Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Membe Anavyojitosa Baharini

Membe Anavyojitosa Baharini

 Membe ni ndege wakubwa wa baharini wanaojitosa baharini kwa mwendo wa kilomita 190 hivi kwa saa. Membe anapoyapiga maji, kishindo chake huwa zaidi ya mara 20 ya nguvu za uvutano. Membe wanafauluje kujitosa tena na tena kwa njia hiyo bila kufa?

 Fikiria hili: Kabla ya membe kujitosa ndani ya maji, yeye hurudisha mabawa yake nyuma na kufanyiza umbo la mshale. Pia anafunika macho yake kwa utando fulani wa kuyalinda na wakati huohuo anajaza hewa katika vifuko fulani vilivyo shingoni na kifuani vinavyomlinda anapogonga maji kwa nguvu.

 Membe anapojitosa ndani ya bahari, kinywa chake, kichwa, na shingo hufanyiza umbo la pia. Kufanyiza umbo hilo humsaidia membe kuelekeza kishindo cha kuyapiga maji kwenye misuli yake ya shingoni yenye nguvu. Membe hurekebisha lenzi ya macho yake na hivyo anafaulu kuona akiwa ndani ya maji mara moja.

 Membe anaweza kuingia umbali gani ndani ya maji? Mwendo anaotumia kujitosa baharini unaweza kumfikisha hadi kwenye kina cha mita 11 hivi, lakini anaweza kuendelea kuingia ndani zaidi kwa kupigapiga mabawa na miguu yake. Kwa kweli, membe fulani wameonekana wakifikia kina cha mita 25 ndani ya bahari. Wanapomaliza kupiga mbizi, membe huelea bila kutumia nguvu zozote hadi juu ya maji na kuruka tena.

 Tazama membe wakijitosa

 Watafiti walibuni membe wa kielektroni ili kuwasaidia katika jitihada za kutafuta na kuokoa maisha. Roboti hizo zilitazamiwa kuwa na uwezo wa kuruka, kujitosa majini, na kuruka tena. Hata hivyo, wakati wa majaribio, roboti moja ilivunjika-vunjika sehemu kadhaa kwa sababu ya kupiga maji kwa kishindo. Hilo liliwafanya watafiti hao wafikie mkataa kwamba uwezo wa roboti zao “hauwezi kulinganishwa na uwezo wa membe wa kujitosa baharini.”

 Una maoni gani? Je, uwezo wa membe wa kujitosa baharini ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?