Japani Anayeishi Kwenye Miti

Mlio wa Chura wa Japani Anayeishi Kwenye Miti

 Vyura wa kiume wa Japani wanaoishi kwenye miti wanafahamika kwa milio yao ya kujirudia-rudia inayoonekana kama haina upatano. Hata hivyo, mlio wa kila mmoja unaweza kutofautishwa hata wanapokuwa wengi sehemu moja. Nchini Japani, watafiti wanaochunguza vyura hao (hyla japonica) wamegundua kwamba milio hiyo inaweza kutofautishwa kwa sababu vyura wa kiume walio katika eneo hususa hutoa milio kwa njia yenye utaratibu wanapowaita vyura wa kike.

 Fikiria hili: Vyura wa kiume wa Japani wanaoishi kwenye miti hutoa sauti ili kuwavutia vyura wa kike. Sauti hiyo huanzia kwenye nyuzi zake za sauti kisha inakuzwa inapovumishwa kwenye kifuko cha sauti kilicho kwenye koo yake.

 Milio ya chura mmoja wa kiume inawezaje kutofautishwa na ile ya vyura wengine wa kiume? Watafiti wamegundua kwamba badala ya kutoa milio yao bila upatano, vyura wa Japani wanaoishi kwenye miti wanapokuwa karibu-karibu wanatoa milio kwa mfuatano fulani, kila chura akitoa sauti kwa zamu yake. Mpangilio huo mzuri husaidia sauti zao zipishane, na hivyo milio yao hufanyiza mfuatano mzuri wa sauti mbalimbali na hilo huwasaidia vyura hao wasitumie nguvu nyingi. Mbali na hilo, kufuata mpangilio huo huwawezesha vyura hao kupata nafasi ya kupumzika kidogo kabla ya kuendelea kutoa sauti.

 Mpangilio huo umewavutia sana watafiti katika kitengo cha mawasiliano yasiyotumia nyaya hivi kwamba wanatumia hisabati za kisasa kujaribu kuboresha mbinu za kuhamisha taarifa ili taarifa zinazohamishwa zisiingiliane. Njia hiyo itahakikisha taarifa zinahamishwa kwa usahihi na kupunguza matumizi ya nishati.

 Una maoni gani? Je, mbinu ya vyura wa Japani wanaoishi kwenye miti ya kutokeza milio kwa mpangilio wenye mfuatano mzuri ilijitokeza yenyewe? Au je, ilibuniwa?