Hamia kwenye habari

E+/IvanJekic via Getty Images

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa Kuelea wa Mbegu ya Shunga Pwapwa

Uwezo wa Kuelea wa Mbegu ya Shunga Pwapwa

 Mbegu za shunga pwapwa au za familia ya dandelion ni mojawapo ya vitu vyenye uwezo wa pekee wa kuelea hewani. Upepo unapopuliza, nyingi kati ya mbegu hizo huelea hewani kama tu parachuti. Licha ya kwamba zinaelea karibu na ardhi, baadhi ya mbegu hizo zinaweza kupeperushwa na upepo umbali wa kilometa moja au zaidi. Ni nini kinachozisaidia kuelea kwa muda mrefu hivyo? Wanasayansi wamegundua kwamba mbegu hizo zina uwezo wa kuelea ambao unazidi mara nne uwezo wa parachuti na pia mbegu hizo zina uwezo wa kustahimili upepo.

 Fikiria hili: Kila mbegu ina shina, na juu ya shina hilo kuna vinywele vingi ambavyo kwa ujumla vinaonekana kama mwamvuli, navyo vinaitwa pappus. Vinywele hivyo vinafanya kazi kama parachuti kwa kuwa vinasaidia mbegu kuendelea kuelea.

Watafiti fulani wanasema kwamba huenda mzunguko wa hewa juu ya vinywele vya mbegu za shunga pwapwa huisaidia mbegu isianguke haraka

 Hata hivyo, vinywele hivyo vinafanya mengi zaidi ya kusaidia mbegu kubaki ikiwa imeelea. Hewa inaweza kupita kati ya unywele mmoja na mwingine na pia kuzunguka vinywele na inapofanya hivyo inatokeza mzunguko wa hewa juu ya vinywele hivyo. Mzunguko huo wa hewa unaofanyizwa juu ya vinywele unatokeza shinikizo dogo la hewa na hilo linavuta mbegu nzima juu na kuifanya isianguke haraka.

 Tunaweza kusema kwamba vinywele hivyo vyenye mpangilio mzuri vinaiwezesha mbegu kuelea kama parachuti yenye matundu lakini yenye uwezo mkubwa zaidi na inayostahimili upepo. Kwa kuongezea, asilimia tisini ya pappus (sehemu yenye vinywele inayoonekana kama mwavuli) ni nafasi tupu. Kwa hiyo, vinywele vyenyewe hufanyiza sehemu ndogo sana ya mwavuli huo.

 Wanasayansi wanachunguza jinsi wanavyoweza kuiga uwezo wa kuelea wa mbegu za shunga pwapwa. Wanafikiria kutumia ustadi huo kutengeneza ndege ndogo ndogo ambazo hazibebi rubani. Ndege hizo zitaokoa nishati kwa kuwa zitatumia nishati kidogo sana au huenda zisitumie nishati kabisa. Ndege hizo zinaweza kutumiwa kwa njia nyingi kutia ndani kupima kiwango cha uchafuzi wa hewa.

 Mbegu za shunga pwapwa zikielea

 Una maoni gani? Je, uwezo wa kuelea wa mbegu ya shunga pwapwa ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?