Hamia kwenye habari

HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Crimea

Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao​—Crimea

Upinzani mkali unaoendelea nchini Urusi umeenea na kufika Crimea. Nchini Urusi serikali imefunga mashirika ya Mashahidi, na imeonyesha waziwazi kwamba imekusudia kuondoa kabisa ibada zozote zinazofanywa ingawa zinafanywa kwa amani. Tangu marufuku ya Aprili 2017, wenye mamlaka nchini Urusi wamewavamia Mashahidi wengi wanakokutanika pamoja nchini humo, na hivyo Mashahidi wengi wamekamatwa na kufungwa. Unyanyasaji wa aina hiyohiyo unaendelea dhidi ya Mashahidi wa Yehova huko Crimea.

Uvamizi wa kwanza mkubwa nchini Crimea ulifanyika Novemba 15, 2018, katika mji wa Dzhankoy. Polisi pamoja na wanajeshi waliokadiriwa kuwa kama 200 hivi walivamia nyumba nane ambamo vikundi vidogo vya Mashahidi vilikuwa vimekutanika ili kusoma na kuzungumzia Biblia. Maofisa 35 hivi waliofunika nyuso zao na waliokuwa na bunduki mikononi walivamia nyumba ya Sergey Filatov, ambako Mashahidi sita walikuwa wamekutania. Mashahidi hao waliingiwa na hofu sana kwa sababu ya uvamizi huo wa kikatili. Wavamizi hao walimsukuma na kumbana mwanamume fulani mwenye umri wa miaka 78 ukutani, wakamlazimisha alale chini na kumfunga pingu, kisha wakampiga vibaya hivi kwamba ilibidi apelekwe hospitalini. Wanaume wengine wawili wenye umri mkubwa walishtuka sana hivi kwamba wakalazimika kukimbizwa hospitali kwa sababu ya shinikizo la damu mwilini lilikuwa limepanda juu. Inasikitisha kwamba mwanamke mmoja aliyekuwa mjamzito alipovamiwa nyumbani kwake aliingiwa na hofu hadi mimba yake ikatoka.

Baada ya uvamizi huo, Bw. Filatov alifunguliwa mashtaka ya uhalifu chini ya Kifungu 282.2(1) cha Sheria ya Uhalifu ya Urusi kwa kosa la kupanga shughuli za “shirika lenye msimamo mkali.” Machi 5, 2020, mahakama ya wilaya huko Crimea ilimhukumu Bw. Filatov kifungo cha miaka sita katika gereza la wahalifu. Baada ya hukumu yake kutangazwa, alipelekwa gerezani moja kwa moja.

Baada ya msako uliofanywa Dzhankoy mwaka wa 2018, maofisa wa polisi wamekuwa wakiendelea kuvamia nyumba za Mashahidi wowote wanaodhaniwa kwamba wanashiriki katika utendaji wa shirika lenye msimamo mkali. Msako wa karibuni zaidi ulifanyika Mei 22, 2023. Saa 12:30 asubuhi, zaidi ya maofisa kumi, watano wakiwa wamebeba silaha, walivamia nyumba moja mjini Feodosia. Maofisa hao waliwaamuru Mashahidi walale sakafuni na wakaanza kuipekua nyumba hiyo, zoezi hilo liliendelea kwa saa tatu. Ndugu mmoja aliwekwa kuzuizini kisha akapelekwa jijini Sevastopol akahojiwe.

Kwa sababu ya misako hiyo, kesi za uhalifu zimekuwa zikifunguliwa na hukumu kutolewa, na sasa wanaume tisa ambao ni Mashahidi wanatumikia vifungo vya mpaka miaka sita na nusu gerezani. Wote hao wameshtakiwa kwa madai ya kuendeleza utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.

Mfuatano wa Matukio

  1. Septemba 17, 2024

    Kwa sasa, Mashahidi tisa wa Yehova wako gerezani Crimea.

  2. Mei 22, 2023

    Maofisa wa usalama wavamia nyumba ya Shahidi mjini Feodosia. Wanachukua vifaa vyao vya kielektroni na Shahidi mmoja awekwa kizuizini.

  3. Agosti 5, 2021

    Nyumba nane za Mashahidi zafanyiwa msako. Aleksandr Dubovenko na Aleksandr Litvinyuk wakamatwa.

  4. Oktoba 1, 2020

    Nyumba tisa zinavamiwa katika eneo la Sevastopol. Igor Shmidt anakamatwa na kuwekwa mahabusu.

  5. Juni 4, 2019

    Maofisa wa kikosi maalumu wavamia nyumba kumi jijini Sevastopol. Bw. Stashevskiy ahukumiwa kwa kupanga utendaji wa kikundi chenye msimamo mkali.

  6. Machi 20, 2019

    Maofisa wa FSB wavamia nyumba nane huko Alupka na Yalta. Bw. Gerasimov ahojiwa na baadaye kushtakiwa kwa kupanga utendaji wa kikundi chenye msimamo mkali.

  7. Novemba 15, 2018

    Kwenye mji wa Dzhankoy, nyumba nane kutia ndani nyumba ya Bw. Flatov zilivamiwa na watu zaidi ya 200 ambao ni polisi walioambatana na wanajeshi.